Mkuu wa Wilaya ya Tabora Kitwala Komanya(kulia) akizungumza na wakazi wa Manispaa ya Tabora jana wakati wa maadhimisho ya siku ya usafi duniani. Katikati ni Mkuu wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri na kushoto ni Mkuu wa Idara ya Mazingira wa Manispaa ya Tabora William Mpangala
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Tabora na wasafiri wakimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Tabora (hayupo katika picha) jana wakati wa maadhimisho ya siku ya usafi duniani.
Na Tiganya Vincent
MKUU wa Mkoa wa Tabora Aggrey Mwanri ameuagiza uongozi wa Manispaa ya Tabora kuhakikisha wanajenga banda kwa ajili ya abiria kupumzikia wakati wakisubiri usafiri au wanapowasili.
Alisema baadhi ya wasafiri wamekuwa na watoto wadogo na wazee ambao wamekuwa wakipata shida ya sehemu ya kujikinga na jua au mvua wakati wa masika.
Mwanri alitoa kauli hiyo jana kufuatia malalamiko kutoka kwa wasafiri wakati akiwa katika maadhimisho ya Siku ya usafi Duniani ambapo Kimkoa yalifanyika katika eneo la Stendi mpya ya Manispaa ya Tabora.
Alisema wanacholalamikia wasafiri kiko sahihi Stendi hiyo haina sehemu ya wasafiri kumpuzika wakati wakisubiri usafiri wa kuendelea au wale wanaowasubiri ndugu zao wawapokee.
Mkuu huyo wa Mkoa alisema ni vema wakatumia sehemu ya fedha wanazokusanya katika Stendi hiyoo kwa ajili ya kuwawekea mazingira mazuri na ambayo ni rafiki kwa wasafiri wote.
Mwanri alisema wakati wanasubiri kuanza ujenzi wa Stendi ya kisasa nje ya mji kwa kutumia fedha kutoka Benki ya Dunia ni vema wakarekebisha kasoro zilizopo katika Stendi ya sasa ili watumiaji wafurahie huduma zake.
Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Tabora William Mpangala alisema watahakikisha wanafanyia marekebisho na kuongeza kuwa mpango wa muda mrefu ni kujenga Stendi ya kisasa nje ya mji ambayo itakuwa na huduma zote muhimu kwa ajili ya abiria.
No comments:
Post a Comment