Advertisements

Monday, August 13, 2018

NAIBU WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII, JAPHET HASUNGA ATEMBELEA HIFADHI

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (katikati) akizungumza na kamati ya ulinzi na usalama ya wilaya ya kilosa mara baada ya kumaliza kufanya mkutano wa Menejimenti ya Hifadhi ya taifa ya Mikumi uliofanyika jana katika ofisi za Hifadhi hiyo wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Adam Mgoyi.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Japhet Hasunga (katikati) akizungumza jambo na Mkuu wa Hifadhi ya Taifa ya Mikumi, Bw. Godwell Ole Meng’ataki (kushoto) mara baada ya kumaliza kufanya mkutano wa Menejimenti ya Hifadhi ya taifa ya Mikumi uliofanyika jana katika ofisi za Hifadhi hiyo wilayani Kilosa mkoani Morogoro. Wwengine ni Kulia ni Mkuu wa wilaya ya Kilosa, Mhe. Adam Mgoyi. 

NA MWANDISHI WETU, KILOSA

SERIKALI imesema inaandaa kanuni zitakazoruhusu kufanyika uwindaji wa kiasili (Local Hunting) kwenye maeneo ya wazi kwa ajili ya kitoweo ili wananchi waweze kunufaika moja kwa moja na Maliasili zao ili waone umuhimu wa kuhifadhi.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga amesema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi ikiwa ni muendelezo wa ziara zake za kikazi mkoani Morogoro kwa ajili ya kutatua changamoto mbalimbali zinazoikabili Maliasili, Malikale na Uendelezaji Utalii.

Amesema wawindaji hao watapewa vibali maalum vitakavyowawezesha kuwinda kwa ajili ya kujipatia vitoweo vya nyamapori na kutakuwa na maeneo maalum kwa ajili ya kuuzia vitoweo hivyo kwa jamii.

Aidha, Ametaja aina za vitoweo vitakavyokuwa vinauzwa kwenye maeneo hayo maalum ikiwa pamoja na nyama ya mamba, nyati,swala viboko na wengineo.

Kwa upande wake, Mhifadhi Mkuu wa Hifadhi za Taifa za Mikumi, Godwell Ole Meng'ataki amesema kama kutakuwa na utaratibu mzuri itaweza kusaidia kuongeza mapato kwa nchi.

Aliongeza kuwa utaratibu huo wa kuwa na sehemu maalum ya kuuzia vitoweo si mgeni kwa vile nchi kama Afrika Kusini wamekuwa wakifanya hivyo na pia wana maeneo maalum kwa ajili ya kuuzia viteweo vya nyamapori.
Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga (wa kwanza kushoto) akizungumza na baadhi ya watalii wa ndani aliokutana nao jana wakati alipotembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi kwa ajili ya kuzungumza na Menejimenti ya Hifadhi hiyo.

Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga akizungumza na Menejimenti ya Hifadhi ya Taifa ya Mikumi wakati alipowatembelea jana katika ofisi za Hifadhi hiyo wilayani Kilosa mkoani Morogoro

No comments: