
Dodoma. Wabunge jana walipitisha bajeti ya Serikali ya mwaka 2018/19 ya Sh32.45 trilioni kwa kura 266 kati ya 348 zilizopigwa sawa na asilimia 76.
Awali, akitoa utaratibu wa shughuli za Bunge asubuhi, Spika Job Ndugai alisema kama wabunge wangeipigia bajeti hiyo kura ya hapana, Rais angeuvunja mhimili huo wa dola.
Akitangaza matokeo ya kura jana jioni, katibu wa Bunge, Stephen Kagaigai alisema wabunge waliokuwa ukumbini wakati wa kupiga kura walikuwa 348.
“Idadi ya wabunge waliopiga kura ni 348, wabunge 43 hawakuwapo. Kura za hapana ni 82, hakuna kura ambao haikuamua na kura za ndiyo ni 266,” alisema Kagaigai na baada ya kauli yake, shangwe kutoka kwa wabunge wa CCM zisikika.
Kauli ya Ndugai
Spika Ndugai aliwashukuru Rais John Magufuli; makamu wake, Samia Suluhu Hassan na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Alisema watakapoondoka Ijumaa baada ya mkutano wa 11 wa Bunge kuahirishwa, mawaziri watakuwa wamesheheni maoni ya wabunge na ushauri wa wananchi.
“Mawaziri tuwakumbushe, si upewe bajeti na hawa ukatumikia hawa,” alisema huku akicheka.
Alisema, “Huwezi kukataa bajeti halafu unakuja kuuliza una mpango gani na daraja langu, sasa bajeti si uliikataa.”
Asubuhi Ndugai akitoa maelezo ya kile kilichofanyika jana saa kumi na moja jioni katika kupitisha bajeti alisema iwapo wabunge wasingeipitisha Rais angelivunja Bunge.
“Endapo mlio wengi mtaikataa bajeti ya Serikali, Bunge hili Rais atalivunja haraka,” alisema kauli iliyoibua minong’ono kutoka pande zote za wabunge.
Spika Ndugai alisema, “Na baadhi yenu, mkirudishwa majimboni hamrudi kwa hiyo akili za kuambiwa changanya na zako.”
Alisema mbunge hapigi kura kwa jambo moja, bali ni kwa mfuko wote wa bajeti na hivyo ni vizuri wananchi wakaelewa.
Upigaji kura
Wabunge wanane wa CUF walipiga kura ya ndiyo kwa bajeti ya Serikali.
Kati ya wabunge hao, wawili ni wa majimbo ambao ni Maftaha Nachuma (Mtwara Mjini) na Magdalena Sakaya (Kaliua).
Wengine sita ni wa viti maalumu ambao ni Zainab Mndolwa; Alfredina Kahigi; Rukia Kassim; Nuru Bafadhili; Kiza Mayeye na Rehema Migilla.
Wabunge hao ni ambao wanamuunga mkono mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na ofisi ya msajili wa vyama vya siasa.
Chama hicho kimegawanyika pande mbili; moja inayomuunga mkono Profesa Lipumba na nyingine inamuunga mkono katibu mkuu, Seif Sharif Hamad.
CUF imekuwa katika mgogoro wa kiuongozi tangu Septemba, 2016 baada ya Profesa Lipumba kubadilisha uamuzi wa kujiuzulu uenyekiti aliouchukua Agosti 2015.
Kura zao za ndiyo za wabunge wa CUF zilishangiliwa na wale wa CCM baadhi wakipiga vigelegele na wengine wakigonga meza, huku wakisimama.
Sakaya akipiga kura alisema, “Ndiyo kwa maendeleo ya wana Kaliua.”
Mbunge wa viti maalumu (CCM), Jacqueline Ngonyani maarufu Msongozi alipoitwa jina ili kupiga kura alianza kupiga vigelegele kisha akasema “ndiyooo” na kuendelea kupiga vigelegele.
Hali hiyo iliibua shangwe ndani ya ukumbi, hasa kutoka kwa wabunge wa CCM.
Baada ya kupiga kura kwa kutamka ndiyo wabunge wa CCM, Hussein Bashe (Nzega Mjini); Nape Nnauye (Mtama) na Abdallah Bulembo (Kuteuliwa) walishangiliwa kwa nguvu na wenzao.
Jina la mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu lilipoitwa kuliibuka ukimya kidogo kabla ya kuitwa mbunge mwingine.
Lissu hayupo bungeni kwa zaidi ya mwaka mmoja baada ya kushambuliwa kwa risasi mjini Dodoma Septemba 7 na sasa anaendelea na matibabu nchini Ubelgiji.
Wakati wa upigaji kura, waziri wa Mambo ya Nje, Dk Augustine Mahiga na wa Sheria na Katiba, Profesa Palamagamba Kabudi hawakuwapo.
Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe pia hakuwapo.
No comments:
Post a Comment