Advertisements

Friday, May 25, 2018

Hoja Ya Nape Yamliza Waziri Kama Mtoto

Hoja  ya Mbunge wa Mtama, Nape Nnauye (CCM), aliyoitoa Mei 16, wakati Bunge likijadili Bajeti ya Wizara ya Kilimo, imemfanya Waziri wa wizara hiyo, Dk. Charles Tizeba, kulia kama mtoto wakati akijitetea mbele ya Kamati ya Bunge ya Bajeti.


Katika hoja yake, Nape alishika shilingi ya mshahara wa waziri wakati Bunge lilipoketi kama kamati kupitisha bajeti hiyo, akihoji sababu za Serikali kutorudisha kwa wakulima fedha za kodi inayotozwa kwenye korosho wakati wa kusafirisha nje zao hilo (export levy), kama ambavyo sheria inataka.

Nape alisema kutokana na kutorudishwa kwa fedha hizo, bei ya dawa za kupulizia mikorosho zimepanda maradufu na sasa ndiyo wakati wa kupuliza dawa hizo vinginevyo zao hilo litavamiwa na wadudu.

 
“Itakumbukwa wakati tunapitisha bajeti ya kilimo, nilikamata shilingi kwa hoja ya fedha za export levy, kiti chako kiliagiza kamati ya bajeti ikutane na nikaahidi kama hatutaafikiana nitarudi hapa,” alisema Nape.

“Bahati mbaya tumekutana mara mbili Wizara ya Fedha; waziri, naibu waziri na kamishna wa fedha hawakuhudhuria.”

Nape alisema kwa sasa kuna ugonjwa unaoshambulia korosho na kwamba, bei ya salfa iliyotakiwa kuuzwa Sh16,000 sasa mfuko mmoja umefika Sh75,000, hivyo hakuna namna mkulima anaweza kulipa.

“Fedha hizi zimeshikwa na Serikali, si fedha zao kisheria ni za wakulima, korosho inalimwa katika mikoa 17, hili ni tatizo kubwa,” alisema. 

Nape alisema, “Huruma ya kwako (Spika Ndugai) na Bunge hili, busara ya kwako na Bunge hili, tujadili tuokoe suala hili na zao hili. Kuendelea Serikali kukamata fedha hizi ni kuhujumu. Naomba huruma yako na Bunge hili, niliahidi kuirudisha hapa kama hatutaelewana na nimeirudisha,” alisema Nape.

Baada ya Nape kuwasilisha hoja hiyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai alitoa fursa kwa mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti, Hawa Ghasia na mbunge wa Kigoma Mjini (ACT- Wazalendo), Zitto Kabwe kutoa ufafanuzi. 

Zitto alisema, “Suala la export levy la korosho si pekee ambalo Serikali inaagizwa na sheria, TRA (Mamlaka ya Mapato Tanzania) wakusanye wapeleke mfuko mkuu na kiasi fulani kipelekwe lakini haifanyiki.”

Alisema katika kamati ya bajeti kulikuwa na mjadala kuhusu makusanyo ya reli kwamba, TRA inakusanya na kupeleka mfuko mkuu na kutopelekwa makato mengine kunakohusika.

“Kuna tatizo la uvunjifu wa sheria, imekuwa kawaida kwa Serikali kuvunja sheria, ninaomba kama alivyosema Nape tulitizame hili ili Bunge liielekeze Serikali kutekeleza sheria,” alisema Zitto.

Ghasia alipotakiwa kutoa maelezo alisema, “Ni kweli suala hili lililetwa na tulipata fursa ya kukutana na mtoa hoja (Nape), wabunge ambao walikuwa na masilahi na hoja hii na tulipata fursa ya kukutana na waziri wa kilimo.

“Baada ya kuipitia hoja na kanuni inayotaka hoja itoke na kwenda kwa kamati, tulikuta inakosa sifa. Kifungu na fedha tunazozizungumzia, hata katika bajeti ya wizara ya kilimo mwaka jana hakuna.”

Ghasia alisema, “Asilimia 65 inakwenda katika mfuko wa korosho, asilimia 35 inakwenda mfuko mkuu. 

“Sheria ile ni ya Bunge na haijabadilishwa, kamati imeshindwa kuendelea na tumeirudisha katika ofisi yako ili uweze kutoa uamuzi,” alisema Ghasia.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Bunge), Jenista Mhagama alisema:

“Wakati tunaendelea kuhangaika na jambo hili kwa siku chache, pamoja na sheria ya mgawanyo na bodi ya korosho, Serikali ilikuwa imeagiza kutoa Sh10 bilioni kwa ajili ya kazi hiyo,” alisema.

Alisema kwa maelezo aliyopewa na waziri wa fedha, kiasi hicho kimeshatolewa.

Akizungumzia hilo, Spika Ndugai alisema, “Nawashukuruni wote kwa miongozo mliyoiomba. Ningeomba mheshimiwa Nape na wabunge, hili mtuachie meza, ili Waziri Mkuu akija, tuone tunafanyaje, kama hatutaona njia, basi tutalirudisha kwenu.

“Haya ni mambo yanasikitisha sana sana, Wizara ya Fedha. Waziri wetu wa Kilimo, mara ya mwisho alipokwenda kwenye kamati ya bajeti, imebidi atoe machozi. Amelia kama mtoto mdogo, watu wanalaumiwa, mtu analaumiwa, wala sio mkosaji. Wizara ya fedha kuna mambo yanaendelea huko. Sasa sisi tunakuwa hatujui, kwa hiyo tunawaona kama nyinyi wabaya...
 
“Hivi kwa nini ukae na hela ya mtu, awe anakuomba, anakupigia magoti, anakulamba lamba na hela ni yake. Hapa tulipofika mbali sana, sasa waheshimiwa mawaziri wawe wanalia kweli, kwenye kamati za Bunge! Kweli hapana hapana, Wizara ya Fedha, hebu mjitathmini.
 
“Mnawafanya wanakuwa ‘very miserable’ hawawezi kusema kwa sababu ya uwajibikaji wa pamoja. Kwa hiyo anagumia tu hapa, anapigwa na wabunge, anagumia tu, anapigwa. Sasa sisi wote hapa tunadhani waziri mbaya.

“Hapa katikati tulikuwa tunapambana na waziri hela ya Rea, kumbe ni hawahawa walikuwa wanashika hela ya Rea ndiyo maana miradi ilikuwa imesimama eeh. Kwa hiyo huenda kuna shida Wizara ya Fedha, kwa sababu sisi hatujui, tunawaoneni wabaya, kwa sababu ni hela za wenyewe, wala si hela za bajeti ambayo tunaiongelea sisi.
 
“Haya ni makato ya wakulima wa korosho. Ni hela zao, kwa hiyo tuachieni mheshimiwa waziri mkuu akirudi tu ‘rub shoulders’, halafu tutarudi kwenu.
 
“Kwa kweli ni jambo ambalo linasikitisha na ninaomba muanze kulifanyia kazi haraka. Kwa sababu mambo ya kilimo yanaenda na msimu. Kama msimu wa kupuliza salfa umepita, ina maana mwaka huo zao zima lime ‘crush’. Kwa hiyo lazima na utoaji fedha uende kwa msimu.
 
“Huwezi kushika dokezo, dokezo sijui limefanyaje, sijui likoje likoje, halafu inachukua mwezi, haiwezekani, haiwezekani.”

No comments: