Advertisements

Saturday, July 7, 2018

Mke akatwa kiganja, mume akiporwa fedha za vicoba mil 4/-

WAKAZI wa Kijiji cha Korotambe wilayani Tarime mkoani Mara, ambao ni mtu na mkewe wamejeruhiwa na watu wanaosadikiwa kuwa majambazi, ambao pia wamewapora Sh milioni nne, walizokuwa wanatunza kwa ajili ya kikundi chao. 

Joseph Makonyo (81) na mke wake, Robhi Makonyo (54), walikumbwa na mkasa huyo mjini hapa juzi baada ya kuvamiwa na majambazi hao majira ya saa moja usiku waliokuwa na silaha zikiwemo za jadi.

Kwa mujibu wa Mwenyekiti wa Kijiji hicho cha Korotambe, Anthony Mwita, katika tukio hilo, Rhobi alikatwa kiganja cha mkono na majambazi hao. Alisema majambazi hao walivamia nyumba ya Makonyo na kumkuta akiwa na mkewe wakiwa jikoni, ambapo ghafla walianza kushambuliwa huku wakilazimishwa watoe fedha zote walizonazo za kikundi.

Mume ndiye aliyekuwa na fedha hizo. Mwita alisema majambazi hao walichukua fedha hizo, lakini tayari walikuwa wameshawajeruhi vibaya wanandoa hao, kwa kuwakata mapanga katika miili yao na Rhobi alikatwa kiganja chake cha mkono. 

Alisema wawili hao walipiga kelele za kuomba msaada, ndipo wananchi walijitokeza, lakini tayari majambazi hao walishakimbia na fedha hizo.

Mwenyekiti huyo alieleza kuwa baada ya kuwasili eneo la tukio, Rhobi ambaye kiganja chake kilikuwa sakafuni, alikimbizwa katika Hospitali ya wilaya Tarime na mumewe na kupatiwa huduma za matibabu na baadaye walihamishiwa katika Hospitali ya Rufaa ya Bugando mkoani Mwanza baada ya hali zao kuwa mbaya.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Tarime Rorya, Henry Mwaibambe alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na kueleza kuwa polisi inaendelea na uchnguzi, ikiwa ni pamoja na kuwasaka watuhumiwa. 

Aliwaomba wananchi kutoa ushirikiano ili kuwakamata watuhumiwa hao waliohusika katika uhalifu huo wa unyang’anyi na kuwajeruhi vibaya wakazi hao.

No comments: