ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, July 19, 2018

Gari La Wagonjwa Lapata Ajali Likitoroshwa Usiku, Ni Siku Chache tu Baada ya Gari Jingine Kunaswa na Mirungi

Gari la kubeba wagonjwa la Wilaya ya Itilima mkoani hapa limepata ajali, huku ndani likiwa na matairi chakavu tisa, siku chache baada ya serikali kupiga marufuku magari hayo kupakia kitu chochote zaidi ya wagonjwa.

Gari hilo lenye namba za usajili STK 6646, lilipata ajali hiyo majira ya saa 10 usiku kuamkia jana, katika eneo la Daraja la Mto Bariadi, katikati ya Mji wa Bariadi na chanzo cha ajali hiyo hakijafahamika.

Serikali kupitia Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, hivi karibuni ilipiga marufuku magari ya wagonjwa kubeba kitu chochote zaidi ya wagonjwa.

Hatua ya kupiga marufuku hiyo inafuatia gari moja la wagonjwa kukutwa likiwa limepakia magunia ya dawa za kulevya aina ya mirungi, huku likiacha wagonjwa wakihangaika usafiri wa kuwawahisha hospitali kupata huduma.

Gari lililokutwa na matairi hayo chakavu ni lenye namba za usajili STK 6646.

Dereva wa gari hilo Ndekeja Makwenu, amelazwa katika hospitali teule ya Mkoa wa Simiyu baada ya kupata marejaha mbalimbali.

Akizungumza na waandishi wa habari, Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Paul Nyalaja, alisema gari hilo ni moja ya magari manne yaliyopelekwa mkoani Mwanza kwa ajili ya matengenezo ya kuondolewa matairi yaliyochakaa, Jumapili iliyopita.

Nyalaja alisema kuwa baada ya matengenezo hayo gari hilo lilibeba matairi yote ya magari manne, ambayo yalikuwa chakavu kwa ajili ya kuyarejesha ofisi za usafirishaji za halmashauri hiyo kama taratibu za manunuzi zinavyotaka.


“Gari lilifika Bariadi Jumatatu usiku na kuegeshwa katika kituo cha afya Muungano, kilichopo Mjini Bariadi, katika mazingira ya kutatanisha muda wa saa 10 usiku, gari liliondolewa kwenye kituo hicho kuelekea kusikojulikana,” alisema Nyalaja.

Alisema walishangaa kukuta gari hilo limepata ajali likiwa limebeba matairi hayo huku likionekana kuligonga tela la trekta lililokuwa limeegeshwa pembezoni mwa barabara baada ya kuharibika.

Kaimu Mkurugenzi huyo alieleza kuwa bado wanachunguza ili kubaini chanzo cha ajali, ikiwa pamoja na sababu za gari hilo kuondolewa kwenye maegesho ya magari ya serikali nyakati za usiku.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa wilaya hiyo, Benson Kilangi, alisema hakuna kifo kilichotokea, lakini amesikitishwa na ajali hiyo.

Alisema kutokana na mazigira ya ajali hiyo kuwa tata, ameagiza kukamatwa Ofisa Usafirishaji wa Halmashauri hiyo, Oswini Mlelwa na kuwekwa ndani kwa ajili ya mahojiano zaidi ikiwa pamoja na kufanyika kwa uchunguzi.

No comments: