ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 23, 2018

BALOZI SEIF ATEMBELEA ZBC RADIO RAHALEO MJINI UNGUJA

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi akilakiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Habari, Utalii na Mambo ya Kale anayesimamia Habari Dr. Yussuf  Mnemo alipofanya ziara fupi  katika Kituo cha Matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – REDIO). Kulia ya Dr. Mnemo ni Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Bibi Iman Duwe na Naibu Wake Bibi Nasra Mohamed.
Msaidizi Mhariri Mkuu wa Chumba cha Habari ZBC –Redio Amour Nassor akimuelezea Balozi Seif  aliyepo (katikati) Majukumu ya Wana Habari katika uwajibikaji wao wa kila siku. Wa kwanza kushoto ni Mkurugenzi Mkuu wa ZBC Bibi Iman Duwe  nas kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Mh. Mihayo Juma N’hunga.
Fundi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar Ali Boud Talib aliyevaa kofia ya Kiua akimpatia maelezo balozi Seif   ndani ya moja ya Studio ya Watangazaji wakati wa ziara yake katika Kituo cha Matangazo ya Redio Rahaleo. Wa kwanza kutoka Kushoto ni Mtangazaji mahiri wa Redio na Televisheni Khamis Mohamed na Mkuu wa Kitengo cha Watangazaji Bibi Suzan Peter Kunambi.
Mtangazaji wa Spice FM ambae pia mpiga picha wa ZBC – TV Said Golo na watangazaji wenzake wakifurahia ujio wa Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi ndani ya Studio yao iliyopo Rahaleo.
Balozi Seif akisisitiza umuhimu wa Uongozi wa ZBC kutumia Bajeti zao za Mwaka katika kutanzua baadhi ya changamoto zinazowakabili ikiwemo Vikalio. Picha na – OPMR – ZNZ.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi  amewashauri Wana Habari wa Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC) kuendelea kuwa wabunifu zaidi wa vipindi  vitakavyoleta mvuto na hatimae kuwa na  wasikilizaji wengi zaidi wa Shirika hilo Nchini.

Alisema licha ya kuwepo kwa vipindi vingi vilivyokuwa maarufu  na kukubalika kwa wasikiizaji wengi akitolea mfano Kipindi cha Mawio na Maelezo baada ya Habari lakini bado juhudi za ubunifu zinahitajika katika kuona Mfumo wa Matangazo unawafikia Wananchi wengi zaidi Mjini na Vijijini.

Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo wakati alipofanya ziara fupi katika Kituo cha Matangazo cha Shirika la Utangazaji Zanzibar (ZBC – REDIO) kiliopo Rahaleo Mjini Zanzibar kuangalia shughuli za utendaji kazi wa Taasisi hiyo ya Habari na kuridhika na jitihada zinazochukuliwa na Watendaji wawake.

Alisema upo umuhimu wa vipindi na matangazo ya ZBC Redio kuangaza zaidi kwa upande wa Majimboni na Vijijini ili Wananchi wa maeneo hayo wawe na fursa ya kuwasilisha changamoto zinazowakabili hasa katika harakazi zao za kujiletea maendeleo.

Balozi Seif alieleza kwamba wakati Serikali Kuu inafikiria jitihada za kusaidia changamoto zinazowakabili watendaji wa Kituo hicho cha Matangazo ya Radio ambapo pia kupitia nafasi yake ya Uwakilishi atajaribu kuwashawishi Wawakilishi wenzake majimboni kutoa ushirikiano utakaowezesha kuendelezwa kwa Vipindi vya kutoka Majimboni.

Alisema vipo vipindi vinavyoweza kusaidia Wananchi kuelimika zaidi ambavyo vinapaswa kupewa umuhimu wa pekee ili kupunguza kero zinazowakabili sambamba na kumrahisishia Mwakilishi kutekeleza majukumu yake badala ya kusubiri Vikao vya Baraza la Wawakilishi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliutaka Uongozi wa Shirika la Habari Zanzibar kupitia Wizara yake ya Habari, Utalii na Mambo ya kale kutoa kipaumbele masuala ya vitendea kazi vinavyohitajiwa na watendaji  na kuainishwa ndani ya Bajeti ya Shirika badala ya kusubiri Serikali Kuu.

Hata hivyo Balozi Seif  alisema mpangilio wa maombi hayo  ni vyema ukafanyika kwa kila Awamu kwa vile hakutakuwa na Bajeti itakayokuwa na uwezo wa kutosheleza mahitaji ya kila Taasisi.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza utaratibu wa kuendeleza Vikao vya utendaji kati ya Uongozi wa Shirika na Wataendaji wake ili kutafuta njia ya kutanzua kasoro zinazojichomoza ndani ya uwajibikaji wa Wafanyakazi na Viongozi wa Taasisi hiyo.

Alisema licha ya vikao hivyo kuibua mapungufu ya utendaji ndani ya kazi lakini pia vitasaidia kupunguza au kuondoa minong’ono ya umbali unaoweza kujitokeza kati ya pande hizo mbili.

Balozi Seif alifahamisha kwamba  mapenzi kati ya Viongozi na Wafanyakazi  hao ni jambo la msingi  na la muhimu hasa kutokana na muingiliano wa kazi zao kwa vile zinategemeana.

Mapema Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alitembelea vitengo mbali mbali vya Kituo hicho cha Matangazo ya Redio cha Shirika la Utangazaji  Zanzibar na kujionea uwajibikaji wa Kizalendo waliokuwa nao watendaji wake ambao umempa faraja kubwa.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC} Bibi Iman Duwe  alimueleza Balozi Seif  kwamba Jengo la Kituo hicho linatarajiwa kufanyiwa matengenezo makubwa chini ya Usimamizi wa Serikali ya Jamuhuri ya Watu wa China.

Bibi Iman alisema Matengenezo hayo yanayotarajiwa kuanza mara baada ya kukamilika Mradi ya Matengenezo uliopo Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja utahusisha marekebisho ya Jengo sambamba na ufungaji wa vifaa vyengine vipya vinavyokwenda na mfumo wa Teknolojia ya Kisasa ya Mawasiliano Ulimwenguni.

“ Tunatarajia kupata Mitambo mengine Mipya  ya Digital itakayoenda sambamba na Mafunzo ya Miezi sita kwa Watendaji wake”. Alisema Mkurugenzi Mkuu huyo wa Shirika la Utangazaji Zanzibar {ZBC}.

Balozi Seif  aliangalia utendaji kazi ndani ya Chumba cha Habari, baadhi ya Studio za Vipindi na Kutangazia, Maktaba ya Vipindi vya Redio, pamoja na chumba maarufu cha kipindi cha Mawio.

No comments: