Dar es Salaam. Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad amedai mkataba wa utiaji saini wa mgawanyo wa uzalishaji wa mafuta na gesi asilia baina Zanzibar na Ras- Alkhaima umekiuka katiba, sheria za nchi hiyo na haukufuta utaratibu unaotakiwa.
Pia, Maalim Seif amedai mkataba umesainiwa katika mazingira yaliyokosa umakini na utasababisha vizazi vijavyo kuingia kwenye janga kubwa la kutofaidika na rasirimali hiyo endapo itapatikana.
Lakini Oktoba 23, 2018 wakati hafla ya utiaji saini mkataba huo Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohammed Shein alisema mchakato huo umezingatia sheria zote za Zanzibar na si vinginevyo.
Maalim Seif ametoa kauli hiyo, leo Jumapili Novemba 11,2018 wakati akizungumza na wanahabari na kusema suala la utafutaji wa mafuta na gesi lina historia ndefu na kilichofanyika Oktoba 23 si kipya.
"Mwaka 2010 kampuni hiyo ilinunua hisa za leseni ya kampuni ya Antrim kuhusu kitalu cha Zanzibar na Pemba na kurithi mkataba wa mgawanyo wa faida kutoka Antrim.”
"Hii si mara ya kwanza ya kitalu hicho kufanyiwa marekebisho sawa na yaliyotiliwa saini Oktoba 23. Makubaliano hayo yalishaingiwa miaka 22 kilichobadilika ni tarehe na watiaji saini na katarasi za makubaliano," amesema Maalim Seif.
Maalim Seif ambaye aliwahi kuwa makamu wa kwanza wa Rais Zanzibar amesema mwaka 2016 Baraza la Wawakilishi Zanzibar lilipitisha Sheria ya Mafuta ya Zanzibar ambayo kimaudhui haina na tofauti na Sheria ya Mafuta ya Bunge mwaka 2015.
Amesema mkataba huo uliosainiwa Oktoba 23 ulitokana na kile kilichoitwa Mamlaka ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ), chini ya Sheria ya Mafuta ya Zanzibar.
Amefafanua kutokana na hali hiyo Serikali ya Zanzibar imetia saini makubaliano hayo kinyume na Katiba ya Jamhuri ya Muungano na azimio la Baraza la Wawakilishi na kinyume cha msimamo wa Wazanzibar na viongozi waliotangulia.
No comments:
Post a Comment