Advertisements

Tuesday, August 7, 2018

KAGAME: AFRIKA INAJITAKIA KUWA OMBAOMBA

Picha
RAIS wa Rwanda, Paul Kagame amesema Afrika itaacha kutegemea fedha za wahisani katika shughuli zake za maendeleo endapo itadhibiti usafirishaji fedha haramu, itaongeza ukusanyaji kodi na pia itaongeza thamani ya malighafi ilizonazo.

Ameyasema hayo wakati akifungua mkutano wa Jukwaa la Viongozi wa Afrika jijini Kigali.

Kagame, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), sasa akiwa anaongoza timu ya mabadiliko ya AU, alisema Afrika inapoteza fedha nyingi kwa njia haramu, wakati huohuo ikitegemea fedha za wahisani ambao kiasi chao cha fedha za misaada ni kidogo ikilinganishwa na fedha zinazoibwa kutoka Afrika.

“Thamani ya fedha haramu zinazosafirishwa, zinazotokana na ukwepaji wa kodi, na kadhalika zinazidi kabisa zile zinazoletwa kama misaada barani Afrika. Ili kuhakikisha tunapata fedha yote na kuachana na misaada, tunapaswa kuangalia mianya ya utoroshaji rasilimali na kuchukua hatua katika udhibiti,” alisema. Alisisitiza kuwa, Afrika kwa sasa inahitaji akili timamu kuliko misaada yenye hila.

“Afrika tuna kila kitu. Kama kuna tunachokikosa, tunaweza kukipata. Lakini inashangaza kuona tunabaki na akili kwamba hatuwezi kuendelea bila ya kupata misaada ya nje. Hii ni dhana potofu kabisa,” alisema.

Rais huyo mchapakazi alisema Afrika ikiamua inaweza kufanya mapinduzi makubwa, ikianza na uwajibikaji utakaorejesha heshima ya Afrika.

Alitolea mfano kuwa makusanyo ya kodi za ndani yanaweza kufanya mambo mengi ya maendeleo badala ya kutegemea wahisani.

Alisema `siasa’ za hovyo pia zinachangia kulegeza kasi ya maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Afrika.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa ambaye yuko nyuma ya Taasisi ya Uongozi iliyoandaa jukwaa hilo, alisema Afrika inapaswa kuziba mianya inayotafuna mapato ya nchi ambayo pia huwezesha uwekezaji wa ndani.

Amesema kama Afrika haitajisaidia kwa kuwekeza katika miradi yake, wawekezaji wa nje wataendelea kumiminika na kunufaika na jasho la Waafrika. Mkutano huo wa tano wa Jukwaa la Viongozi Afrika, ulibeba ujumbe wa 'Kufanyia Mapinduzi Maendeleo ya Afrika’ na ulishirikisha viongozi saba mashuhuri wa Afrika wakiwemo Mkapa, Joaquim Chissano wa Msumbiji, Olusegun Obasanjo wa Nigeria, Armando Guebuza wa Msumbiji, Moncef Marzouki wa Tunisia na Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.

Mbali ya viongozi hao, walikuwepo pia Dk Vera Songwe, Katibu Mtendaji wa UNECA; Dk Donald Kaberuka ambaye ni Rais wa zamani wa Benki ya Maendeleo Afrika (AfDB) na Dk Mukhisa Kituyi, Katibu Mkuu wa Mikutano ya Biashara na Maendeleo katika Umoja wa Mataifa.

Kwa mujibu wa Profesa Joseph Semboja, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Uongozi, mkutano huo ulilenga pia kuangalia mafanikio na kinyume chake katika ngazi ya taifa, ukanda na Afrika kwa ujumla.

HABARI LEO

No comments: