Advertisements

Friday, May 11, 2018

Ndugai amuunga mkono Zitto kuhusu mawaziri wawili kusafiri nje ya nchi


By Ibrahim Yamola, Mwananchi iyamola@mwananchi.co.tz

Dodoma. Spika wa Bunge, Job Ndugai amesema waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage na yule wa Maliasili na Utalii, Dk Hamis Kigwangalla wanapaswa kusafiri nje ya nchi ili kutafuta fursa za biashara na uwekezaji.

Alipoingia madarakani, Rais John Magufuli alisitisha safari za nje na zisizo na tija kwa watendaji wa Serikali na kueleza kuwa yeye, makamu wake na katibu mkuu kiongozi ndio watakaotoa vibali vya safari za kwenda nje ya nchi.

Hata hivyo, jana Spika Ndugai aliwapa ushauri wa kusafiri nje ya nchi mawaziri hao wawili baada ya mbunge wa Kigoma Mjini (ACT-Wazalendo), Zitto Kabwe kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ya mwaka 2018/19.

Mchango wa Zitto

Akichangia bungeni, Zitto alisema waziri wa wizara hiyo, Mwijage anaiendesha kama ilivyo Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) badala ya kuiongoza kidiplomasia.

“Wizara ya Viwanda na Biashara tumepoteza Dola za Marekani bilioni moja (zaidi ya Sh2.4 trilioni) katika kipindi cha miezi 24, ni sawasawa na kupoteza kila siku Sh3 bilioni kwa mwaka uliopita, bado upo hapa kwa nini usijiuzulu? Umeshindwa kazi, huwezi kuendesha Wizara ya Viwanda na Biashara kama Tamisemi, ni diplomasia kwenda nje kutafuta masoko,” alisema Zitto.

“Malaysia, nenda huko ni rafiki wa Mwalimu (Julius) Nyerere, huwezi kujidanganya na viwanda vya cherehani, biashara ina nguvu na Wahindi waliopo hapa ni kutoka Bujarati zungumza nao waliopo hapa. Bidhaa zote zimeshuka bei unafanya nini?”

Msisitizo wa Ndugai

Baada ya Zitto kumaliza kuchangia, Spika Ndugai alisema, “Ni kweli alichokisema Zitto, mawaziri lazima msafiri kweli, eeee, waziri wa biashara hawezi kukaa hapa na sisi, lazima asafiri, eeee, tumwombee popote pale kwenye mamlaka.”

Huku akishangiliwa na wabunge, Spika alisema, “Lazima asafiri sasa bidhaa zetu tutauza wapi? Kongwa, Kongwa kuna soko, waziri wa Maliasili na Utalii aondoke wapige mawingu huko, ndio ukweli wenyewe. Sisi wabunge lazima tuwasemee.”

Kamati yalizwa na urasimu

Awali, akiwasilisha maoni ya kamati, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Viwanda, Biashara na Mazingira, Suleiman Sadiq alisema kuna urasimu katika uwekezaji ikiwamo upatikanaji wa vibali vya uhamiaji.

Alisema pamoja na hatua nzuri zinazochukuliwa na Serikali, yapo malalamiko kutoka kwa wawekezaji kuhusu mazingira ya uwekezaji nchini.

“Baadhi ya wawekezaji wanalalamikia uwepo wa changamoto kama mamlaka nyingi za udhibiti, urasimu katika upatikanaji wa vibali vya uhamiaji na mlolongo wa kupata vibali vya uwekezaji,” alisema na kuongeza:

“Kamati inaishauri Serikali iendelee kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini ili kuvutia wawekezaji wengi.”Kadhalika, alisema kumekuwa na uwekezaji katika sekta ya viwanda usiozingatia upatikanaji wa malighafi na faida za kijiografia za eneo husika.

“Kamati inaishauri Serikali kabla ya kuanzisha viwanda ufanyike utafiti wa kutosha ili kutambua aina ya kiwanda cha kuanzisha kutokana na faida za kijiografia za eneo husika,” alisema.

Sadiq ambaye pia ni mbunge wa Mvomero (CCM), aligusia utekelezaji wa bajeti ya mwaka 2017/18 ya wizara hiyo akisema Serikali imeshindwa kuipelekea fedha za maendeleo kama zilivyopitishwa na Bunge.

Alisema hadi kufikia Machi 2018 kati ya Sh80.11 bilioni zilizopitishwa kwa ajili ya miradi ya maendeleo, Sh8 bilioni ndizo zilizopokewa wizarani.

Akichangia bajeti hiyo, mbunge wa viti maalumu (CCM), Kiteto Koshuma alishangazwa na kitabu cha hotuba ya bajeti ya wizara hiyo kutokuwa na sehemu inayozungumzia viwanda vya nguo akisisitiza kwamba umaskini uliopo nchini unasababishwa na kubinafsishwa kwa viwanda 146 vya nguo vilivyokuwepo miaka ya nyuma.

No comments: