ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, April 4, 2018

Mbowe, wenzake waachiwa kwa dhamana

Tokeo la picha la mbowe waachiwa
BAADA ya kukaa mahabusu gereza la Segerea kwa siku saba, viongozi sita wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) akiwemo Mwenyekiti wa Taifa, Freeman Mbowe wameachiwa kwa dhamana.

Waliachiwa jana na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, baada ya kukidhi masharti ya dhamana waliyopewa wiki iliyopita. Mbunge wa Kawe, Halima Mdee aliunganishwa na washitakiwa hao sita wa awali na kufanya jumla yao kuwa watu saba.Kwa pamoja wanakabiliwa na mashitaka tisa, ikiwemo ya kufanya mkusanyiko usio halali, uliosababisha kifo cha mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Akwilin, hivi karibuni.

Washitakiwa wengine ni Katibu Mkuu wa Chama hicho, Dk Vicent Mashinji, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema (Zanzibar), Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu (Tanzania Bara) na Mbunge wa Kibamba, John Mnyika. Washitakiwa wengine ni Mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa na Mbunge wa Tarime Mjini, Ester Matiko. Wote walikana mashitaka. Hakimu Mkazi Mkuu, Wilbard Mashauri alimtaka kila mshitakiwa kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini bondi ya Sh milioni 20 na wanaopaswa kuwa na barua za utambulisho kutoka katika taasisi yoyote inayotambulika.

Pia aliwataka washitakiwa hao, kuripoti mara moja kwa wiki (Ijumaa) katika Kituo Kikuu cha Polisi; na wadhamini wahakikishe washitakiwa hao, wanafika mahakamani kila wanapoitwa. Baada ya Mdee kuunganishwa na washitakiwa wenzake, upande wa mashitaka ulipinga dhamana kwamba mshitakiwa huyo, amekuwa akipewa dhamana na hakidhi matakwa hayo. Wakili wa Serikali Mkuu, Dk Zainabu Mango alidai Mdee alipewa dhamana na Polisi ya kuripoti kituoni, lakini alishindwa kuhudhuria mara tatu, Machi 15, 22 na 25, mwaka huu.

Pia waliomba kama Mahakama itatoa dhamana, utekelezaji wake uzingatie vigezo vya lazima kwa mujibu wa sheria, kwa kutoa maelekezo ya kutoa hati ya kusafiria na kuzuia safari zisizo na lazima. Akijibu hoja hizo, Wakili wake, Kibatala alidai Mahakama haiwezi kutoa maamuzi ya hisia za mawakili, kwani hawana hati za kiapo, kuthibitisha kuwa Mdee aliruka masharti. “Mshitakiwa ana wadhamini wanaoaminika hivyo Mahakama itoe masharti yanayofanana na ya awali kwani Mahakama kutaka washitakiwa kuripoti mara moja kwa wiki Polisi inawaumiza lakini ina maslahi kwa wote,” alidai Kibatala.

Hakimu Mashauri alimtaka Mdee kuwa na wadhamini wawili, watakaosaini bondi ya Sh milioni 20 kila mmoja na kuripoti kituo cha Polisi mara moja kwa wiki kama wenzake. Wadhamini 14 waliweza kuwadhamini washitakiwa hao, ambao kwa pamoja walisaini hati za mahakama kama kumbukumbu. Akisoma mashitaka hayo upya, Wakili wa Serikali Mwandamizi, Faraja Nchimbi alidai washitakiwa kwa pamoja walitenda makosa hayo Februari 16, mwaka huu maeneo ya Viwanja vya Buibui na Barabara ya Kawawa, Mkwajuni wilayani Kinondoni, Dar es Salaam.

Nchimbi alidai katika mashitaka ya kwanza ya kufanya mkusanyiko usio halali kinyume na sheria, Februari 16, mwaka huu, katika Barabara ya Kawawa, Mkwajuni wilayani Kinondoni Dar es Salaam, wakiwa wamekusanyika kutekeleza lengo la pamoja, waliendelea katika mkusanyiko huo na kufanya watu waogope kwamba watakwenda kusababisha uvunjifu wa amani.

Pia alidai Februari 16, mwaka huu katika Barabara ya Kawawa eneo la Mkwajuni wilayani Kinondoni Dar es Salaam, wakiwa wamekusanyika wao na wenzao 12 ambao wamefikishwa mahakamani, wakiwa kwenye maandamano na pasipo kuzingatia agizo lililotolewa na Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Gerald Ngiichi, waligoma na kuendelea na maandamano na kusababisha kifo cha Akwilina na majeruhi kwa askari wawili, Konstebo wa Polisi, H 7856 Fikiri na E 6976 Rahim Msangi. Mashitaka ya tatu, ilidaiwa Februari 16, mwaka huu viwanja vya Buibui wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Mbowe akihutubia wananchi wa jimbo hilo alihamasisha chuki isivyo halali.

HABARI LEO

No comments: