Advertisements

Saturday, April 21, 2018

Aliyemtukana Rais Magufuli Ahukumiwa Miaka Mitatu Jela

Wakili wa Kujitegemea Leonard Kyaruzi amehukumiwa kulipa faini ya Sh. 5,000,000  au kwenda jela miaka mitatu.
 
Alikutwa na hatia ya kumkashifu Rais wa Jamhuri ya Muungano Tanzania, Dk. John Magufuli kwa kumwita Zuzu.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi Godfrey Mwambapa, baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi wanne wa Jamhuri na utetezi wa mshtakiwa.

Katika hukumu hiyo, hakimu aliegemea katika maelezo yake ya onyo ambayo yamepita bila kupingwa kama kielelezo cha upande wa Jamhuri mahakamani hapo.

"Mahakama hii bila kuacha shaka imepitia ushahidi wa mashahidi wanne wa upande wa Jamhuri, imekuona una hatia, utalipa faini ya Sh. milioni tano ukishindwa utakwenda jela kutumikia kifungo cha miaka mitatu," alisema hakimu Mwambapa.

Katika kesi ya msingi, ilidaiwa kuwa Juni 2, 2016 katika jengo la Tanzanite lililopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam,  mshtakiwa alichapisha taarifa kwenye mtandao wa Whatsapp kwa lengo la kumkashifu Rais Magufuli.


Ilidaiwa kuwa mshtakiwa alichapisha taarifa kwamba "Hivi huyu Pombe ni kwamba hana washauri? Hashauriki? Au zuzu? Bwege sana huyu jamaa, he doesn't consider the law in place before opening his mouth! Au na yeye anaumwa ugonjwa wa Mnyika" alinukuliwa mshtakiwa.

No comments: