Advertisements

Monday, June 18, 2018

UPINZANI WASEMA SERIKALI INAWABANA

Naibu Msemaji wa kambi hiyo wa Wizara ya Fedha
By Mwandishi Wetu, Mwananchi mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dodoma. Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imesema Serikali imefanikiwa kuwabana wapinzani na kuzuia kusomwa kwa bajeti yake mbadala ya upinzani kwa mwaka 2018/19.

Hayo yamesemwa leo Juni 18, 2018 na Kaimu Mnadhimu wa kambi hiyo, Joseph Selasini na Naibu Msemaji wa kambi hiyo wa Wizara ya Fedha na Mipango, David Silinde katika mkutano wao na waandishi wa habari uliofanyika viwanja vya Bunge jijini Dodoma.

Soma Zaidi: Silinde atoa malalamiko Bajeti ya Upinzani kukataliwa, wasusia bunge

Silinde ambaye ni Mbunge wa Momba (Chadema) amesema wameiwasilisha hotuba yao mapema na kwa mujibu wa dokezo la Spika Job Ndugai la Aprili 19, 2018 inatakiwa kuwasilishwa bungeni siku moja kabla.

“Mimi ni mjumbe wa Kamati ya Bajeti, taarifa ya kamati iliyosomwa leo tuliiandaa hadi saa 4 usiku jana, lakini hotuba hii yetu tumeiwasilisha saa 8 mchana imekataliwa, tumefuata taratibu zote lakini wamekataa,” amesema Silinde na kuongeza:

“Yaani taarifa iliyochelewa imepata nafasi ila taarifa iliyowahi imezuiliwa, Serikali haitaki kukosolewa, kama ilivyozuia mikutano ya hadhara, imefanikiwa kuzuia na Bunge, nchi imebadilika, sasa wanazuia maoni mbadala.”

Selasini ambaye pia ni Mbunge wa Rombo (Chadema) amesema, Serikali inaogopa maoni mbadala, kukosolewa, na wanajua bajeti yao ni hewa ndiyo maana wanawazuia wapinzani.

“Wanafikiri tutachukia na kuondoka, hatuondoki, tunarudi bungeni kuichambua kwani wanajua tukifanya hivi wataondoka, hatuondoki tunarudi,” amesema

Awali, wapinzani waliondoka bungeni hapo baada ya Silinde kuhoji kuhusu kukataliwa kwa bajeti hiyo. Wamerudi bungeni na kuendelea na kikao.

No comments: