ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 15, 2018

NEC YATANGAZA TAREHE YA UCHAGUZI MDOGO SERENGETI, SIMANJIRO NA KATA 21 ZA TANZANIA BARA

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetangaza Tarehe mbili Desemba (Desemba 2, 2018) kuwa siku ya Uchaguzi Mdogo kwenye Jimbo la Simanjiro, Serengeti na kata 21 za Tanzania Bara.

Akitoa taarifa kwa umma Jijini Dar es Salaam  leo (Jumatatu Oktoba 15, 2018), Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) Jaji wa Mahakama ya Rufaa Semistocles Kaijage amesema fomu za Uteuzi  wa  Wagombea zitatolewa kati ya  tarehe 28 Oktoba hadi 03 Novemba mwaka huu.

“Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 03 Novemba mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kuanzia tarehe 04 Novemba hadi tarehe 01 Desemba mwaka huu na siku ya Uchaguzi itakuwa ni tarehe 2 Desemba, mwaka huu,” Jaji Kaijage amesema.

Mwenyekiti huyo wa Tume amesema kwamba Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika Majimbo mawili (2), Jimbo la Serengeti lililopo Halmashauri ya Serengeti Mkoani Mara na Jimbo la Simanjiro katika Halmashauri ya Simanjiro Mkoani Manyara.

Jaji Kaijage alisema kwamba barua hiyo imepokelewa kufuatia Wabunge wa Majimbo hayo Waheshimiwa Marwa Ryoba Chacha,  na James Ole Millya kujiuzulu na kutoka  kwenye Chama vyama vyao vya awali.

Amesema Tume pia imepokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana na Serikali za Mitaa ambaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, aliitaarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 21 za Tanzania Bara.   Nafasi hizo wazi zimetokana na sababu mbalimbali ikiwemo vifo na kujiuzulu.

“Tunapenda kuvikumbusha Vyama vya Siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yanayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi chote cha Uchaguzi huu mdogo,” alisema.

Kata zenye uchaguzi nah almashauri zao kwenye mabano ni pamoja na Ilboru, Mlanfarini na Oldonyosambu (Wilaya ya Arusha), Engutoto na Olasiti (Manispaa ya Arusha), Hazina (Manispaa ya Dodoma), Chinugulu (Wilaya ya Chamwino), Kasharu, Nyakimbili, Kishongo (Wilaya ya Bukoba), Chonyonyo, Ihanda (Wilaya ya Karagwe).

Nyingine ni pamoja na Muhindawa, Mnanila (Wilaya ya Buhigwe), Mnerongongo (Wilaya ya Nachingwea) Ngarenairobi (Wilaya ya Siha), Kyanyari (Wilaya ya Butiama), Namilembe (Wilaya ya Ukerewe), Lukanga, Beta (Wilaya ya Mkuranga) na Chikola (Wilaya ya Manyoni)

No comments: