ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, August 29, 2018

SHIMO LA PANYA HALIZIBWI KWA MKATE

ALIYEKU-DANGANYA siku hizi maneno ya kwenye kanga yanatumika kuchamba nani? Heeeeeloooo utajibeba mwaka huu kama siyo kujiangusha, upo nyonyo?

Siku hizi vigodoro ndiyo habari ya mjini, weka spika mi niweke mduara tukuchambe mpaka kunakucha, wee kalia na kubadili kanga zenye maneno ya kizamani, mara ohh wee wasusa siye twala, utaliwa mwenyewe wenzako tunapeta, heee heeeiyaaaa! Tafuta kazi ufanye shoga umbeya hauna mshahara! Kama ulikuwa hujui jua sasa, papai la kuiva halibonyezwi, utaliona lenyewe limebadilika rangi, upo?

Shoga baada ya kukupa udambwiudambwi huo, leo bado tena nipo kwa hawahawa kinababa, nakwambia mwaka huu lazima wanyooke, kama walikuwa hawajui kutamka chai watasema chei! Juzi nilipata meseji kwa msomaji roho ikaniuma sana, nikajiuliza usiku kutwa kwa nini tufanyiwe sisi tu kina mama? Sawa wakati mwingine huwa tunalalamika sana lakini malalamishi yetu yanasababishwa na haohao kinababa! Tena wengine wamekataa kona wanakubali penati kirahisi!

Kama mapenzi ni pesa nenda kafunge ndoa na benki! Basi shoga msomaji wangu alikuwa akinilalamikia tabia chafu ya mumewe aliyoianzisha mbaya zaidi amefikia hatua ya kumtishia maisha endapo atasikia maneno hayo kwa watu! Sasa nikupashe tu wewe baba, dawa ya maji ni moto japo hayachomi nyumba, kama ulikuwa hujui kwangu yameshafika na wasomaji wote watayajua ili iwe funzo kwa wale wengine wenye tabia kama hiyo!

Katika meseji aliyonitumia msomaji wangu alikuwa akilalamika tabia chafu aliyoianzisha mumewe kwake, aliandika hivi; “Anti Naa, pole kwa majukumu, nimekuwa nikizisoma sana makala zako za kuelimisha watu, kiukweli napendezwa na unachoandika kwani kinatufunza sana.

“Kilichonifanya niandike haya, nina mume wangu ambaye bado hatujabahatika kupata mtoto licha ya kufunga naye ndoa miaka miwili iliyopita. Anti Naa, bwana wangu amekuwa na tabia ya kunitaka kuniingilia kinyume na maumbile, nimejaribu kumkatalia sana lakini amekuwa mkali na kunitishia maisha, kuna siku moja tu alinishikia kisu nikafanikiwa kupiga kelele akaniachia, hata meseji hii ninayokuandikia, akiiona nahisi kabisa ataniweka katika hali ya hatari. Nitunzie jina langu.” Aliandika msomaji huyo.

Nikugeukie sasa na wewe mbaba mwenye tabia hii, hivi jamani ndo tuseme mitandao inawaharibu au? Hii michezo siyo kwa msomaji huyu tu, nimekuwa nikipata meseji nyingi zikiwalaumu watu wa aina hii, kwa nini lakini? Nyie wanawake mnaotendewa hivi, tena muwaambie kabisa hao wanaume ipo siku, dawa yao ipo jikoni, sishindwi kitu miye! Usione ukubwa wa tingatinga ukajua utanishindwa nafasi ya dereva ni ileile, upo shoga?

Haya basi, wengine wakiona wananyimwa hivyo vitendo vichafu wanakimbilia kwa michepuko au kwa watu wanaowakubalia ujinga huo! Shuuutuuuuu! Tangu lini shimo la panya likazibwa kwa mkate? Baiskeli ya kawaida imekushinda, pikipiki utaweza?

Badilikeni nyie wanaume, michezo kama hiyo ni hatari siyo kwako tu hata kwetu siye wanawake! Supu haichotwi kwa uma! Ukisikia mwanaume anang’ang’ania hayo mamichezo angalia akili yake, huenda ameharibikiwa na kitu, tena akizidi kukusumbua mlete jina lake kwangu kama sijamuanika hadi na eneo analoishi.

Kwa leo sitaki kuongea mengi lakini, nawaambia tu nyie kinababa dawa yenu inachemka, sitachoka kuwasema hadi mbadilike!

Ni mimi Shangingi Mstaafu, Anti Nasra. GPL

No comments: