ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, April 3, 2018

Kampala latajwa jiji bora kuishi, kufanya kazi EAC

UTAFITI uliofanywa na taasisi moja isiyo ya kiserikali ya nchini Marekani ya Consultancy Mercer, imesema Jiji la Kampala ni jiji bora kwa kuishi na kufanya kazi katika nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).

Utafiti huo uliopewa jina la ‘Utafiti wa Ubora wa Maisha 2018’ umelitaja jiji la Nairobi nchini Kenya kushika nafasi ya pili kwa ubora wa kuishi na kufanya kazi kati ya majiji ya mataifa sita ya Afrika Mashariki.

Katika utafiti uliofanywa na taasisi hiyohiyo mwaka 2017, jiji la Kampala linaonekana kuimarika katika nafasi yake kidunia. Mwaka jana Kampala ilishika nafasi ya 173 wakati mwaka huu imeshika nafasi ya 172.

Jiji la Nairobi limeendelea kushikilia nafasi yake ya mwaka jana ambapo kati ya majiji 231, Nairobi imeendelea kushika nafasi ya 186 ile ile iliyoshika mwaka jana. Jiji la tatu kwa ubora wa kuishi na kufanya kazi Afrika Mashariki limetajwa kuwa ni Kigali ambao ni Mji mkuu wa Rwanda.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kigali imeimarika kutoka nafasi ya 192 mwaka jana hadi kushika nafasi ya 190 mwaka huu. Nafasi ya nne katika nchi za Afrika Mashariki inashikiliwa na jiji la kibiashara la Dar es Salaam nchini Tanzania ambalo utafiti unaonesha kuwa limeshikilia nafasi ile ile ya 199 kati ya 231 iliyoshika katika utafiti wa mwaka jana. Vigezo vilivyotumika katika kufanya utafiti huo na hatimaye kupata washindi ni pamoja na usalama katika miji hiyo.

HABARI LEO

No comments: