Advertisements

Monday, May 14, 2018

Dk Slaa ajitosa sakata la Sh1.5 trilioni

Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod
By Tausi Mbowe, Mwananchi tmbowe@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Balozi wa Tanzania nchini Sweden, Dk Wilbrod Slaa amejitosa katika mjadala wa Sh1.5 trilioni ulioibuka baada ya kutolewa kwa ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).

Sakata la Sh1.5 trilioni liliibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe ambaye alihoji kutoonekana kwa matumizi ya fedha hizo katika ripoti ya CAG, kama zilivyoidhinishwa na bunge.

Akizungumza kwa njia ya simu katika mahojiano maalumu na Mwananchi juzi, Dk Slaa ambaye alitangaza kuachana na siasa za vyama muda mfupi kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015, alisema kutoonekana kwa fedha hizo ni matokeo ya kanuni na mfumo uliopo katika Bunge ambao unaruhusu wabunge kupitisha bajeti hewa.

Alisema sheria ya fedha inaruhusu wabunge kupitisha bajeti za wizara bila kuwa na kiasi halisi na kiasi hicho kinawekwa mara tu baada ya fungu hilo kupatikana ama kwa wafadhili au mchakato mwingine wowote.

“Unaporuhusu katika vitabu vya bajeti yaani volume (Juzuu) 1, 2, 3 mpaka 4 kuwepo kwa neno ‘T’ au kuandikwa 100 ina maana hapo huna fedha na unatarajia kuzipata wakati bajeti hiyo ishapitishwa, hapo unawezaje kuhoji matumizi ambayo hukuyajua mapema?” Alihoji Dk Slaa.

Dk Slaa, ambaye alikuwa mbunge wa Karatu (Chadema) kuanzia mwaka 1995 mpaka 2010, alisema huo ni uzembe mkubwa unaofanywa na wabunge na kutoa mfano wa yeye akiwa mbunge aliwahi kukataa kupitisha bajeti ya wizara moja.

“Niligoma kupitisha bajeti ile, jambo lililosababisha aliyekuwa Spika wa Bunge hayati Samuel Sitta anisihi sana kwani hakukuwa na jinsi alisema hatuwezi jua maana wakati mwingine fedha za wafadhili zinachelewa hivyo zikija kipindi cha bajeti kinakuwa kimeshamalizika. Nililazimika kukubaliana naye hivyo hivyo, lakini mpaka leo sikubaliani na utaratibu huo,” alisema.

“Kama fedha nyingi zinatumika bila kupitishwa na Bunge kwa sababu ndiyo mfumo wetu uliopo unawezaje kuhoji fedha hizo zilitumikaje?” Alisisitiza Dk Slaa ambaye aligombea urais mwaka 2010 na kushika nafasi ya pili kwa kupata asilimia 27 ya kura zote.

Hata hiyo, Dk Slaa alisema kuwa huenda fedha hizo zilitumika katika ujenzi wa miradi moja kwa moja bila kufuata taratibu.

Dk Slaa, ambaye aliwahi kuwa katibu mkuu wa Chadema, alisema takwimu za miradi hasa mikubwa haziwezi kupatikana katika kipindi cha mwaka wa fedha wa Serikali kwani utekelezaji wake huwa unaendelea.

“Ndiyo maana hata taarifa za CAG haijadiliwi kipindi tu inapowasilishwa inabidi watendaji wapewe muda wa kwenda kujibu hoja ingawa haikatazwi kama kuna jambo limejitokeza mawaziri kutoa ufafanuzi.”

“Cha ajabu wabunge wetu sasa huwezi kumsikia akihoji na badala yake wanafanya vitu vingi kwa ushabiki tu. Siku hizi hakuna mtu anayekuja na hoja, matokeo wana-conclude (wanahitimisha) tu,” alisisitiza Dk Slaa.

Dk Slaa alijigamba kwamba wakati wake alikuwa hatoki hadharani hata siku moja bila kuwa na data.

“Nilikuwa nafanya utafiti na kama ni suala la kupambana na ufisadi nilihakikisha kila kitu nakipata ndiyo maana uliona wakati huo niliweza kuwachachafya baadhi ya mawaziri kwa kuwa nilikuwa sikurupuki,”alisema

Hata hivyo, Dk Slaa alisema jambo la msingi kwa wabunge wenyewe ni kuwa makini kusimamia fedha za bajeti ya maendeleo zinazopangwa kupelekwa katika maeneo yao.

“Kwanza siku zote fedha za maendeleo zinazopangwa katika wizara hazizidi hata asilimia 40, lakini wabunge wenyewe hawako makini katika kufuatilia fedha zinazopaswa kufika katika maeneo yao,”alisema.

Alisema anafahamu kwa jinsi gani wizi ulivyo mkubwa katika halmashauri mbalimbali huku baadhi ya miradi ikishindwa kutekelezwa kwa wakati, lakini wabunge wake au diwani ama hawaoni au hawana muda wa kufuatilia fedha hizo.

“Wabunge wanashindwa kufuatilia fedha zinazoenda katika maeneo yao hivyo kurahisisha ulaji kwa watu wasio na maadili,”aliongeza.

Dk Slaa, ambaye aliteuliwa kuwa balozi akiwa nchini Canada mara baada ya kutangaza kuachana na siasa za vyama, alipoulizwa anakumbuka nini katika siasa za Tanzania alisema hana anachokumbuka.

“Sina ninacho-miss nyumbani, sasa dunia ni kijiji kila kitu au taarifa yoyote ninayotaka kuipata naipata,” aliongeza.

Changamoto

Akizungumzia changamoto anazokutana nazo katika kazi yake mpya ya ubalozi, Dk Slaa alisema yeye kama balozi anayesimamia nchi tisa ikiwamo Sweden anapata wakati mgumu kutokana na taratibu za kidiplomasia.

Alisema mpaka sasa amepata utambulisho nchini Sweden tu, lakini bado barua yake ya utambulisho katika nchi nyingine nane hazijapokelewa hivyo kumlazimu kufanya kazi za nchi hizo akiwa Sweden.

Changamoto nyingine alisema ni upungufu wa watumishi katika balozi hizo.

SOMA ZAIDI-Dk Slaa awapa wapinzani mbinu kwa Rais Magufuli

No comments: