Advertisements

Wednesday, October 10, 2018

SERIKALI KUWAFUTIA USAJILI MADAKTARI WATAKAOFICHA USHAIDI VITENDO VYA UKATILI

Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katikati pamoja na Naibu wake Dkt. Faustine Ndugulile kushoto wakiwa na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Tellack katika picha yenye mabango ya kupinga ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni kabla ya kushiriki mdahalo wa siku moja kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Waziri wa Afya ,Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Ummy Mwalimu na Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Bi. Zainabu Tellack wakipata maelekezo kutoka kwa mfanyakazi wa shirika la Save the Children Bi. Neema Bwaira walipotembelea Banda la Maonesho la Shirika hilo kabla ya kushiriki mdahalo wa siku moja kupinga vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.
Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. John Jingu akitoa hotuba kwa mgeni rasmi mdahalo wa Kitaifa wa kutokomeza ukeketaji, mimba na ndoa za utotoni unaondelea leo Jijini Dar es Salaam kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike.(PICHA ZOTE NA KITENGO CHA MAWASILIANO WAMJW)

NA MWANDISHI WETU- DAR ES SALAAM

SERIKALI itafuta usajili kwa madaktari wote watakaobainika kukiuka viapo vyao kwa kuficha ushahidi kwa watoto wahanga wa ukatili kwa sababu ripoti ya utabibu ni ushaidi muhimu kuwatia hatiani wale wote wanaofanya ukatili dhidi ya wanawake na watoto.

Hayo yamesemwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mdahalo wa Kitaifa wa kutokomeza Ukeketaji, Mimba na Ndoa za utotoni nchini.

Waziri Ummy Mwalimu amewataka madaktari hao kuandika ukweli kwasababu wanawake na watoto ambao wamekuwa wakifanyiwa vitendo vya ukatili na kukosa ushaidi wenye nguvu kutokana na Madaktari kutoa ripoti inayokinzana na uhalisia hivyo kuzidisha vitendo hivyo dhidi ya wanawake na watoto.

Waziri Ummy amevitaja vitendo vya ukatili kuwa tishio kwa mtoto wa kike kwakuwa kwa kila kundi la wasichana 100 wenye umri chini ya miaka 18 kati yao watoto 27 ni wahanga wa mimba na ndoa za utotoni na wasichana 10 kati ya 100 kwasasa wamefanyiwa ukatili wa ukeketaji.

Aidha Waziri Ummy akiongea kuhusu ndoa za utotoni amesema kuwa hapa nchini robo tatu ya wanawake wote wameolewa katika umri chini ya miaka 18 akiitaja mikoa ya Katavi, Tabora, Shinyanga, Mara na Lindi kuwa na viwango vikubwa vya mimba na ndoa za utotoni.

Aidha Waziri Ummy aliwaambia wajumbe wa mdahalo huo kuwa Serikali imefanya juhudi kubwa kuhakikisha inapambana na vitendo vya ukatili dhidi ya watoto baada ya serikali kufanya mapitio ya Sheria ya elimu sura ya 353 inayotoa kifungo cha miaka 30 kwa yoyote atakaye mpa mimba au kumuoa msichana aliyeko shule.

‘’Pamoja na uwepo wa Sheria hii pia nimemwandikia barua Waziri wa TAMISEMI kuwakumbusha walimu wakuu wote nchini kuhakikisha wanawasilisha takwimu za wasichana wote wanaolewa au kupata mimba kwa Kamishna wa Elimu nchini kila robo mwaka” alisisitiza Waziri Ummy.

Aidha Waziri Ummy alisema kuwa Sera ya Elimu bure imewezesha wasichana wengi nchini kupata fursa zaidi ya kupata elimu tofauti na awali ambapo wazazi walichagua kutoa kipaumbele kwa mtoto wa kiume kwa madai ya wazazi kushindwa gharama za masomo.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Mara Bw. Adam Malima akiongea katika mdahalo huo ameutaja Mkoa wa Mara kuwa ndio kitovu cha ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto akisema ukatili dhidi ya wanawake na watoto umejificha katika kivuli cha mila na desturi za Mkoa huo.

Mkuu huyo wa Mkoa amesema kwa Mkoa wa Mara vitendo vya ukeketeji ni sehemu ya mila na desturi na unapochagua kupambana na ukatili huo utangundua kuna mambo mengi yaliyojificha nyuma pazia na vigumu kupata ushirikiano kutoka kwa jamii kwasababu ya kuogopa kupata matatizo hata kama kuna lengo la kutoa ushirikiano.

Aidha Mkuu huyo wa Mkoa wa Mara aliwaambia wajumbe wa mdahalo kuwa kumekuwepo na msemo wa uwongo kuwa wanawake Mara wanapenda kupigwa na kudai Jambo hilo sio la kweli kwakuwa hakuna mwanamke hata mmmoja anayependa kupigwa wala kuachishwa shule bali ni mtizamo wa kinadharia ambao hauna maana yoyote.

Naye Katibu Mkuu Idara Kuu Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akitoa maelezo mafupi katika mdahalo huo amesema ni muhimu kwa jamii kuenzi na kutunza mila na desturi lakini kuna mila na desturi zenye madhara ambazo zinaleta mahumivu ya mwili na kisaikolojia.

Mdahalo huo unaendelea kuelekea maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Mtoto wa Kike kwa mwaka 2018 ambayo yatafanyika Mkoani Dar es Salaam na kilele cha maadhimisho hayo ufanyika kila mwaka tarehe 11/10 kufuatia agizo la Umoja wa Mataifa la mwezi Desemba mwaka 2011 ni kuzitaka nchi Wanachama wa Umoja huo kuadhimisha siku hii ili kuwalinda watoto wa kike dhidi ya ukatili.

No comments: