Advertisements

Tuesday, August 7, 2018

MABASI YAZUIWA KWENDA MIKOANI

Picha
MABASI 12 yanayofanya safari zake kutoka jijini Dar es Salaam kwenda katika mikoa mbalimbali nchini leo yamezuiwa kufanya safari baada ya kubainika kuwa na hitilafu.

Jeshi la Polisi limefanya uamuzi huo baada ya kufanya ukaguzi wa kushitukiza kwenye Kituo Kikuu cha Mabasi cha Ubungo.

Akizungumza kituoni hapo Mrakibu wa Jeshi la Polisi ambaye pia ni Mkuu wa Kitengo cha Elimu kwa Umma wa Kitengo cha Usalama Barabarani, Abel Swai amesema mabasi hayo hayataruhusiwa kuondoka mpaka yatengenezwe.

Ukaguzi huo uliofanywa katika kituo hicho ulibaini tatizo kubwa la mabasi yaliyositishiwa safari zake ni hitilafu katika mikono ya usukani ambapo yasipofanyiwa matengenezo yanaweza kusababisha ajali.

Pia Kamanda Swai alisema ukaguzi huo ni wa mara kwa mara na unafanyika kwa mujibu wa Sheria ya Usalama Barabarani ya Mwaka 2002 ili kudhibiti ongezeko la ajali nchini.

Katika hatua nyingine Mkuu wa Kitengo cha Sheria cha Jeshi la Polisi Kikosi cha Usalama Barabarani, Deus Sokoni amewatoa hofu madereva kufuatia agizo la ukaguzi wa leseni za udereva nchini.

"Hatutawanyang'anya leseni madereva wasio na vyeti ila tutahakikisha wanapata mafunzo maalumu ya udereva ili kumudu kuendesha kwa usalama na kuepusha ajali," amesema.

Kamanda huyo aliyasema hayo aliposimama kwa muda Kibaha Mkoa wa Pwani kufuatia ajali ya lori la mizigo lenye namba za usajili T 357 CXF kugongana uso kwa uso na lori jingine mbele ya Kituo cha Polisi Mlandizi jana ambapo mtu mmoja alikufa katika ajali hiyo.

HABARI LEO

No comments: