Advertisements

Wednesday, May 16, 2018

BALOZI WA INDONESIA AAHIDI KUWAALIKA WAWEKEZAJI WA VIWANDA VYA NGUO, NGOZI NA MBOLEA KUWEKEZA SIMIYU

 Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede (wa tatu kulia) akipewa maelezo juu ya hatua za utengenezaji wa kiatu cha ngozi wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi kilichopo Senani wilayani Maswa akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu.
 Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede  akiweka saini katika ubao kwa kutumia Maswa Chalks wakati alipotembelea kiwanda cha kutengeneza Chaki  wilayani Maswa akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu.
 Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede (wa tatu kushoto) akiwa na viongozi wengine wa mkoa wa Simiyu wakati alipotembelea kiwanda cha kuchambua Pamba cha Kasoli Alliance kilichopo wilayani Bariadi akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu.
 Meneja mkuu wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola(kushoto) akitoa maelezo kwa Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede( wa nne kushoto) wakati alipotembelea kiwanda hicho,  kilichopo wilayani Bariadi akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu
 Mkuu wa Wilaya ya Maswa, mhe. Dkt. Seif Shekalaghe ( wa pili kulia) akitoa maelezo ya namna chaki zinavyotengenezwa kwa Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede  (kulia) wakati alipotembelea kiwanda cha chaki,  kilichopo wilayani Maswa akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu.
 Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka(kulia) akiteta jambo na Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede wakati wa ziara yake katika wilaya ya Maswa mkoani humo Mei, 15 mwaka huu.
 Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Mhe. Dkt. Seif Shekalaghe (kulia), Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede(katikati) na Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe.Anthony Mtaka wakionesha boksi la Chaki za Maswa(Maswa Chalks) wakati wa ziara ya Balozi huyo katika kiwanda cha kutengeneza Chaki wilayani humo.
 Meneja Mkuu wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola(kulia) akitoa maelezo kwa Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede( wa nne kushoto) wakati alipotembelea kiwanda hicho,  kilichopo wilayani Bariadi akiwa katika ziara yake Mkoani Simiyu.
 Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Simiyu, Mhe. Enock Yakobo akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Senani Wilaya ya Maswa wakati wa ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede katika kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi wilayani humo, akiwa katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.
 Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Mhe. Lucas Mwaniyuki akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Senani Wilaya ya Maswa wakati wa ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede katika kiwanda cha kuchakata bidhaa za ngozi wilayani humo, akiwa katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.
Kikundi cha Ngoma ya Asili cha Wagoyangi cha Wilaya ya Maswa kikitumbuiza wakati wa ziara ya Balozi wa Indonesia hapa nchini, Prof. Dkt. Ratlan Pardede wilayani humo, akiwa katika ziara ya siku nne Mkoani Simiyu.



Na Stella Kalinga, Simiyu
Balozi wa Indonesia hapa nchini Prof.Dkt. Ratlan Pardede amewaahidi viongozi wa Mkoa wa Simiyu kuwa atawaalika wawekezaji wa Viwanda vya nguo, viwanda vya kuchakata ngozi  na viwanda vya kutengeneza  mbolea kutoka nchini Indonesia kuja kuwekeza Mkoani Simiyu.

Mhe. Balozi Pardede ameyasema hayo Mei 15, alipokuwa katika ziara yake Mkoani Simiyu mara baada ya kutembelea kiwanda cha Kuchambua pamba cha Kasoli Alliance kilichopo Wilayani Bariadi na Kiwanda cha kuchakata ngozi cha Senani wilayani Maswa.

Amesema atawaalika wafanyabiashara kutoka nchini Indonesia kuja Simiyu ili wakutane na viongozi wa mkoa huo pamoja na wafanyabiashara wenzao kujadili juu ya kuongeza uzalishaji wa pamba bora, bei ya pamba na kuona namna ya kuuza pamba ya Simiyu (Tanzania) nchini Indonesia moja kwa moja.

Pamoja na kuahidi kuwaalika wawekezaji wa viwanda vya kuchakata bidhaa za ngozi, Balozi Pardede akiwa katika kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi cha Senani Maswa ameahidi kusaidia kuleta wataalam kutoka Indonesia watakaosaidia wafanyakazi wa kiwanda kutengeneza bidhaa bora za ngozi na kuwapeleka wafanyakazi hao Indonesia kujifunza na kupata maarifa na uzoefu.

Meneja mkuu wa Kiwanda cha kuchambua pamba cha Alliance Bw. Boaz Ogola amesema ujio wa Balozi wa Indonesia ni fursa kubwa kwa wanunuzi wa pamba kutokana na nchi hiyo kuwa na uhitaji mkubwa wa pamba kwa ajili ya viwanda vya nguo na utafungua milango ya majadiliano na wafanyanyabiashara wa Indonesia na kufanya biashara ya moja kwa moja.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Simiyu, Mhe. Anthony Mtaka amesema wamezungumza na Mhe.Balozi kumuomba awaalike wafanyabiashara wa Indonesia Mkoani humo kuwekeza kwenye viwanda vya kuchakata ngozi, ili viwanda vidogo vilivyopo na vitakapojengwa viwanda vikubwa uwekezaji wake uanze na malighafi kutoka ndani ya mkoa.

Aidha, Mtaka amesema Simiyu kama mkoa unaojihusisha na kilimo na unaopakana na mikoa inayofanya shughuli za kilimo unaona ipo haja ya kuwa na wawekezaji wanaotengeneza mbolea jambo ambalo limepokelewa na Mhe. Balozi na kuahidi kulifanyika kazi kwa kuwaalika wawekezaji.

“Tumezungumza na Mhe. Balozi na ameona uhitaji na umuhimu wa kuwakaribisha wawekezaji kulingana na mkoa jinsi ulivyo, jambo hili la kupata wawekezaji kwenye uzalishaji wa mbolea lipo pia katika mwongozo wetu wa uwekezaji kwa ajili ya kusaidia mikoa inayotuzunguka kama sehemu ya kuboresha eneo la kilimo” alisema.

Wakati huo huo Mtaka amesema wamezungumza na Mhe. Balozi kuona uwezekano wa Mkoa wa Simiyu kuwa mwenyeji kufanya mkutano wa Wizara ya Kilimo ya Indonesia na Wizara ya kilimo ya Tanzania mkoani Simiyu ambao unatarajia kufanyika mwezi Septemba mwaka huu.

Mhe.Balozi alipata nafasiya kutembelea kiwanda cha Chaki wilayani Maswa, ambapo Mkuu wa Mkoa amesema Serikali imetoa shilingi bilioni 8.2 kwa ajili ya upanuzi wa kiwanda hicho na ujenzi wa kiwanda cha vifungashio, hivyo akawataka vijana wanaofanya kazi katika kiwanda hicho kufanya kazi kwa bidii ambapo amewahakikishia kuwa baada ya upanuzi wa kiwanda hicho watakuwa waajiriwa wa kudumu.

Mhe. Balozi bado anaendelea na ziara yake mkoani Simiyu ambapo amepata nafasi ya kutembelea kiwanda cha kuchambua pamba Kasoli Alliance, Kiwanda cha kutengeneza bidhaa za ngozi na kiwanda cha chaki wilayani Maswa.

No comments: