
Dodoma. Serikali imemuomba mbunge wa Kawe (Chadema), Halima Mdee kutoa elimu kwa wananchi waliovamia shamba la Somji ili wakubali kufanya mazungumzo yatakayowezesha kufanyika kwa malipo ya fidia stahiki kwa mmiliki wa shamba hilo ili wao warasimishwe maeneo hayo.
Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angelina Mabula amesema kama suala hilo litashindikana, Serikali itatoa uamuzi kama ilivyotolewa na mahakama kuwa wananchi wa eneo hilo ni wavamizi.
Mabula ametoa kauli hiyo leo Jumatano Aprili 4, 2018 wakati akijibu swali la Mbunge Mdee ambaye alitaka kujua kuhusu mgogoro katika eneo la eka 357.5 Boko Dovya kati ya wananchi na wamiliki halali wa eneo hilo.
“Je hatua gani zimeanza kuchukuliwa ili kero hiyo ya muda mrefu iweze kumalizika na wananchi waendelee na shughuli zao,” amehoji Mdee.
Swali hilo namba 17 liliulizwa kwa niaba yake na mbunge wa Liwale (CUF), Zuberi Kuchauka kutokana na Mdee kutokuwepo bungeni.
Mabula amesema awali shamba hilo lilikuwa na ukubwa wa eka 366 Mbweni (maarufu kama Somji Farm) ambalo lilipimwa E7/37F na kupewa namba 10917 Agosti 15,1958 na kumilikiwa kwa Hussein Somji na Munaver Somji mwaka 1961 ambapo walipewa hati namba 14573 ya umiliki wa miaka 99.
“Sehemu ya shamba hilo ekari 8.5 zilitwaliwa kwa matumizi mahususi ya Serikali mwaka 1975 na sehemu iliyobaki ilitwaliwa mwaka 2002 kwa ajili ya mradi wa viwanja 20,000 lakini wamiliki walifungua kesi mahakamani kupinga eneo lao kutwaliwa,” alisema Mabula.
Kuhusu wavamizi amesema wizara imekutana nao pamoja na uongozi wa wilaya ya Kinondoni kwa lengo la kuweka utaratibu utakaowezesha wamiliki wa awali kulipwa fidia stahiki kwa fedha itakayopatikana kutoka kwa wananchi waliovamia ili kurasimishwa maeneo waliyojenga lakini wananchi hao wameonyesha kutokuwa tayari kuchangia gharama hizo.
No comments:
Post a Comment