ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, October 3, 2018

Polisi Marekani kumwanika Ronaldo

Las Vegas, Marekani.Mshambuliaji nguli wa Juventus ‘Kibibi Kizee’ cha Turin, Cristiano Ronaldo ameanza kuchunguzwa na Polisi wa Marekani kwa tuhuma za ubakaji.

Polisi wa Las Vegas wamekabidhiwa jalada na Mahakama kufanya upepelezi kuhusu tuhuma za nahodha huyo wa Ureno anayedaiwa kumbaka Kathryn Mayorga.

Taarifa ya Polisi imekuja siku moja baada ya mwanamke huyo kujitokeza hadharani, kudai alibakwa na Ronaldo mwaka 2009 walipokutana hotelini Las Vegas.

Mwanamke huyo ameweka kwenye mtandao picha alizopiga na mshambuliaji huyo wa zamani wa Real Madrid wakiwa katika moja ya klabu za usiku.

Kathryn mwenye miaka 34, amefichua madai hayo baada ya mwanasheria wake kufungua kesi mahakamani akidai tukio hilo lilitokea bafuni kwenye Hoteli ya Palms and Casino mjini Las Vegas, Juni 13, 2009.

Hata hivyo, Ronaldo amekanusha taarifa hizo akidai zina lengo la kumchafua na mwanamke huyo anataka kupata umaarufu kupitia jina lake ingawa tayari mwanasheria wake Christian Schertz, anajiandaa kulishitaki gazeti la Der Spiegel la Ujerumani lililochapisha habari hiyo kwa mara ya kwanza.

Tayari mwanasheria wa Kathryn amefungua kesi Mahakama ya Wilaya ya Clark County Ijumaa iliyopita na katika maelezo yake alidai alibakwa mara kadhaa.

Awali, Kathryn anayedai kuwa alikuwa mwalimu wa wanamitindo wakati huo, alisema alikaa kimya muda mrefu sababu aliahidiwa fedha na Ronaldo, ingawa katika maelezo alidai aliogopa aibu.

mwanaspoti

No comments: