ANGALIA LIVE NEWS

Friday, July 20, 2018

TRA YAWATAKA WENYE VIWANDA KUTOA TAKWIMU SAHIHI ZA UZALISHAJI WAO


 Kamishna wa Kodi za Ndani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kulia) akiwa ameongozana na uongozi wa Kiwanda cha Manyara Sugar Company Limited kuelekea katika eneo la uzalishaji sukari wakati alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza changamoto za Wafanyabiashara.
 Kamishna wa Kodi za Ndani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Elijah Mwandumbya (katikati) akitoa maagizo kwa uongozi wa Kiwanda cha Manyara Sugar Company Limited kuhusu kutoa takwimu sahihi uzalishaji sukari wakati alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza changamoto za Wafanyabiashara.
 Kamishna wa Kodi za Ndani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Elijah Mwandumbya (kulia) akimsikiliza Mkurugenzi wa Kiwanda cha Manyara Sugar Company Limited, Bw. Pratap Sisudya wakati alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza changamoto za Wafanyabiashara.
Mkurugenzi wa Kiwanda cha Manyara Sugar Company Limited, Bw. Pratap Sisudya (katikati) akimweleza Kamishna wa Kodi za Ndani Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Bw. Elijah Mwandumbya (wa pili kulia) moja ya mtambo utumikao kuzalisha sukari wakati alipofanya ziara ya kikazi kusikiliza changamoto za Wafanyabiashara.
(PICHA ZOTE NA BENEDICT LIWENGA-TRA)

Na Rachel Mkundai, Manyara
Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imewataka wafanyabiashara wenye viwanda vya kutengeneza mali ghafi za kutengenezea pombe kali kutoa tawimu sahihi ya kiasi kinachozalishwa na mahali inapouzwa ili serikali iweze kukusanya kodi yake stahiki kupitia pombe kali.

Hayo yamesemwa na Kamishna waKodi za Ndani wa TRA Bw Elijah Mwandumbya mara baada ya kutembelea kiwanda cha kutengeneza sukari cha Manyara Sugar Company Limited kilichopo mkoani Manyara na kuongeza kuwa takwimu hizo zitawezesha TRA kufuatilia kwa karibu na kupata takwimu sahihi za kikodi na kuongeza makusanyo ya mapato.

“Tunafahamu kwamba “Molasis”  au mali ghafi inayotokana na zao la miwa baada ya kutengeneza sukari ni bidhaa inayotumika kutengenezea pombe kali na hivyo takwimu zitatuwezesha kufuatilia wafanyabiashara wanaonunua bidhaa hiyo na kutengenezea pombe kali ili nasi tukadai kodi yetu na kodi hiyo ilete tija kwa taifa”, amesema Bw. Mwandumbya 

Naye Mkuu wa mkoa wa Manyara Bw. Alexander Mnyeti amesema mkoa una mkakati wa kuongeza viwanda vingi vikubwa na vidogo ili viweze kuleta tija kwa mkoa kwa kuongeza ajira na pato la taifa kwa ujumla.

“Tunataka kuongeza viwanda vingi katika mkoa wetu ili serikali iweze kupata kodi zaidi na kuongeza mapato kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wetu”, amesema Bw. Mnyeti.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa kiwanda cha sukari cha Manyara Sugar Company Limited, Bw. Pratap Sisudya ameshukuru ujio wa Kamishna wa kodi za ndani na kuahidi kushirikiana na TRA kuhakikisha kuwa wanalipa kodi zote kwa wakati pamoja na kutoa takwimu sahihi za uzalishaji wa kiwanda.

 “Ni wajibu wetu kutoa taarifa zahihi kwa TRA pamoja na kulipakodi stahiki kwa wakati ambapo kwa mwaka 2017/2018 tumelipa kodi kwa serikali takribani Shilingi bilioni 1”, alisema Bw. Sisudya.
Kiwanda cha Manyara Sugar Company kinazalisha zaidi ya tani 4,000 za sukari kwa mwaka na kina mashamba ya miwa ekari 1,600 na kutoa ajira za muda kwa watu 350 hadi 400 kwa siku.

No comments: