ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 23, 2018

Tanzania na Korea zakubaliana kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kibiashara

TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Tanzania imeiomba Jamhuri ya Korea iendelee kushirikiana na Serikali katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo ambayo Serikali ya awamu ya tano imeifanya kuwa ya kipaumbele katika kufikia azma ya uchumi wa viwanda.

Kauli hiyo ilitolewa leo Ikulu jijini Dar Es Salaam na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa (Mb) mbele ya waandishi wa habari akiwa na mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon.

Miradi ambayo Mhe. Waziri Mkuu aliitaja ni pamoja na ujenzi wa Daraja la Kigongo-Busisi mkoani Mwanza lenye urefu wa mita 3200, barabara ya Chaya mkoani Tabora yenye urefu wa kilomita 42 na ujenzi wa barabara ya juu ya bahari kutoka ufukwe wa Coco, Osterbay hadi Aga Khan, Upanga jijini Dar Es Salaam yenye urefu wa mita 1030. Miradi mingine ni ujenzi wa hospitali tano za rufaa katika kanda mbalimbali nchini na ujenzi wa reli ya kisasa ya kiwango cha kimataifa utakaotekelezwa kwa awamu tano ambapo awamu ya kwanza na ya pili kutoka Dar Es Salaam - Morogoro hadi Dodoma umeshaanza kwa kutumia Fedha za ndani.

Mhe. Majaliwa kabla ya kuzungumza na wana habari alikuwa na mazungumzo rasmi na mwenyeji wake na baadaye viongozi hao walishuhudia uwekaji saini wa Mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na utumishi baina ya Tanzania na Korea.

Mkataba huo kwa upande wa Tanzania ulisainiwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga na kwa upande wa Korea, Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje, Mhe. Lim Sung- Nam aliweka saini kwa niaba ya Serikali yake.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lee pamoja na mambo mengine alitembelea Kituo cha Kutunzia kumbukumbu cha Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa ambacho ujenzi wake ulitokana na mkopo wa masharti nafuu wa benki ya Exim ya Korea. Aidha, alitembelea hospitali ya Mnazi mmoja na kutoa msaada wa gari mbili za kubebea wagonjwa.

Wakati wa mazungumzo rasmi na mwenyeji wake, Mhe. Majaliwa alitumia fursa hiyo kuwakarabisha wafanyabiashara wa Korea kuja kuwekeza nchini katika sekta mbalimbali ikiwemo utalii.

Kuhusu utalii, Waziri Mkuu Majaliwa alieleza kuwa Korea imekubali kutangaza vivutio vya utalii vilivyopo nchini ili kuhamasisha watalii wengi kutoka nchi hiyo kuvitembelea na kubainisha kuwa michoro ya tingatinga ambayo asili yake ni Tanzania inapendwa sana nchini humo.

Katika ziara hiyo, Mhe. Lee amefuatana na wafanyabiashara wakubwa ambao watafanya mkutano na wafanyabiashara wa Tanzania siku ya Jumatatu tarehe 23 Julai 2018 unaolenga kuangalia namna watakavyoweza kushirikiana katika uwekezaji kwenye sekta mbalimbali hapa nchini.

Mhe. Majaliwa alieleza kuwa Serikali ya Tanzania inasifu na kuunga mkono jitihada zinazofanywa kati ya Korea Kusini na Korea Kaskazini za kumaliza tofauti zao kupitia mazungumzo ya amani.

Alihitimisha kwa kuwahakikishia wananchi kuwa Korea inaridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali ya awamu ya tano za kuinua uchumi wa Tanzania na kwamba nchi hiyo itaendelea kuunga mkono jitihada hizo. Aidha, Korea inasifu uwepo wa amani nchini na kuwasihi Watanzania waendelee kuitunza kwa kuwa ndio msingi wa maendeleo duniani.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam
22 Julai 2018
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa akisalimiana na Mgeni wake, Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Mhe. Lee Nak-yon walipokutana kwa ajili ya kufanya mazungumzo jijini Dar Es Salaam.
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Augustine Mahiga (kulia) na Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Korea, Mhe. Lim Sung- Nam wakiweka saini Mkataba wa kuondoa hitaji la viza kwa wenye hati za kusafiria za kidiplomasia na utumishi wanaposafiri baina ya nchi hizo mbili. 

No comments: