Advertisements

Wednesday, August 8, 2018

Tundu Lissu Aruhusiwa Kutoka Hospitali, Atakaa na Chuma kwa Miezi 6 Zaidi

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu ameruhusiwa kutoka hospitalini alipolazwa kuanzia sasa ataishi nyumbani.

Tangu Septemba 7 mwaka jana aliposhambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 jijini Dodoma, Lissu amekuwa akiishi hospitalini kwa matibabu zaidi.

Ujumbe wa Lissu alioutoa jana  Agosti 7, 2018ulisema; “Hello Friends of Me!!! Good afternoon to y'all. Kwa mara nyingine nawaleteeni habari njema."

Alisema alfajiri ya Januari 6, 2018 aliondoka Hospitali ya Nairobi  nchini Kenya na kusafiri hadi Leuven nchini Ubelgiji, kwa ajili ya matibabu zaidi.

Lissu alisema  Agosti 6, 2018 alitimiza miezi saba tangu alipowasili nchini humo.

“Agosti 7 ni miezi 11 toka siku niliposhambuliwa na watu wanaojulikana sana kama 'watu wasiojulikana.'"

"Septemba 7 mwaka jana sikulala nyumbani kwangu. Agosti 7 ya leo, miezi 11 kamili baadae, nimeamkia nyumbani kwangu," alisema Lissu.

Aliongeza:  "Septemba 7 iliyopita wote mlikuwa na hofu kubwa kama ningemaliza siku hiyo au siku chache zilizofuata, nikiwa hai. Miezi 11 kamili baadae, Professor Dk Wilhelmus Jan Mertsemakers, daktari wangu tangu nilipokuja University Hospital Leuven, amesema sina sababu ya kitabibu ya kuendelea kukaa hospitali."

"Profesa Mertsemakers amesema nitaendelea na uponyaji nikiwa nyumbani kwangu. Nitatembelewa na  wauguzi kila siku nyumbani kuniangalia naendeleaje. Na nitarudi hospitali kumwona kila baada ya wiki mbili," alisema Lissu.

Katika ujumbe huo,  Lissu aliendelea kusema, bado ana chuma kubwa kwenye paja .

“Liko kama antenna ya TV za mwaka '47 na Profesa Mertsemakers amesema nitakaa nalo kwa si chini ya miezi sita. Lakini habari ya mujini ndio hiyo: nimetoka hospitalini."alisema na kuongeza;

"Hongereni sana kwa kazi nzuri ya kuniuguza na kuniponya na chochote mtakachokula au kunywa siku ya leo mnibakishie. Siko mbali."

1 comment:

Anonymous said...

Congrats for the good news our brother Lissu! Mwenyezi Mungu ataendelea kukubariki. Na wale "wasiojulikana" waliokutendea maovu nao watakipata chuma siku moja na kulia mpaka kiama.