Advertisements

Monday, April 16, 2018

Ukuta wadondoka na kuua mtoto Dar

Mtoto mmoja aliyefahamika kwa jina la Nasra Ally (9) amefariki dunia na wengine sita kujeruhiwa baada ya kuangukiwa na ukuta usiku wa kuamkia leo Jumatatu, Aprili 16.
Tukio hilo limetokea katika Mtaa wa Kinzinga pembezoni mwa mto Kizinga kata ya Kijichi jijini Dar es Salaam.
Diwani wa kata hiyo Eliasa Mtalawanje amesema Nasra na wenzake walihifadhiwa katika nyumba hiyo kutokana na nyumba za wazazi wao kujaa maji yaliyotokana na mvua zinazoendelea kunyesha.
Amesema hadi sasa nyumba 50 zimejaa maji hali iliyosababisha wengine kulala nje wakilinda mali zao.
"Vitu vingine wamefanikiwa kuviokoa lakini vingine vimeharibika, mimi naomba wawe wavumilivu hasa katika kipindi hiki na waishi kwa tahadhari zaidi," amesema.
Baba mzazi wa marehemu Ally Abeid amesema walisikia kishindo kikubwa huku baadhi ya kinamama kupiga kelele kuashiria kwamba kuna hatari.
"Sisi tulikuwa huku bondeni, kwa sababu tangu juzi tunalala nje, tulivyofika tulikuta ukuta umebomoka na watoto sita wakiwa nje lakini kati yao wa kwangu hakuwepo," amesema huku akinyoosha mikono kumshukuru Mungu.
Amesema kwa sasa mwili umepelekwa katika hospitali ya Temeke na taratibu za mazishi zinaendelea.

Chanzo: Mwananchi

No comments: