Advertisements

Tuesday, May 8, 2018

CSI WAHIMIZA USHIRIKIANO ILI KUPUNGUZA VIFO VITOKANAVYO NA UZAZI, WAELEZEA UMUHIMU WA WAKUNGA KATIKA KUTOA HUDUMA ZENYE HESHIMA

Na Said Mwishehe, Globu ya jamii
SHIRIKA la Childbirth Survival International (CSI) limesema ipo haja kwa wakunga wote nchini kutoa huduma yenye heshima kwa mama mjazito ili ajifungue salama huku likitoa ombi kwa Serikali kuendelea kutoa fedha katika sekta ya afya kwa lengo la kupunguza vifo kwa mama wajawazito na watoto.
Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la CSI Stella Mpanda wakati anazungumza kwenye Maadhimisho ya Siku ya Wakunga Duniani ambapo kwa Tanzania maadhimisho hayo yalifanyika kitaifa mkoani Morogoro na kauli mbiu ilikuwa inasema "Ukunga ni chachu ya huduma bora kwa akina mama".


Amesema kutokana na kauli mbiu hiyo Shirika la CSI linaungana na wakunga wote nchini na duniani kwa ujumla kuhakikisha wakunga wanatoa huduma bora zenye ustadi kwa mama mjazito na lengo ni kuhakikisha mama anajifungua salama.

Mpanda amesema ili kupunguza vifo vya mama mjazito na watoto ni vema jamii ya Watanzania kwa pamoja wakashirikiana kwa kila mmoja kutimiza wajibu wake na kufafanua mashirika yanatakiwa kutimiza wajibu wao, Serikali na wananchi nao kutimiza wajibu wao na  kwa kufanya hivyo CSI inaamini vifo hivyo vitapungua.

Pia amezungumzia umuhimu wa jamii kutambua vidokezo hatari kwa mama mjazito ambavyo husababisha vifo iwapo atachelewa kwenda hospitali na kueleza vidokezo hivyo mama ,baba na wananchi wanapaswa kuvitambua kwani itasaidia katika kupunguza vifo hivyo vinavyotokea wakati wa kujifungua kwa baadhi ya akina mama.

Amefafanua Shirika la CSI kwa muda mrefu limekuwa likitoa mafunzo ya elimu ya uzazi salama kwa jamii ambapo pia wamekuwa na programu maalumu zinazolenga kuwajengea uwezo wakungwa ili watoe huduma bora na zenye ustadi wa hali ya juu na kusisitiza wataendelea na jukumu hilo kwani dhamira yao ni kuona vifo vitokanavyo na uzazi vinapungua au kwisha kabisa nchini na duniani kwa ujumla.

"CSI tumekuwa na jukumu la kutoa mafunzo kwa wakunga ili waendelee kutoa huduma bora.Pia tumekuwa tukitoa mafunzo kwa vijana na mabinti kuhusu stadi za maisha pamoja na jinsi ya kujilinda hasa kwa watoto wa kike ili wafikie malengo yao.

"Tunaamini tukiendelea kushirikiana katika eneo hili tutapunguza changamoto ambazo mama mjazito anazipitia wakati wa kujifungua.CSI tunalo jukumu la kuiona jamii ya Watanzania linapofika suala la uzazi linakuwa jambo lenye kufurahiwa na kila mmoja wetu badala ya kuibua hofu kwa jamii kwa kuwaza iwapo mama atajifungua salama au laa.Tutaendelea kushirikiana na Serikali na wadau wengine kuhakikisha tunapunguza vifo kwa mama wajawazito na watoto,"amesema Mama Stella Mpanda ambaye pia ni mwanzilishi wa CSI akishirikiana na Profesa Tausi Kagasheki.

No comments: