ANGALIA LIVE NEWS

Monday, June 11, 2018

Waziri Kalemani aitaka Tanesco kukamilisha ukarabati wa miundombinu kabla ya Juni 30

 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (katikati) akikata utepe kuashiria uwashaji umeme katika kijiji cha Kyerwa kilichopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera. Kulia ni Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa, Kanali Mstaafu Shabani Lissu.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akibonyeza kitufe kuashiria uwashaji umeme katika kijiji cha Kyerwa kilichopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
 Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani akifafanua jambo kwenye mkutano wa hadhara uliofanyika kijiji cha Kyerwa kilichopo wilayani Kyerwa mkoani Kagera.
 Watendaji kutoka Wizara ya Nishati, Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na mkandarasi kutoka kampuni ya Nakuroi Investment Company Limited wakifuatilia maelekezo yaliyokuwa yanatolewa na Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani)
Sehemu ya wakazi wa kijiji cha Katanda kilichopo wilayani Karagwe wakimsikiliza Waziri wa Nishati, Dkt. Medard Kalemani (hayupo pichani) kwenye mkutano wa hadhara.


Na Greyson Mwase, Kagera
Waziri wa Nishati Dkt. Medard Kalemani amelitaka Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO), kuhakikisha linakamilisha kazi  ya ukarabati wa miundombinu yote ya umeme nchi nzima kabla ya Juni 30 mwaka huu.
Dkt. Kalemani ameyasema  hayo leo tarehe 10 Juni, 2018 alipokuwa akizungumza katika ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera kwenye ziara yake ya kukagua mradi wa ujenzi wa miundombinu ya usambazaji umeme inayosimamiwa na Wakala wa Nishati Vijijini Awamu ya Tatu (REA III) na ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme kwa kutumia maji cha Rusumo  kitakachokuwa na uwezo wa kuzalisha Megawati 80 baada ya kukamilika Februari, 2020.
Alisema kuwa, kwa sasa nchi ina nishati ya  umeme wa uhakika mbali na  kuwepo kwa changamoto ya kukatika kwa umeme inayotokana na uchakavu wa miundombinu ya kusafirisha umeme.
“ Tulikubaliana na uongozi wa TANESCO kuhakikisha kazi ya ukarabati wa miundombinu ya umeme nchi nzima, inakamilika ndani ya miezi mitatu yaani hadi mwishoni mwa mwezi Juni mwaka huu ili wananchi waanze kupata nishati ya umeme wa uhakika,” alisema Waziri Kalemani.
Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani alimtaka mkandarasi anayefanya kazi ya ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mkoa wa Kagera kupitia Mradi wa REA Awamu ya Tatu, kampuni ya Nakuroi Investment Company Limited kuongeza kasi ya usambazaji katika mkoa wa Kagera ili mradi uweze kukamilika kwa wakati na wananchi kupata umeme wa uhakika.
Aidha, alizitaka taasisi za umma kama vile mashule, vituo vya afya na halmashauri kutenga fedha kwa ajili utandazaji wa nyaya za mifumo ya  umeme (wiring) katika majengo yao ili waweze kuunganishiwa umeme mapema wakati wa utekelezaji wa mradi.
Wakati huohuo, Dkt. Kalemani aliitaka Serikali ya Mkoa  na Wilaya kutenga maeneo kwa ajili ya viwanda ili iwe rahisi kuwekewa miundombinu ya umeme wakati wa utekelezaji wa miradi.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa mradi wa REA Awamu ya Tatu katika mkoa wa Kagera, Mhandisi Miradi ya TANESCO katika mkoa wa Kagera, Jackson Kamuli alisema kuwa mradi  huo ulizinduliwa mwezi Julai mwaka jana katika kijiji cha Rwabigaga wilyani Kyerwa.
Alifafanua kuwa, mradi huo unatekelezwa kwenye wilaya saba ambazo ni pamoja na Bukoba Vijijini, Biharamulo, Karagwe, Kyerwa, Misenyi, Muleba na Ngara kupitia mkandarasi ambaye ni Nakuroi Investment Company Limited ya hapa nchini.
Alisema mradi unatarajiwa kujenga laini za msongo  wa kati  wa kilovolti 33 zenye  urefu wa kilomita 299.01; laini za msongo mdogo wa kilovolti 0.4 zenye urefu wa kilomita 574 na kufunga jumla ya transfoma 287.
Mhandisi Kamuli aliongeza kuwa mradi utakapokamilika utanufaisha vijiji 141 ambapo jumla ya wateja 9,141 wanatarajiwa kuunganishwa na huduma ya umeme.
Akielezea gharama za mradi, Mhandisi Kamuli alisema mradi utagharimu  kiasi cha shilingi bilioni 38.5.
Wakati huohuo akizungumza na wananchi wa vijiji vilivyopo katika wilaya za Kyerwa, Karagwe na Misenyi mkoani Kagera, Waziri Kalemani  alimtaka mkandarasi anayetekeleza kazi ya usambazaji wa miundombinu ya umeme  katika mkoa huo kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ambaye ni Nakuroi Investment  Company Limited kuhakikisha vijiji vyote pamoja na vitongoji vyake vinapata umeme wa uhakika na kukamilisha kazi kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Dkt. Kalemani alilitaka  Shirika la TANESCO kufungua kituo cha huduma kwa wateja katika vijiji vyote ili kuondoa kero ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma ya  umeme.
Aidha, Waziri Kalemani aliwataka wananchi kujiandaa na huduma ya umeme kwa kutandaza mifumo ya nyaya (wiring) kwenye nyumba zao au kuweka kifaa kijulikanacho kama Umeme Tayari (UMETA) ili watakapofikiwa na mradi waweze kuunganishwa mara moja.
Aliwataka wananchi kutumia fursa zitokanazo na upatikanaji wa huduma ya umeme wa uhakika kama kufungua viwanda kwa ajili ya mazao na mashine za kuchomelea ili waweze kujiongezea kipato
Dkt. Kalemani alisema umeme wa uhakika utachochea kasi ya ukuaji wa uchumi wa nchi hasa katika maeneo ya vijijini  kutokana na shughuli za viwanda vidogo vidogo na kilimo.

No comments: