ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, August 28, 2018

Serikali yathibitisha kuwepo kwa saruji ya kutosha nchini, Wanaopandisha Bei Kiholela Kunyang’anywa Leseni


Serikali imethibitisha kuna saruji ya kutosha nchini baada ya kuwepo kwa hifadhi ya Tani 16,000 kwa jana pekee ambapo uzalishaji ukiendelea vizuri utafikia Tani Milioni 5.8 kwa mwaka wakati mahitaji ya mwaka ni tani Milioni 4.8.

Kutokana na hali kuwa hivyo, Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Charles Mwijage amewaagiza watengenezaji saruji kuwafutia leseni mawakala ambao watabainika kupandisha bei huku pia akitumia fursa hiyo kuwakaribisha wageni kutoka nje kuja kununua saruji nchini.

Mwijage ametoa kauli hiyo jana Agosti 27, 2018 jijini Dar es Salaam wakati alipotembelea kiwanda Tanzania Portland Cement (Twiga)  kilichopo Wazo na Camel Cement Company kilichopo Mbagala.

Akizungumza na uongozi wa kiwanda kinachozalisha saruji ya Twiga, Mwijage alisema lazima baadhi ya mawakala watolewe kafara ili kudhibiti hali hiyo.

Pia ameuagiza uongozi wa kiwanda hicho kumpatia orodha ya mawakala wote wanaosambaza bidhaa hiyo pia waagizwe kushusha bei ya saruji  ambayo sasa imepaa hadi Sh 18,000 katika baadhi ya maeneo.

“Mimi nimefanya kazi hapa miaka 18, nafahamu mchezo wote wa vijana wako wanaoufanya, ndio maana nakuagiza uniletee orodha ya mawakala wote wanaosambaza saruji ili niwabaini na kuwafutia leseni.

“Kwa sababu sasa Dangote anazalisha tani 4,500 kutoka tani 2000 kwa siku, Twiga anazalisha tani 6,000 kutoka tani 3,500 kwa siku, Tembo tani 1,100, Nyati tani 2,000 hivyo hakuna uhaba wa saruji sasa. Tayari hali imetangamaa ila kwanini bei iendelee kubaki juu.

“Kiujumla kwa siku tunazalisha tani 16,000 na sasa tunatumia tani milioni 5.8 kutoka tani milioni 4.8 kwa mwaka na viwanda vyote vilivyosimikwa sasa vina uwezo wa kuzalisha tani milioni 10.5 kwa mwaka,” alisema.

Aidha, alisema ili kuendelea kuhimili soko la ndani na la nje, tayari kuna viwanda vitatu ambavyo ni cha Mamba,  Nyati namba 2 na kiwanda cha wachina cha Engian ambacho kitakuwa na uwezo wa kuzalisha malighafi inayotumika kuzalisha saruji (clinker) zaidi ya tani milioni saba kwa mwaka.

“Suala hili la saruji kupanda, naomba watu wanivumilie, dawa ya kupanda naijua, saruji imejaa sokoni, bei inashuka yenyewe, ila wale wanaopandisha inaitwa ‘profiteering’ siku ya kiama inshallah basi hukumu ni yao kama wanataka kuishi duniani shauri yao hukumu ni yao.

Aidha, Meneja Undelezaji Biashara wa Kampuni ya Saruji ya Twiga (TPCC), Mhandisi Danford Semwenda  ni kazi ngumu kuwadhibiti mawakala wa uuzaji wa saruji hiyo hivyo wanaomba ushirikiano kutoka serikali ili kudhibiti hali hiyo.

Kwa upande wake Meneja Mkuu Msaidizi wa Kiwanda cha Camel, Ghalib Hassan Ghalib  alisema kutokuwapo kwa umeme wa uhakika nao umekuwa kikwazo kwa kiwanda hicho kufikia malengo ya kuzalisha tani 600 kwa siku na hivyo kuzalisha tani 400.

No comments: