Advertisements

Friday, November 16, 2018

HOTUBA YA WAZIRI MKUU MAJALIWA WAKATI AKIAHIRISHA MKUTANO WA 13 WA BUNGE

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akisoma hotuba ya kuahirisha Mkutano wa Kumi na Tatu wa Bunge jijini Dodoma, Novemba 16, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)

UTANGULIZI
       Mheshimiwa Spika, awali ya yote, namshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa rehema kwa kutujalia uzima na afya njema na kutufikisha siku ya leo tunapohitimisha Mkutano wa 13 wa Bunge lako tukufu tuliouanza siku ya Jumanne tarehe 6 Novemba, 2018.

     Mheshimiwa Spika, ninakushukuru sana na kukupongeza kwa kuendelea kuliongoza Bunge hili Tukufu kwa umahiri mkubwa. Niwashukuru pia Mheshimiwa Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wa Bunge kwa kuendelea kukusaidia katika kutekeleza ipasavyo majukumu ya kuliongoza Bunge lako Tukufu.
      Mheshimiwa Spika, vilevile, niwapongeze Waheshimiwa Wabunge wenzangu kwa kukamilisha shughuli zote zilizopangwa kutekelezwa kwenye Mkutano huu, na kutoa michango mingi mizuri kupitia mijadala ya hoja mbalimbali zilizowasilishwa na Serikali. Nitumie fursa hii kuwahakikishia kuwa, Serikali imepokea michango yenu yenye nia ya kujenga na kuimarisha utendaji wa Serikali na tutaifanyia kazi.

Salamu za Pole

     Mheshimiwa Spika, tarehe 20 Septemba 2018, Taifa lilipokea kwa mshtuko mkubwa taarifa za kuhuzunisha za kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere. Ajali hiyo mbaya iligharimu maisha ya Watanzania wapatao 227.  Aidha, katika kipindi cha Septemba hadi Novemba 2018, wapo Watanzania wenzetu waliopatwa na maafa mbalimbali ikiwemo ajali za barabarani ambazo zimegharimu maisha, kusababisha majeruhi na uharibifu mkubwa wa mali.

    Mheshimiwa Spika, vilevile, mvua iliyoambatana na upepo mkali pamoja na radi iliyonyesha mkoani Geita tarehe 17 Oktoba 2018 ilisababisha vifo vya wanafunzi sita na walimu wawili wa Shule ya Msingi Emaco na kujeruhi wengine 25. Hivyo, nitumie fursa hii kutuma salamu zangu za pole kwa wale wote waliopoteza wapendwa wao Mungu aweke roho zao mahali pema peponi, Amina. Tuendelee kuwaombea uponaji wa haraka kwa waliopata majeraha kwenye ajali mbalimbali. Mwenyezi Mungu azilaze roho za marehemu mahala pema peponi. Amina!


Pongezi

     Mheshimiwa Spika, kama unavyofahamu Wabunge wanne walishinda chaguzi ndogo zilizoendeshwa katika majimbo ya Monduli, Ukonga, Korogwe Vijijini na Liwale. Wabunge hao ni Mheshimiwa Julius Kalanga Laizer (Mb.), Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara (Mb.), Mheshimiwa Timotheo Paul Mnzava (Mb.) na Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka (Mb.). Hongereni sana Waheshimiwa Wabunge kwa heshima kubwa mliyoipata ya kuaminiwa na wananchi wa majimbo yenu. Nitumie nafasi hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wanne walioapishwa jana tarehe 15 Novemba, 2018 ambao ni Mheshimiwa James Kinyasi Millya (Mb.), Simanjiro; Mheshimiwa Joseph Michael Mkundi (Mb.), Ukerewe; Mheshimiwa Ryoba Chacha Marwa (Mb.), Serengeti na Mheshimiwa Paulina Philip Gekul (Mb.), Babati kwa kupita bila kupingwa kwenye majimbo yao.

      Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wapya kwa kuaminiwa na kuteuliwa kushika nyadhifa mbalimbali  ambao ni Mheshimiwa Joseph George Kakunda (Mb.), Waziri wa Viwanda Biashara na Uwekezaji; Mheshimiwa Japhet Ngailonga Hasunga (Mb.), Waziri wa Kilimo; Mheshimiwa Mary Machuche Mwanjelwa, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora; Mheshimiwa Constantine John Kanyasu (Mb.), Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii; Mheshimiwa Mwita Mwikwabe Waitara (Mb.), Naibu Waziri Ofisi ya Rais - TAMISEMI na Mheshimiwa Innocent Lugha Bashungwa (Mb.), Naibu Waziri wa Kilimo.

        Mheshimiwa Spika, niwakumbushe Waheshimiwa Mawaziri na Naibu Mawaziri wote kuwa Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na wananchi wana matarajio makubwa kutoka kwenu katika kuwaletea maendeleo.  Hivyo, nawaomba tusiwaangushe.

HALI YA USALAMA WA VYOMBO VYA USAFIRI

           Mheshimiwa Spika, wakati naanza kusoma hotuba yangu nimetoa salamu za pole kutokana na ajali mbalimbali zilizohusisha vyombo vya usafiri. Ajali hizo ambazo zimegharimu maisha ya wananchi wengi ni pamoja na kuzama kwa kivuko cha MV Nyerere.

      Mheshimiwa Spika, kufuatia ajali hiyo Serikali iliunda Tume ya kuchunguza chanzo cha ajali na kutoa mapendekezo yatakayosaidia kuepusha ajali nyingine ya aina hiyo na kubainisha vyanzo vya ajali na watendaji ambao hawakutekeleza wajibu wao ipasavyo. Tayari Serikali imepokea taarifa ya tume hiyo na inaifanyia kazi.

      Mheshimiwa Spika, hali ya usalama barabarani bado ina changamoto nyingi licha ya takwimu kuonesha kupungua kwa matukio na vifo vinavyosababishwa na ajali hizo. Mathalan, katika mwaka 2016 matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 9,856 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika mwaka 2017 ambayo ni pungufu kwa matukio 4,278 sawa na asilimia 43.

        Mheshimiwa Spika, vilevile, katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Oktoba 2018, matukio ya ajali za barabarani yalikuwa 3,209 ikilinganishwa na matukio 5,578 katika kipindi cha kuanzia Januari hadi Desemba 2017.

      Mheshimiwa Spika, Serikali inachukua hatua mbalimbali kukabiliana na matukio ya usalama barabarani. Miongoni mwa hatua hizo ni kuendesha operesheni za kuhakikisha sheria zote za usalama barabarani zinafuatwa kikamilifu.

ELIMU

     Mheshimiwa Spika; katika kuimarisha usimamizi na uendeshaji wa shule nchini, Serikali inapeleka fedha za elimumsingi bila malipo moja kwa moja shuleni. Kwa mfano, katika kipindi cha Julai hadi Oktoba, 2018 shilingi bilioni 38.6 zilipelekwa katika shule za msingi na shilingi bilioni 44.6 kwa shule za sekondari.

     Mheshimiwa Spika, tangu kuanza kutekelezwa kwa mpango wa elimumsingi bila malipo, uandikishaji wa watoto wa darasa la awali na darasa la kwanza umeimarika. Vilevile, kumekuwepo na mwenendo mzuri wa ufaulu katika mitihani ya kumaliza darasa la saba, ambapo mwaka 2016 ilikuwa wastani wa asilimia 70 na mwaka 2018 ilikuwa ni wastani wa asilimia 78. Hali hiyo, imeongeza mahitaji mbalimbali, ikiwemo miundombinu katika shule zetu za msingi na sekondari.

     Mheshimiwa Spika, katika kukabiliana na hali hiyo, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa elimu inaendelea na mikakati ya ujenzi na ukamilishaji wa miundombinu muhimu ya shule.

Kwa mfano, kupitia programu ya Lipa Kulingana na Matokeo katika Elimu (EP4R), shilingi bilioni 53.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya shule za msingi na sekondari. Aidha, shilingi bilioni 9.2 zimeelekezwa kuimarisha miundombinu ya elimu kupitia programu ya kuboresha elimu ya shule za msingi (EQUIP-T).

      Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu na kuweka mazingira mazuri katika mfumo mzima wa elimu nchini kwa kushirikiana na wadau wote.

      Mheshimiwa Spika, natambua kuwa mitihani ya Taifa kwa darasa la nne, kidato cha pili na kidato cha nne inaendelea. Hata hivyo, katika kipindi cha hivi karibuni kumezuka matukio ya kuvuja kwa mitihani. Naziagiza taasisi zote zinazohusika na usimamizi na uendeshaji wa mitihani ya Taifa kuhakikisha wanasimamia kikamilifu mitihani hiyo ili kuepuka udanganyifu. Itakapobainika kuwepo kwa udanganyifu wa mitihani, hatua stahiki zichukuliwe kwa mujibu wa sheria dhidi ya yeyote atakayehusika.

UHARIBIFU WA MAZINGIRA NA VYANZO VYA MAJI

       Mheshimiwa Spika, nchi yetu inakabiliwa na changamoto kubwa ya uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Kwa msingi huo, hatuna budi kuchukua hatua stahiki ili kudhibiti hali hiyo isiendelee. Mfano, miradi mingi ya maji nchini imekwama au kutoleta tija kutokana na uharibifu wa mazingira na vyanzo vya maji. Hivyo, niwasihi Waheshimiwa Wabunge wenzangu wahamasishe wananchi na wadau kutoa maoni yatakayosaidia kujenga na kuboresha vema sheria zinazokusudiwa kulinda mazingira yetu pamoja na vyanzo vya maji. Wakati wote, Serikali ipo tayari kusikiliza maoni ya wananchi na Waheshimiwa Wabunge.

        Mheshimiwa Spika, katika ziara yangu ya hivi karibuni wilayani Lushoto, nilifarijika mno kuona jitihada kubwa zinazofanywa na wananchi wa wilaya hiyo katika kuhifadhi mazingira. Nitumie fursa hii kuwapongeza wananchi wa Halmashauri za Wilaya ya Lushoto na Bumbuli kwa utunzaji mzuri wa mazingira. Naziagiza Halmashauri nyingine nchini ziige mfano huo mzuri wa kuhifadhi mazingira.

MWENENDO WA UNUNUZI WA MAZAO NCHINI

        Mheshimiwa Spika, kumejitokeza hali ya kuyumba kwa bei kwa baadhi ya mazao yetu ya kimkakati, yaani kahawa, tumbaku, pamba na korosho. Hali hiyo, imesababishwa na kuyumba kwa bei za mazao hayo katika soko la dunia. Aidha, pale ambapo bei za mazao zinakuwa nzuri tutakuwa tunatoa taarifa kwa wakulima wanaolima zao husika.

       Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa maelekezo yake mahsusi kuhusu namna bora ya uendeshaji wa biashara za mazao nchini. Kufuatia maelekezo hayo, sasa sekta binafsi hasa wafanyabiashara wanapaswa kuzingatia maslahi mapana ya wakulima na Taifa kwa ujumla.

      Mheshimiwa Spika, vilevile, Mheshimiwa Rais ametoa maelekezo kwa taasisi zote za umma zinazohusika na masoko ya mazao, kama vile TanTrade, Bodi ya Mazao Mchanganyiko na Kampuni ya Soko la Bidhaa Tanzania (Tanzania Mercantile Exchange -TMX) kutafuta masoko mapya ya mazao yetu badala ya kutegemea wafanyabiashara pekee ambao baadhi yao si waadilifu.

Tunampongeza Mheshimiwa Rais kwa maamuzi yake ya kuokoa wakulima wa korosho kukosa masoko ya uhakika. Korosho hizo sasa zinanunuliwa kwa bei ya shilingi 3,300 na tayari malipo yameanza kulipwa.

     Mheshimiwa Spika, niwaombe wananchi wenzangu kuendelea kutoa ushirikiano na kutambua kuwa, dhamira ya Serikali ni kuona kila mkulima ananufaika sambamba na kupata tija ya mazao anayozalisha.

MAONESHO YA VIWANDA NA TEKNOLOJIA YA MADINI

    Mheshimiwa Spika, tarehe 4 Novemba, 2018 nilipata fursa ya kufunga Maonesho ya Viwanda ya Mkoa wa Pwani ambayo yalifunguliwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tarehe 29 Oktoba 2018.Aidha, tarehe 23 Oktoba, 2018 nilifungua maonesho mengine ya viwanda vidogo na biashara ndogondogo yaliyofanyika katika viwanja vya Nyakabindi, wilayani Bariadi, Mkoa wa Simiyu.

       Mheshimiwa Spika, sambamba na maonesho yaliyofanyika mkoani Simiyu na Pwani, tarehe 30 Septemba, 2018 nilipata pia fursa ya kufunga maonesho ya teknolojia na uwekezaji katika sekta ya madini ya dhahabu yaliyofanyika katika Mkoa wa Geita.

     Mheshimiwa Spika, maonesho hayo yalikuwa na lengo la kuwakutanisha wadau mbalimbali wa sekta ya madini na kutangaza fursa za kiuchumi na uwekezaji zilizopo katika mnyororo mzima wa uchimbaji madini hususan dhahabu. Aidha, kupitia maonesho hayo wajasiriamali wa sekta ya madini hususan wachimbaji wadogo walipata fursa ya kujifunza teknolojia bora ya uchenjuaji madini ambayo ni rafiki kwa mazingira.

     Mheshimiwa Spika, wachimbaji hao wadogo, pia waliweza kukutana na wataalamu wanaosimamia sekta ya madini na mabenki kwa lengo la kujifunza matumizi ya teknolojia mpya sambamba na kufahamu taratibu mbalimbali za kupata mikopo ya kuendesha shughuli zao za uchimbaji madini.

        Mheshimiwa Spika, napenda nitumie fursa hii kuwapongeza Wakuu wa Mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita kwa ubunifu wao huo. Vilevile, niwapongeze sana wazalishaji wenye viwanda na madini pamoja na wadau wote walioshiriki kuonesha teknolojia mbalimbali na bidhaa mpya za kilimo na madini katika maonesho hayo.

       Mheshimiwa Spika, ubunifu huu wa kufanya maonesho ya viwanda ya Kimkoa, Kikanda na Kitaifa ni jambo muhimu sana. Maonesho haya, yanatupa fursa ya kutangaza na kutathmini hatua tuliyofikia katika utekelezaji wa agenda ya ujenzi wa uchumi wa viwanda na kubaini changamoto zilizopo. Vilevile, maonesho hayo yanahamasisha wananchi wengi zaidi kushiriki katika ujenzi wa uchumi wa viwanda.

       Mheshimiwa Spika, pia, maonesho hayo yanatoa fursa kwa wadau husika kukutana na kubadilishana utaalam, uzoefu na teknolojia mbalimbali mpya. Tarehe 22 Novemba, 2018 nitakuwa mkoani Tabora kuzindua Jukwaa la Fursa za Biashara na Uwekezaji.

       Mheshimiwa Spika, napenda kuielekeza mikoa mingine kuiga mifano hiyo ya Mikoa ya Pwani, Simiyu na Geita, ili kuhamasisha wananchi na wadau wengine washiriki ipasavyo katika ujenzi wa viwanda na kuleta teknolojia mpya za viwanda na sekta ya madini.

       Mheshimiwa Spika, nitumie fursa hii pia, kuwataka wananchi wajenge utamaduni wa kutumia bidhaa zetu zinazozalishwa nchini ili kulinda viwanda vyetu na kukuza uchumi.

SHUGHULI ZA BUNGE

    Mheshimiwa Spika, naomba nihitimishe kwa kuainisha kwa uchache yaliyojiri katika mkutano huu wa Bunge na mazingatio ya Serikali:-

Maswali na Majibu

       Mheshimiwa Spika, idadi ya maswali 120 ya msingi na 272 ya nyongeza yaliulizwa Bungeni kuhusu kero na utekelezaji wa miradi mbalimbali. Aidha, katika utaratibu wa maswali kwa Waziri Mkuu, niliulizwa maswali ya msingi 12 na moja la nyongeza. Hii ni ishara kuwa wabunge wana hamu ya kuona huduma na maendeleo yanawafikia wananchi kwa wakati. 

       Mheshimiwa Spika, pamoja na majibu yaliyotolewa naomba kulihakikishia Bunge lako tukufu kuwa, Serikali itaongeza kasi katika kutekeleza na kukamilisha miradi mbalimbali ya maendeleo kwa kadri hali ya uchumi itakavyoruhusu.

Hoja za Serikali

     Mheshimiwa Spika, Serikali imewasilisha mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa na Mwongozo wa Maandalizi ya Bajeti ya mwaka 2019/2020. Bunge lako tukufu, lilipata fursa ya kujadili kwa kina Mpango na Mwongozo wa Bajeti kwa muda wa siku tano. Katika siku hizo, tulipokea michango mbalimbali muhimu itakayotusaidia sana katika utendaji wa kazi zetu.

       Mheshimiwa Spika, michango hiyo pia itasaidia kuboresha mpango na bajeti ya mwaka ujao na hivyo, kuondoa changamoto za wananchi na kuakisi dhamira ya Serikali ya awamu ya tano ya kuleta maendeleo, ili kuifikisha nchi katika uchumi wa kati. Niwaombe Waheshimiwa Wabunge muendelee kuishauri Serikali kwenye sekta zote za uzalishaji, hususan kilimo, uvuvi, madini, mifugo, viwanda na utalii.

Miswada ya Serikali

     Mheshimiwa Spika, tarehe 15 Novemba, 2018 Serikali iliwasilisha Muswada wa Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha wa mwaka 2018 (The Microfinance Act, 2018) ambao umesomwa kwa hatua zake zote na kupitishwa na Bunge lako tukufu, ukisubiri kibali cha Mheshimiwa Rais ili kuwa sheria kamili.

      Mheshimiwa Spika, kwa muda mrefu sekta ndogo ya fedha haikuwa na udhibiti wa kutosha. Hali hiyo ilisababisha kuwepo uendeshaji usio rasmi wa shughuli mbalimbali za kifedha. Mathalan, taasisi zinazochukua amana, vikundi vya fedha vya jamii na wakopeshaji binafsi.

        Mheshimiwa Spika, shughuli hizo ambazo nyingi ziliendeshwa katika utaratibu usio rasmi ziliwaletea athari mbalimbali wananchi ikiwemo kupoteza mali zao zilizowekwa kama amana kwenye taasisi hizo. Aidha, baadhi ya watu wasiokuwa waaminifu wamekuwa wakitumia mwanya wa kutokuwepo udhibiti wa kutosha kwenye sekta hiyo ndogo ya fedha kuendesha vitendo mbalimbali vya kihalifu ikiwemo utakatishaji fedha.

       Mheshimiwa Spika, kutokana na sababu hizo, Serikali iliamua kutunga Sheria ya Huduma Ndogo za Fedha ya mwaka 2018 kwa lengo la kuongeza udhibiti wa sekta hiyo ndogo ya fedha na kuiwezesha kuchangia ipasavyo katika kuimarisha uchumi wa nchi yetu na kulinda mali na fedha za wananchi wetu.

      Mheshimiwa Spika, miswada mingine mitano imesomwa kwa mara ya kwanza ambayo ni:

  1. Muswada wa Marekebisho ya Sheria Mbalimbali Na. 4 wa mwaka 2018;

  1. Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Vyama vya Siasa wa mwaka 2018;

  1. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania ya mwaka 2018;

  1. Muswada wa Sheria ya Mamlaka ya Usimamizi wa Usafiri wa Nchi Kavu wa mwaka 2018; na

  1. Muswada wa Kutunga Sheria ya Maji na Usafi wa Mazingira wa mwaka 2018.

Maazimio ya Kuridhia Mikataba na Itifaki za Kimataifa

    Mheshimiwa Spika, katika Mkutano huu wa Bunge maazimio yafuatayo yaliwasilishwa na kuridhiwa na Bunge:

  1. Azimio la Kuridhia Itifaki ya Nchi za Kusini mwa Afrika kuhusu Kulinda Hatimiliki za Wagunduzi wa Aina Mpya za Mbegu za Mimea;

  1. Azimio la Kuridhia Mkataba wa Kimataifa wa Kuzuia Matumizi ya Silaha za Kibaiolojia na Sumu; na,

  1. Mapendekezo ya Kuridhia Mkataba wa Takwimu wa Afrika. Bunge limeridhia kwa kauli moja kupitisha azimio hili. Serikali inawataka Watanzania wote watumie takwimu sahihi kutoka vyanzo sahihi ili kukidhi mahitaji na kuondoa mkanganyiko kwa matumizi ya takwimu zisizokuwa sahihi.

HITIMISHO 

       Mheshimiwa Spika, naomba nitumie nafasi hii kwenu Waheshimiwa Wabunge na Watanzania wote kuwatakia heri, maandalizi mema na ushindi timu yetu ya Taifa ya mpira wa miguu (Taifa Stars), wakati wa mchezo wake dhidi ya timu ya Taifa ya Lesotho tarehe 18 Novemba 2018 ili kuwania tiketi ya kufuzu kwa michuano ya AFCON nchini Cameroon mwaka 2019.  Safari ya kuelekea Cameroon iko nyeupeee. Sasa ni zamu yetu.

        Mheshimiwa Spika, kipekee, naomba nitumie nafasi hii kuwatakia maandalzi mema timu yetu ya Bunge Sports Club ambayo mwaka huu inaenda kucheza nchini Burundi ikiliwakilisha Bunge letu na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwenye michezo hiyo.

Ni matumaini yetu kuwa mwaka huu wa 2018, timu ya Bunge Sports Club itarudi na makombe yote. Kwa niaba ya Waheshimiwa Wabunge, tunaitakia mafanikio timu yetu mafanikio mema na mrudi mkiwa na makombe yote ili tuweze kushangilia hapa nyumbani.

      Mheshimiwa Spika, natoa shukrani za dhati kwa Katibu wa Bunge, watendaji na maafisa wengine wa Serikali kwa kuratibu na kufanikisha shughuli za mkutano huu kama zilivyopangwa.

      Mheshimiwa Spika, Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) limetangaza kuwa Maulid ya kuadhimisha mazazi ya Mtume Muhammad Swalla Allahu Alayh Wasallam kitaifa itasomwa usiku wa Jumatatu tarehe 19 Novemba 2018 Korogwe mkoani Tanga. Napenda kutumia fursa hii kuwatakia waumini wote wa dini ya Kiislamu sherehe njema za maadhimisho ya Maulid. Aidha, kwa waumini wote wa Kikristo, niwatakie sikukuu njema ya Krismasi tarehe 25 Desemba 2018. Vilevile, Mheshimiwa Spika, nawatakia Watanzania wote heri ya mwaka mpya wa 2019.

        Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja kuwa Bunge lako tukufu liahirishwe hadi siku ya Jumanne, tarehe 29 Januari 2019 saa tatu asubuhi.

       Mheshimiwa Spika, naomba kutoa hoja.

No comments: