Polisi wamemkamata mwanamke wa kijiji cha Sokoni wilayani Tarime, kwa kumuua mtoto wake wa miaka minane kwa kumpiga na mwiko.
Kamanda wa polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo lilitokea Machi 25 .
Mwaibambe alisema chanzo ni baada ya mtoto Debora Jomo kula chakula ambacho mama yake alikiandaa kwa ajili ya kula mdogo wake ambaye ni mgonjwa.
Alisema mtoto huyo alifariki dunia Machi 26 saa 11:00 asubuhi kutokana na kutopelekwa hospitalini.
‘’Inasikitisha sana kuona mama anaua mtoto wake tena wa kumzaa mwenyewe, mtoto alitoka shuleni akakuta chakula alikuwa na njaa na alijua aliachiwa akala,” alisema.
Naye diwani wa Sirari, Paul Nyangoko aliwataka wazazi kuangalia adhabu za kuwapa watoto kwa kuwa vipigo vikali vinaathiri afya ya mtoto na kumsabaibishia kifo.
Alisema kwenye kata yake hakuna njaa na debe la mahindi linauzwa kwa Sh7,000.
No comments:
Post a Comment