ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 3, 2018

Afrika Mashariki yaweka rekodi kiuchumi

NCHI za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), zimeweka rekodi ya ukuaji kiuchumi mwaka 2017 kwa wastani wa pato la taifa wa asilimia 5.9, tofauti na wastani wa bara la Afrika wa asilimia 3.6.

Mafanikio hayo yamekuja katika mwaka ambao kulikuwa na matumaini madogo ya kufanya vizuri kiuchumi kutokana dalili kuonesha kungekuwa na hali mbaya. Katika mwaka huo, kampuni katika nchi nyingi zilionekana kuyumba na hata kupunguza wafanyakazi, benki zilipata wakati mgumu kukopesha, kulikuwa na gharama kubwa za maisha, mambo ambayo kwa ujumla yalitoa taswira mbaya kiuchumi. Kwa mujibu wa Taarifa ya Kiuchumi ya Afrika Mashariki mwaka 2018 iliyotolewa na Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) hivi karibuni inaonesha kuwa, ukuaji kiuchumi kwa EAC iliongozwa na Rwanda na Kenya.

“Katika ukuaji wa uchumi, ukuaji ulitokana na matumizi binafsi ya ndani, uwekezaji katika miundombinu, ukuaji katika sekta ya kilimo na ongezeko la viwanda vidogo na kadhalika,” imesema sehemu ya taarifa hiyo. Ukuaji unatabiriwa kuongezeka kwa miaka miwili zaidi hadi kufikia asilimi 6.2 ifikapo mwakani, huku Tanzania, Rwanda na Kenya zikitajwa kuwa vinara katika ukuaji.

Kisekta, ukuaji wa uchumi umetajwa kuongoza na kilimo ambacho kimechangia pato la taifa katika nchi nyingi, lakini pia ajira. Kilimo kimetajwa kuchangia asilimia 41 ya pato la katika katika nchi za Afrika Mashariki. “Hali iko hivyo Ethiopia, Rwanda na Tanzania, hizi ni nchi zinazonufaika na kilimo. Kama hali hii ikiendelea, Afrika Mashariki itakua kwa kasi katika viwanda vidogo, ukuaji wa miji na shughuli nyingine nje ya sekta ya kilimo,” imesema taarifa hiyo.

Uwekezaji katika miradi ya miundombinu, uchimbaji madini na ujenzi pia vimetajwa kuchangia ukuaji kutokana na kuimarika kwa sekta hizo. Mambo hayo matatu yanatarajiwa kuibeba Afrika Mashariki katika mwaka huu, hivyo kufungua zaidi mipaka ya ukuaji kiuchumi hadi katika kanda nyingine ikiwemo Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA).

HABARI LEO

No comments: