Posted On: October 17th, 2018
Taasisi ya HEAD Inc. inayongozwa na Watanzania wanne waishio Nchini Marekani, imetoa msaada wa fremu za Miwani zenye thamani ya Shilingi Milioni 14 za Kitanzania kwa Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kusaidia Wananchi na kuimarisha kitengo cha Macho katika Hospitali hiyo.
Msaada huo umetolewa leo na mmoja wa Viongozi wa Taasisi hiyo Ndg. Mayor Mlima, alipotembelea Hospitalini hapo na kukutana na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bagamoyo pamoja na timu ya uendeshaji huduma za Afya ndani ya Halmashauri CHMT’s ikiongozwa na Daktari Mkuu wa Wilaya Dr. Sylivia Mamkwe.
Bw. Mayor amesema, yeye na wenzake watatu wanaounda taasisi ya HEAD Inc. (Health, Education and Other Development Incorporation) ambao ni Watanzania waishio Nchini Marekani, walioungana kwa ajili ya kujitolea misaada hasa ya Afya Nchini.
“Tumeamua kujiunga na kujitolea misaada katika sekta za Afya, Elimu na mambo mengine yahusuyo maendeleo Nchini na kwa mara ya kwanza tumeamua kufika na kutoa msaada katika Hospitali ya Wilaya ya Bagamoyo ili kusaidia Wananchi wenye matatizo ya Macho waweze kupatiwa huduma ya miwani bure bila kugharimia chochote lakini pia kukiimarisha kitengo cha Macho katika Hospitali hii ya Wilaya” Anasema Bw. Mayor
Nae Ndg. Julius Mwang’anda aliemwakilisha Mkurugenzi Mtendaji katika mapokezi hayo, ameishukuru sana taasisi hiyo ya HEAD Inc. kwa msaada huo ambao amekiri kuwa utawasaidia sana Wananchi kuweza kupata huduma hiyo ya miwani kwa urahisi wafikapo katika Hospitali hiyo ya Wilaya na kuiomba taasisi hiyo kutoishia hapo bali waikumbuke tena Bagamoyo kila watakapopata nafasi na kuipa misaada hata katika nyanja zingine kama Elimu, Maji n.k ili tu kuiletea Bagamoyo maendeleo na kumsaidia Mwananchi wa hali ya chini.
Taasisi ya HEAD Inc. imekuwa ikitoa misaada katika Sekta za Afya Nchini na kwa Mwaka huu wametoa huduma ya kliniki tembezi katika Hospitali ya Mji Kondoa na katika Hospitali ya Kijenge na Makunduchi huko Unguja kwa kushirikiana na madaktari bingwa wa wanawake, watoto na ngozi toka Hospitali ya Mnazi Mmoja ya huko Unguja ambapo walitoa huduma za utafiti na tiba.
No comments:
Post a Comment