ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, September 26, 2018

Rais Magufuli kuwa Mgeni Rasmi Kampeni ya Uzalendo na Utaifa

 Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) leo jijini Dar esa Salaam, kuhusu maadhimisho ya Kampeni ya Uzalendo na Utaifa kwa mwaka huu kuwa itafanyika Desemba O8  Jijini Dodoma na Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Baadhi ya Watendaji mbalimbali wa Taasisi za Serikali na wandishi wa habari wakimsikiliza kwa makini Mheshimiwa Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt.Harrison Mwakyembe (hayupo pichani) alipokuwa akitangaza maadhimisho ya Kampeni ya Uzalendo na Utaifa utakaofanyika Desemba Mwaka huu jijini Dodoma.



Na Anitha Jonas – WHUSM
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mheshimiwa  Dkt. John Pombe Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika Kampeni ya Uzalendo na Utaifa ambayo itafanyika  Desemba 08 Mwaka huu  Jijini Dodoma.
Hayo yamebainishwa leo Jijini Dar es Salaaam na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo  Mheshimiwa Dkt. Harrison Mwakyembe alipokuwa akitangaza utaratibu wa Kampeni hiyo ambayo ni endelevu yenye lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu uzalendo na kutunza mali za nchi bila kuwa na maslahi binafsi.
Akielezea kuhusu Kampeni hiyo Waziri Mwakyembe amewataka watanzania kuwa wazalendo kwa kutumia lugha ya Kiswahili popote  duniani bila kuona aibu kwani ni moja ya lugha mashuhuri na watanzania wote wanakila sababu ya kujivunia mafanikio ya lugha hiyo sababu kwa nchi za Afrika Tanzania ndiyo nchi ya kwanza kuitangaza lugha hii kuwa lugha ya Taifa.
“Mafanikio ya ukuaji wa Lugha ya Kiswahili yanatokana na jitihada za watanzania katika matumizi ya lugha hiyo kwani Kiswahili ni lugha ya kumi katika lugha elfu sita zinazoongelewa sana Duniani na katika kuweka msisitizo wa suala la watanzania kuwa wazalendo ni muhimu watanzania kutumia lugha hii wakiwa na ujasiri kama ilivyo kwa mataifa mengine yanayotumia lugha zao pasipo aibu”,alisema Dkt.Mwakyembe.
Naye Mdau wa Kampeni ya Uzalendo nchini Msanii Mrisho Mpoto alifafanua kuwa kila lugha inakopa kutoka kwa lugha nyingine hivyo pamoja na watanzania kusisitizwa kuzungumza lugha ya Kiswahili lakini hii haina maana kuwa hatutakiwi kujifunza lugha za wenzetu cha msingi ni kuitumia  lugha hiyo zaidi hata kama unaweza kuzungumza lugha nyingine za kigeni kama ilivyokwa mataifa ya wenzetu waliyoendelea.

“Lugha ni Utamaduni na ndiyo utambulisho wa taifa la mtu hivyo kwa kuonyesha Uzalendo na Utaifa ni vyema sisi Watanzania kuhakikisha tunatumia lugha hii ipasavyo kwani dunia inafahamu kuwa sisi ndiyo wa asisi  wa lugha hii adhimu”,alisema Msanii Mpoto.
Halikadhalika nae Kaimu Mkurugenzi Idara ya Sanaa kutoka Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Bibi.Leah Kihimbi alieleza kuwa kampeni hiyo ya Uzalendo kwa sasa itakuwa na shughuli mbalimbali ikiwemo kuendesha mijadala na makongamano yatakayo jadili changamoto mbalimbali za lugha ya Kiswahili katika kusimamia uzalendo wa Taifa.
Aidha, Mheshimiwa Dkt. Mwakyembe aliwataka wataalamu wa lugha ya Kiswahili nchini kuacha kusuasua katika suala la kujiandikisha katika Kanzi Data inayoratibiwa na Baraza la Kiswahili La Taifa (BAKITA) kwani kanzi data hiyo inaumuhimu na njia moja wapo ya kuwa ongezea fursa za ajira.
Hata hivyo Waziri Mwakyembe ameeleza kuwa mwaka huu Kampeni hiyo ya Uzalendo imebeba Kauli Mbiu ya “Kiswahili Uhai Wetu  na Utashi Wetu” na pia amewataka wazazi majumbani kuwa mabalozi wa kwanza wa kusimamia Maadili na Uzalendo kwa Taifa na pia.

No comments: