Advertisements

Tuesday, August 7, 2018

DKT TIZEBA AAGIZA VIUATILIFU VYOTE VINAVYO ONYESHWA BILA KUFUATA UTARATIBU KUONDOLEWA KWENYE MAONESHO YA NANENANE

Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akizungumza jambo mara baada ya kutembelea Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Leo 6 Agosti 2018. (Picha Zote Na Mathias Canal, Wizara ya Kilimo)
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akikagua mashine ya mbalimbali za kilimo mara baada ya kutembelea banda la Halmashauri ya Wilaya ya Kilombero, Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Leo 6 Agosti 2018. 
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akijionea michoro mbalimbali ya ramani za nyumba mara baada ya kutembelea banda la VETA, Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Leo 6 Agosti 2018.
Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba akimsikiliza Mhandisi wa Kanda ya Umwagiliaji Morogoro Mhandisi Senzia Maeda mara baada ya kutembelea banda la Tume ya Umwagiliaji, Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro Leo 6 Agosti 2018.

Na Mathias Canal, WK-Morogoro

Waziri wa kilimo Mhe Dkt Charles Tizeba Leo 6 Agosti 2018 amewaagiza waratibu wa maonesho ya nanenane kuhakikisha Viuatilifu vinavyoonyeshwa kwenye maonesho ya sikukuu ya wakulima Nanenane pasina kufuata utaratibu wa kisheria vinaondolewa haraka.

Waziri Tizeba ameyasema hayo wakati akizungumza na wauzaji wa viuatilifu Kanda ya Mashariki Mkoani Morogoro mara baada ya kutembelea banda la Tan Vaterinary ambalo linauza viuatilifu vya aina mbalimbali zikiwemo dawa za virutubisho kwa ajili ya Nguruwe na kuku.

Alisema katika agizo hilo kuwa viuatilifu vyote vinavyouzwa pasina nembo ya Mamlaka ya viwango Tanzania (TBS), Mamlaka ya chakula na dawa (TFDA) na kampuni ya kutoa barcode za bidhaa zilizofungashwa (GS 1) hazipaswi kuwepo kwenye maonesho ya Nanenane kote nchini kwani kuruhusu viendelee kuuzwa ni hatari kwa wanyama sambamba na binadamu.

Alisema kuwa katika maeneo mengi nchini udhibiti wa viuatilifu ni mdogo hivyo wakaguzi wa viuatilifu wanapaswa kutilia mkazo ukaguzi ili kuzuia viuatilifu vinavyoingia nchini kinyume cha sheria na taratibu za nchi.

Kuhusu elimu kwa wananchi juu ya njia bora za kuhifadhi mahindi Waziri huyo anayeshughulikia sekta ya kilimo nchini aliagiza elimu kutolewa kwa kina kwa wananchi ili wawe na uelewa mkubwa pindi wanapomaliza kuvuna.

Alisema kuwa kumekuwa na biashara ya vihenge jambo ambalo ni zuri lakini changamoto kubwa wananchi bado hawajapatiwa elimu ya namna bora ya kuvitumia vihenge hivyo.

Aidha, amewataka washiriki mbalimbali kutuma wawakilishi kwenye weledi kuhusu bidhaa wanazoonyesha kwani kumekuwa na wawakilishi wengi ambao sio msaada kwa wakulima ambao wengi wao wanatembelea katika maonesho hayo kwa mtazamo wa kujifunza.

Katika hatua nyingine akiwa katika banda la maonesho ya Mifugo, Waziri Tizeba amewataka wataalamu hao wa Mifugo kubadili mtazamo wa kifikra kwa kuonyesha bidhaa bora, "Kila mwaka mnaleta Ng'ombe wa kisasa kwenye maonesho ya Nanenane wakati wanaokuja kujionea maonesho wengi ni wafugaji wa Ng'ombe wa kienyeji, hivyo badilikeni leteni Ng'ombe wa kienyeji" Alikaririwa Dkt Charles Tizeba


MWISHO.

No comments: