Advertisements

Tuesday, June 19, 2018

ZFDA YAKAMATA BIDHA MBALIMBALI ZISIZOFAA KWA MATUMIZI YA BINADAMU

MKURUGENZI Mtendaji Bodi ya Chakula na Dawa Zanzibar, Dkt. Burhan Othman Simai (kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusiana na zoezi la Kukamata bidhaa zisizofaa kwa matumizi ya Binaadamu miezi miwili iliyopita. 
 Mkuu wa Ukaguzi wa Chakula Mohammed Shadhil (kushoto) na Muangalizi wa Ofisi Mussa Bakar Othman wakionesha  vipodozi vyenye chemicali za sumu zilizoingizwa kwa ajili ya siku kuu.
Aina za Bidhaa za Mchele, Unga wa Ngano,Mafuta ya Kula na vipodozi zilizokamatwa na ZFDA ambazo  hazifai kwa  matumizi ya Binaadamu.
Picha na Abdalla omar Maelezo – Zanzibar.

Ramadhani Ali – Maelezo Zanzibar
Wakala wa Chakula na Dawa  Zanzibar (ZFDA) imezuia kusambazwa bidhaa za chakula na vipodozi zilizoingizwa nchini kwa ajili ya mwezi mtukufu wa Ramadhani na siku kuu ya Idd el Fitri kinyume na taratibu na zilizokuwa hazifai kwa matumizi ya binadamu.

Mkurugenzi Mtendaji wa ZFDA Dkt. Burhan Othman Simai alisema bidhaa hizo zilikamatwa kufuatia operesheni maalumu waliyoifanya katika kipindi cha miezi miwili kwenye maghala ya wafanyabiashara na baadhi ziligundulika zimetupwa katika jaa la Kibele na eneo la Migombani.

Akizungumza na waandishi wa habari Ofisini kwake Mombasa Dkt. Burhani alizitaja bidhaa zilizokamatwa na zilizotupwa kuwa ni mchele tani 40, unga wa sembe tani 75,  sukari tani 25 na lita 15,000 za mafuta ya kula.

Alisema dawa na vipodozi vilivyokamatwa ni vichupa 4000 vya chanjo aina ya ATS kutoka China zilizoingizwa nchini kinyume na miongozo ya uingizaji na utoaji wa dawa nchini, na tani tisa za vipodozi vyenye viambata vya sumu kali inayosababisha saratani ya ngozi.

Dkt. Burhan alieleza masikitiko yako kwa baadhi ya wafanyabiashara kutoa sadaka bidhaa hizo bila kuangalia athari inayoweza kuwapata wananchi wenzao baada ya kuzitumia.

Alizitaka Taasisi za Seriakli na Asasi za kiraia zinazotaka kutoa sadaka inayohusiana na chakula kwenda ofisini kwao ili kupata ithibati juu ya ubora na usalama wa Chakula husika kwani bidhaa nyingi za chakula huwekwa katika ghala kwa kipindi kirefu na kupoteza ubora wake wakati wa kuzihifadhi.

Aliwashukuru wananchi walioshirikiana na Bodi ya Chakula na Dawa Zanzibar kwa kutoa taarifa katika juhudi za kuibua na kudhibiti aina hizo mpya za uhalifu nchini.

Alisema wahusika wote wa matukio hayo wamepelekwa katika vyombo vya sheria na alieleza matarajio yake kuwa vyombo hivyo vitatekeleza  wajibu wake ili kuzuia vitendo hivyo visiendelee  na kuwanusu wananchi kuathirika na bidhaa mbovu.


Mkurugenzi Mtendaji ZFDA alisema wataendelea kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa bidhaa bandarini na kwenye maghala na maduka na watandaa operesheni maalumu karibu na mwezi wa Ramadhani kwani baadhi ya wafanyabiashara hutumia kipindi hicho kuingiza bidhaa kinyume na taratibu na zisizofaa kutokana na mahitaji ya wananci kuongezeka katika kipindi hicho.

No comments: