Viongozi wa zamani wa Chama Cha Ushirika Kagera (KCU 1990 Limited) wataendelea kusota rumande baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Bukoba mkoa wa Kagera kuwanyima dhamana kutokana na kukabiliwa na mashtaka ya kuhujumu uchumi kwa ubadhilifu wa shilingi Milioni 218 wanaodaiwa kuufanya.
Akisoma uamuzi kuhusu ombi la washitakiwa kutaka wapatiwe dhamana jana Agosti 27, 2018 hakimu mkazi mfawidhi, John Kapokolo alisema mahakama hiyo haina uwezo wa kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kutaka maombi yao yapelekwe kwenye mahakama sahihi.
Akizungumza mara baada Hakimu Kapokoro kutoa uamuzi huo, mwendesha mashaka wa serikali alisema mahakama hiyo haina mamlaka ya kutoa dhamana kwa watuhumiwa hao kwa kuwa baadhi ya tuhuma zinazowakabili zinahusiana masuala ya kuhujumu uchumi.
Kufuatia uamuzi huo wakili anayewatetea watuhumiwa hao, Aron Kabunga alisema mahakama hiyo haikuwatendea haki wateja wake kwani mahakama hiyo haikuwa na sababu zozote za kuwanyima dhamana hadi kesi hiyo itapotajwa tena Septemba 10, mwaka huu.
Washitakiwa hao John Binunshu aliyekuwa mwenyekiti wa bodi, Vedastus Ngaiza aliyekuwa meneja mkuu na Bestina Rwebangira walifikishwa katika mahakama hiyo wiki iliyopita na kusomewa mashitaka matano.
Mashtaka yaliyosomwa na wakili mwandamizi wa Serikali, Athumani Matuma ni kula njama, matumizi mabaya ya ofisi, matumizi mabaya ya madaraka, kughushi nyaraka na kuhujumu uchumi na kusababisha hasara ya Sh124 milioni.
Wakili wa washitakiwa Aaron Kabunga alipinga hati ya mashitaka kuwa iliunganisha makosa ya uhujumu uchumi na mengine bila kuwa na kibali cha mkurugenzi wa mashitaka na hivyo alitaka hati hiyo itupiliwe mbali na wateja wake wapewe dhamana.
Tayari Serikali Ilishavunja Uongozi huu uliofikishwa mahakamani na kuchagua uongozi mpya unaokiendesha chama hicho cha Ushirika KCU 1990 Ltd.
No comments:
Post a Comment