ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, November 11, 2018

JPM awafukuza Tizeba, Mwijage

By Ibrahim Yamola na Julius Mnganga, Mwananchi Mwananchipapers@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Saa chache baada ya Rais John Magufuli kuliagiza Jeshi la Ulinzi la Wananchi la Tanzania (JWTZ), kujiandaa kwenda kusomba korosho katika mikoa ya Lindi na Mtwara, kiongozi huyo amewafukuza mawaziri wawili.

Mawaziri waliofukuzwa kwenye baraza lake la mawaziri ni Dk Charles Tizeba wa Kilimo na Charles Mwijage wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji.

Dk Tizeba ambaye ni mbunge wa Buchosha amefukuzwa kazi akiwa mkoani Kilimanjaro na jana asubuhi alionekana Moshi Mjini katika ofisi za Bodi ya Kahawa Tanzania.

Mbali na kuwafukuza kazi mawaziri hao na kuteua wengine, Rais Magufuli ameivunja Bodi ya Korosho Tanzania (TCB) na kutengua uteuzi wa mwenyekiti wake, Anna Abdallah.

Rais Magufuli alitangaza mabadiliko hayo saa chache baada ya kutoka kukagua magari katika Kambi ya Jeshi ya Twalipo, Kikosi cha Usafirishaji cha 95KJ Mgulani, Temeke jijini Dar es Salaam nikiwa ni maandalizi ya kubeba korosho endapo wanunuzi binafsi hawatatii maagizo ya Serikali kuandika barua kama watanunua zao hilo au la ifikapo kesho, saa 10:00 jioni.

Hatua ya Rais imekuja siku moja baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kuwapa siku nne wanunuzi hao (kuanzia Ijumaa hadi kesho saa 10 jioni) wawe wamepeleka barua za maelezo ofisini kwake wakibainisha wanataka kununua kiasi gani na lini.

Majaliwa alitoa agizo hilo wiki moja baada ya Serikali kuruhusu kuendelea kwa minada ya korosho kuanzia Novemba Mosi baada ya kusimamishwa kwa wiki moja, Oktoba 26 kutokana na wakulima kugoma kuuza korosho zao kutokana na bei ndogo ambayo ilitolewa na wanunuzi hao ya kati ya Sh1,900 hadi Sh2,700 kwa kilo.

Mgomo wa wakulima ulimalizika baada ya Serikali kuagiza wanunuzi hao kununua korosho kwa Sh3,000 lakini hata hivyo, uliibuka mgomo mwingine wa wanunuzi.

Kudhihirisha mgomo wa wanunuzi, Rais alisema kati ya kampuni 37 zilizopewa kibali ni 14 tu ndizo zilikuwa zinajitokeza kwenye minada ingawa zilinunua kwa kusuasua.

“Nimeambiwa kuna takriban tani 210,000 za korosho mwaka huu na kule Lindi na Mtwara kuna maghala yanayoweza kuhifadhi tani 77,000 hapa Dar es Salaam zaidi ya tani 90,000. Nimefurahi kwamba jeshi letu lipo tayari kufanya operesheni hii,” alisema Rais Magufuli.

Alisema ikiwa hawatajitokeza hadi kesho jioni, Serikali itatumia JWTZ na Bodi ya Mazao Mchanganyiko kununua korosho zote za wakulima na hakuna mnunuzi atakayeruhusiwa tena.

Rais Magufuli alisema baaada ya kuzinunua, Serikali itatafuta soko na nyingine zitabanguliwa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

“Nataka kuwahakikishia wakulima wa korosho, Serikali ipo na itaendelea kuwapigania, ikifika Jumatatu saa 10:00 jioni, hawa wanunuzi binafsi hawajajitokeza na kueleza watanunua tani ngapi, Serikali itanunua korosho zote na fedha za kununulia zipo” alisema.

“Kutokana na jambo hili, sasa JWTZ kupitia Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ianze kufikiria kuanzisha kiwanda kikubwa cha kubangua korosho, hata kama itabidi Serikali kutoa fedha za kujenga kiwanda hicho.”

Rais alisema umefika wakati wa kuachana na uuzaji wa korosho ghafi kwani: “Huo ni utumwa, tuwe na viwanda vyetu na vijana wetu wapate ajira.”

Akitoa taarifa ya maandalizi, Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo alisema licha ya magari 75 yaliyopo, tani nyingine 500 zitabebwa na meli ya kijeshi (Landing Craft) ambayo inaweza kutia nanga mahali popote katika ufukwe wa bahari.

“Tupo tayari kutekeleza jukumu hili,” alisema Jenerali Mabeyo.

Akitoa maoni yake baada ya uamuzi huo wa Serikali kununua korosho, Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT Wazalendo), Zitto Kabwe aliishauri kufuata sheria katika kufanikisha ununuzi huo.

“Serikali itahitaji zaidi ya Sh600 bilioni kuwalipa wakulima. Fedha hizi zinahitaji idhini ya Bunge kwa kufanya marekebisho ya bajeti ya mwaka 2018/19. Rais akitaka kulifanya hili bila kufuata sheria tutampinga. Serikali izingatie hilo kwenye kutafuta jawabu la korosho,” ameandika Zito kwenye ukurasa wake wa Twitter.

Mawaziri kutimuliwa

Jana saa moja usiku, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, Gerson Msigwa alitoa taarifa ikitangaza mabadiliko hayo ya baraza la mawaziri.

Katika mabadiliko hayo, Rais Magufuli alimteua naibu waziri wa Maliasili na Utalii, Japhet Hasunga kuwa waziri wa Kilimo.

Nafasi ya Mwijage ambaye ni mbunge wa Muleba Kaskazini (CCM) imejazwa na Joseph Kakunda aliyekuwa naibu waziri, ofisi ya Rais, (Tamisemi).

Katika mabadiliko hayo, mbunge wa Geita Mjini (CCM), Constantine Kanyasu ameteuliwa kuwa naibu waziri wa Maliasili na Utalii kuchukua nafsi ya Hasunga.

Mary Mwanjelwa amehamishwa kutoka wizara ya Kilimo na sasa anakuwa naibu waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Katika uteuzi huo, mbunge wa Ukonga, Mwita Waitara ameteuliwa kuwa Naibu Waziri wa Tamisemi kuchukua nafasi ya iliyoachwa na Kakunda.

Waitara aliapishwa Jumanne iliyopita kuwa mbunge kwa mara ya pili ndani ya miaka mitatu baada ya kujiuzulu ubunge akiwa Chadema na kuhamia CCM alikopitishwa tena kugombea ubunge.

Mbunge wa Karagwe (CCM), Innocent Bashungwa ameteuliwa kuwa naibu waziri wa Kilimo, akichukua nafasi ya Mwanjelwa.

No comments: