ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 28, 2018

LUGOLA AMSWEKA NDANI MKUU WA KITUO KIKUU POLISI MTWARA KWA KUSHINDWA KUWAWEKA WATUHUMIWA MAHABUSU

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimuuliza maswali Mkuu wa Kituo cha Polisi Mtwara mjini, Ibrahim Mhando (kushoto) baada ya kushindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne akiwemo Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Y&P Architects ambaye ni mshauri mkuu wa ujenzi wa Ofisi Kuu ya Uhamiaji Mkoani Mtwara. Katikati ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu. Wapili kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Lucas Mkondya. Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi. 
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kushoto) akimuonyesha Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mtwara, Lucas Mkondya (kulia), watuhumiwa ambao Mkuu wa Kituo cha Kati mjini humo, aliwaweka chumba cha upelelezi kituoni hapo badala ya mahabusu. Lugola alimsweka ndani Mkuu wa Kituo hicho pamoja na mahabusu hao
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola akitoka Kituo cha Polisi cha Kati mjini Mtwara mara baada ya kumsweka ndani Mkuu wa Kituo cha Polisi hicho ambaye aliwaweka watuhumiwa chumba cha upelelezi badala ya mahabusu kituoni hapo. Nyuma ya Waziri ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu. Kulia ni Kamanda wa Polisi Mkoa huo, Lucas Mkondya
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akifurahia jambo na Mkuu wa Wilaya ya Lindi, Shaibu Ndemanga wakati alipokua analikagua jengo la ofisi Kuu ya Uhamiaji Mkoa wa Lindi ambalo lililalamikiwa na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola (kulia) akimuangalia Mkurugenzi wa Ufundi wa Kampuni ya Ujenzi ya Lucas, ambaye pia kandarasi aliyejenga Jengo la Uhamiaji Mkoa wa Mtwara, Theophilius Kessy, wakati alipokua anambana maswali ya kutaka kujua kwanini Jengo la Uhamiaji Mkoa wa Mtwara limejengwa chini ya kiwango. Aliyeshika kitabu ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu.

Na Mwandishi Wetu, Mtwara

WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amemweka ndani Mkuu wa Kituo cha Polisi cha Kati mjini Mtwara (OCS), Ibrahim Mhando, kwa kushindwa kuwaweka mahabusu watuhumiwa wanne akiwemo Mhandisi Mshauri wa Kampuni ya Y&P Architects ambaye alitoa taarifa ya uongo kwa Waziri huyo kuhusu ujenzi wa Makao Makuu ya Uhamiaji Mkoani humo.

Tukio hilo lilitokea saa 12:46 asubuhi Agosti 27 leo Jumatatu, wakati Waziri Lugola na Katibu Mkuu wa Wizara yake, Meja Jenerali, Jacob Kingu walipofika Kituo hicho kikuu cha mkoa kwa kushtukiza wakati alipokua anakwenda Uwanja wa Ndege kwa ajili ya kurudi jijini Dar es Salaam, ndipo Waziri huyo alitaka kuthibitisha kama mtuhumiwa ambaye alielekeza jana usiku akamatwe awekwe mahabusu endapo Polisi walitekeleza agizo lake.

Hata hivyo, Waziri Lugola alimkuta mtuhumiwa huyo, Benjamin Kasiga akiwa chumba cha upelelezi badala ya kuwekwa mahabusu ya polisi hiyo, ndipo akamuuliza Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Lucas Mkondya, kwanini agizo lake halijatekelezwa.

“Hivi ndivyo polisi mnafanya hivi, haya ndio madudu mnayoyafanya? Tabia hii siku zote tunaipinga ikichafua Jeshi la Polisi, na hii ndiyo tabia yenu, najua ndio mana nimekuja ghafla, mnafahamu maadili ya Jeshi? RPC hawa polisi wako wanafanya nini, OCS njoo hapa, kwanini umeweka hawa watuhumiwa chumba cha upepelezi badala ya mahabusu, nawe unaingia ndani kwa kushindwa kuwaweka ndani hawa watuhumiwa, RPC muweke ndani sasa hivi huyu,” alisema Lugola akiwa amekasirika.

Hata hivyo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo (RPC), Mkondya alimweleza Waziri Lugola kituoni hapo kuwa, Polisi wake walifanya makosa kwa kutowaweka mahabusu watuhumiwa hao.

Kwa upande wake mkuu wa kituo huyo, Mhando kabla ya kuwekwa mahabusu pamoja na wale watuhumiwa ambao alishindwa kuwaweka mahabusu, alisema sababu kuu yakutowaweka mahabusu watuhumiwa hao ni kwasababu mahabusu ilijaa na wanafanya hivyo mara chache inapotokea mahabusu wamekuwa wengi kituoni hapo.

Waziri Lugola aliipinga kauli ya OCD huyo kuhusu mahabusu hiyo kujaa wakati nafasi ya kukaa watuhumiwa hao ilikuwepo ndani ya mahabusu hiyo, na watuhumiwa wangeweza kukaa bila tatizo lolote.

“Mbona nafasi ipo pale mahabusu, ile pale nafasi naiona, siwezi kukubaliana na uzembe huu, na hii ni tabia yenu huwa amnakamata watuhumiwa lakini baadhi hamuwaweki mahabusu, unanidanganya kuwa mahabusu imejaa, hii haikubaliki,” alisema Lugola.

Lugola ambaye alikua katika ziara ya dharura katika Mkoa wa Mtwara na Lindi, baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ulinzi na Usalama kugundua majengo ya uhamiaji mikoa hiyo pamoja na Gereza Ruangwa yamejengwa chini ya kiwango.

Aidha, akiwa wilayani Ruangwa, Lugola aliwataka wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama vilivyopo ndani ya Wizara yake kuwaondoa mara moja wananchi wote waliovamia katika maeneo ya majeshi nchini.

Lugola alisema hayo baada ya kulikagua Gereza jipya la Wilaya ya Ruangwa mkoani Lindi linalojengwa ambalo lina ekari 100 lakini ekari 20 limevamiwa kwa kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti, ufuta na korosho katika eneo hilo la Jeshi la Magereza.

Akizungumza baada ya kulikagua Gereza hilo, mjini Ruangwa, Lugola alisema kuanzia sasa viongozi wa vyombo vyake wahakikishe hawaruhusu mwananchi yeyote kuingia katika maeneo ya jeshi na atakua mkali kulifuatilia suala hilo.

Lugola ambaye pia aliikataa kuipokea taarifa ya ujenzi wa gereza hilo ambayo ilikua inasomwa na Mkuu wa Magereza Mkoa wa Lindi, Rajabu Nyange, alisema taarifa hiyo ina upungufu mkubwa na hawezi kuipokea licha ya kua imeeleza kuhusu ardhi ya jeshi hilo kuvamiwa.

“Mimi huwa nashangaa sana inakuaje wananchi wanavamia ardhi ya jeshi tena bila woga, halafu jeshi linakaa kimya linabaki kunung’unika, hii haijakaa sawa kabisa na kamwe sikubaliani nalo,” alisema Lugola.

Lugola aliongeza kua, “uvamizi wa ardhi mara nyingi unakua kwa jeshi la polisi na magereza, mbona Jeshi la Wananchi silisikii hili, kwanini nyie mnakaa kimya wananchi wakivamia ardhi yenu, sasa nawataka muhakikishe ardhi ya jeshi popote nchini iliyoporwa inarudishwa ndani ya jeshi, na wote waliovmia waondooeni haraka iwezekanavyo.”

Kwa upande wake Mkuu wa Magereza mkoani humo, alisema licha ya ujenzi wa gereza hilo kuendelea kujengwa lakini ekari 20 ilichukuliwa kimakosa na kujengwa kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti na ufuta pamoja na kubangua korosho vinavyomilikiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Ruangwa.

“Jitihada za ufuatiliaji urejeshaji wa eneo hilo zimefanyika ambapo Mkurugenzi wa Halmashauri hii ameonyesha nia ya kurejeshwa eneo hlo,” alisema Bakari.

Aliongeza kuwa, ujenzi wa gereza hilo ambalo linatarajiwa kukamilika Septemba mwaka huu, unatarajiwa kumaliza msongamano wa wafungwa na mahabusu kwenye Gereza la Wilaya ya Nachingwea kutokana na mahabusu wengi kutoka Ruangwa.

Waziri Lugola alifanya ziara ya dharura katika mikoa hiyo, pia aliambatana na Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Meja Jenerali, Jacob Kingu kwa kufanya ziara ya kutembelea Jengo lililokwama ujenzi la uhamiaji Mkoa wa Mtwara na Lindi na pia kulitembelea Gereza la mahabusu na wafungwa linalojengwa mjini Ruangwa, mara baada ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kubaini mapungufu ya ujenzi wa majengo hayo.

Mwisho/-

1 comment:

Anonymous said...

Bongo tusifikie stage hii mbaya ya kuwadhalilisha watumishi wa serikali. Mheshimiwa Waziri Lugola, huyo OCD ni bwana na baba, kumdhalilisha kwa kosa dogo kama hili is unimaginable. Huu udikteta in a long run utatuporomosha. Watanzania tunahitaji viongozi wenye busara na hekima rather than ones with dictatorial mentality.