Advertisements

Wednesday, November 14, 2018

‘MWANZA NYEGEZI’ KUFUNGIWA, RAYVANNY AWANDIKIA WARAKA KWA BASATA

IKIWA ni takribani saa 24 baada ya wimbo mpya wa Msanii wa WCB, Raymond Shaban Mwakyusa maarufu Rayvanny aliyomshirikisha Diamond Platinumz uitwao Mwanza kufungiwa na Baraza la Sanaa Tanzania (BASATA) na kumtaka auondoe mitandaoni, msanii huyo amefunguka na kuonyesha kutoridhika kwake na uamuzi wa Baraza hilo kuufungia wimbo wake.

Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Rayvanny amesema wimbo huo ulilenga kupeleka maudhui kwa vijana kuachana na tabia chafu ikiwemo kuvaa mavazi ya kujisitili, kutokufanya matendo yaliyo kinyume na maadili kama mapenzi kinyume na maumbile na kusambaza picha chafu mitandaoni kwani wataishia sentro kama msanii Amber Rutty.

Aidha, Rayvanny amesema walilenga kupeleka ujumbe huo kwa vijana zaidi ya umri wa miaka 18 na kwamba ilikuwa ni sehemu ya kuwafariji watu wa Mwanza waliyokumbwa na tukio la ajali ya MV Nyerere. Hivyo ili kuwafariji ilibidi wimbo huo uchanganywe na radha ya burudani ili kufikisha ujumbe.

Rayvanny ameandika;

HABARI za asubuhi ndugu zangu, taarifa za kufungiwa kwa wimbo wangu nimezipata, lakini katika hili nina haya machache yakusema.

Sanaa ni nini?

Sanaa ni neno lililotokana na lugha ya kiarabu, lenye maana ya ufundi anaoutumia mwanadamu, kuwasilisha fikra au mawazo yaliyo ndani ya fikra zake, vile vile sanaa ni uzuri unaojiibua katika umbo lililosanifiwa, usanifu ni kuumba/kufanya kitu kwa kutumia ustadi ili kiweze kuvutia watu kwa uzuri wake.

Hivyo kazi yoyote ya sanaa inategemea ionyeshe ufundi wa hali ya juu, ili iwe na mvuto kwa hadhira yake iliokusudiwa, hayo maneno si yangu mimi, ni tafsiri ya neno sanaa.

2. Dhamira ya wimbo


Dhamira yetu haikua kutukana, kama inavyoonekana sasa, dhamira yetu ilikua kutoa burudani kwa hadhira iliokusudiwa ambao ni vijana wenzetu, lakini pia na mafundiosho ambayo kila siku Serikali imekua ikiyapiga vita.

Suala kama la Amber Rutty.

Katika wimbo wetu tumesema (nami naogopa sentro, michezo ya Amber Rutty, kwamba kijana yoyote anaesikiliza aogope kitendo hicho ataishia pabaya. Pia kuna mistari inasema (hapendagi mpasuo, hataki shida basata) ukiwa na maana ya kukataza mavazi mabaya, mavazi ya wazi nakusisitizia kwamba hata basata hayaruhusiwi. Ukiangalia haya yote ni mafundisho ambayo mwanasanaa lazima uyafikishe katika ligha iliosanifiwa.

3. Kwa nini Mwanza?


Tungeweza kuuita huu wimbo jina lingine lolote, Mbeya, Kigoma au mkoa wowote tofauti lakini kwanini Mwanza? Ikumbukwe siku chache zilizopita kumetokea maafa makubwa yaliyowakuta ndugu zetu wa Mwanza. Watu wamepoteza ndugu jamaa na marafiki.

Kama wasanii tuliwaza sana hususani kwa vijana wenzetu wa Mwanza tuwafanyie kitu gani ikiwa ni sehemu ya faraja kwao. Ndipo lilipokuja wazo la kutengeneza wimbo kwa ajili ya Mwanza. Unaosema kwetu Mwanza Nyegezi lakini tukasema usiende hivyo tu uwe na mafundisho ndani yake lakini pia burudani kwa vijana wa Mwanza na maeneo mengine. Na kiukweli wimbo huu umepokelewa vizuri sana Mwanza na maeneo mbalimbali ikiwa ni ishara ya ile dhamira tulio ikusudia imefanya kazi.

Kufungiwa

Kuna vyombo vya habari, na sehemu mbali mbali miziki yetu inaposikika yawezekana kukawa na watoto pengine wimbo huu haikua ni hadhira tulioikusudia. Hivyo ukisikika kwao ikawa ni kinyume na maadili kwa sababu hadhira tulioikusudia ni ya watu wazima yani miaka 18 na kuendelea.

Ambao tunaamini ndiyo wapo kwenye mitandao ya kijamii, ndiyo wanunuzi wa kazi zetu, na ndiyo wahudhuriaji wa matamasha yetu.

2 Maoni yangu

Nilikua naona suala la kufungia wimbo huu kwa vijana wenzetu ni kutunyima kufikisha ujumbe, burudani kwa hadhira yetu ya sanaa. Mfano, mitandao ya kijamii, hakuna mtoto atakyeingia katika mitandao, lakini pia kwenye matamasha kama Wasafi Festival pale wanaokuja ni watu wazima, ambao wimbo huu hauna madhara kwao.

Kwenye TV na redio naweza kusema ni sawa kutokana na watoto watakao tazama wimbo huu ila mitandao ya kijamii na kwenye matamasha naomba Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) mkiwa kama walezi wa sanaa mulitazame hili na kuona mnatusaidiaje. Sanaa ni kazi / sanaa ni ajira lakini pia sanaa ni ubunifu asante

Hata hivyo, Basata wamewaita Diamond na Rayvanny kwenye ofisi za Baraza hilo leo Jumanne, Novemba 13, 2018

GPL

No comments: