ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, November 28, 2018

ZAIDI YA SH. BILIONI TATU ZAPOTEA WILAYANI NYANGW’ALE

 Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akihutubia Mkutano wa hadhara kwenye kiwanja cha Sabasaba kilichopo Karumwa wilayani Nyang'hwale, Novemba 28, 2018. (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu)
  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akiwasalimia wananchi wakati alipowasili kwenye Kiwanja cha Sabasaba  kilichopo Karumwa wilayani Nyang'hwale kuhutubia mkutano wa hadhara, Novemba 28, 2018.  
 Baadhi ya wananchi wa wilaya ya Nyang'hwale mkoani Geita wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipohutubia Mkutano wa hadhara katika kiwanja cha Sabasaba  kilichopo Karumwa, Novemba 28, 2018.

*Waziri Mkuu aagiza kuchukuliwa hatua kwa watumishi wote waliohusika
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameagiza watumishi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Nyangw’ale waliohusika na ubadhilifu wa zaidi ya sh. bilioni tatu fedha ambazo zilitolewa na Serikali kugharamia miradi ya maendeleo wachukuliwe hatua.
Pia ameagiza kukamatwa na kuchukuliwa hatua kwa Mkaguzi wa Ndani wa halmashauri hiyo, Gavana Matesa kwa sababu ameshindwa kutoa kwa mamlaka husika kuhusu taarifa za wizi wa fedha za maendeleo zilizotafunwa.
Waziri Mkuu ametoa maagizo hayo leo (Jumatano, Novemba 28, 2018) wakati akizungumza na watumishi wa halmashauri ya wilaya ya Nyangw’ale akiwa katika ziara yake ya kikazi ya siku nne mkoani Geita.
Miongoni mwa miradi ambayo fedha zake zimepotea ni pamoja na sh. bilioni 1.2 za ujenzi ofisi ya halmashauri hiyo, sh. milioni 400 za ukarabati wa kituo cha afya Nyangw’ale, sh. milioni 611.230 za miradi ya maji.
Nyingine ni sh. milioni 536.119 za mpango wa malipo kulingana na huduma (EP4R), sh. milioni 125.914 za ushuru wa huduma, sh. milioni 31 za ujenzi wa ofisi ya mbunge na sh. milioni 109 za mfuko wa barabara.
“Wilaya ya Nyangw’ale ni mpya na Serikali imekuwa ikileta fedha nyingi lakini fedha zote zimetafunwa, Serikali ipo makini sana na moja kati ya vita kubwa ni dhidi ya mafisadi, wala rushwa ambayo ni endelevu hivyo tutashughulika na kila mmoja.
Tayari watu saba akiwemo aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya wilaya ya Nyangw’ale, Carlos Gwamagobe na wenzake wamekamatwa. Wizi unatisha Nyangw’ale wilaya inatia aibu tutawaondoa watu wote waliohusika na tutaendelea kuwakamata.”
Hata hivyo Waziri Mkuu amewahakikishia wananchi wa wilaya hiyo kwamba Serikali itahakikisha miradi yote iliyoahidiwa kujengwa kwenye wilaya hiyo ikiwemo ya maji itatekelezwa kama ilivyopangwa, waendelee kuwa na imani na Serikali yao.
Kuhusua suala la watumishi, amesema wilaya hiyo lazima iwe na watumishi wasafi wenye weledi wa kufanya kazi na lazima wahakikishe fedha za miradi zinazotolewa katika halmashauri hiyo zinalingana na thamani halisi ya mradi.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Robert Gabriel amesema atahakikisha watumishi wote wa umma waliohusika na wizi huo wanachukuliwa hatua stahili na kwamba tayari baadhi yao wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola. 
Amesema halmashauri ya wilaya ya Nyangw’ale inaongoza kwa matumizi mabaya ya fedha za maendeleo kwa kuwa awali lilikuwa chaka kubwa la wizi, ambapo amesema ni bora watumishi wote wasiokuwa waadifu waondolewe na waletwe wengine.
Mkuu huyo wa Mkoa wa Geita, Mhandisi Gabriel amesema tayari baadhi ya watumishi wanaotuhumiwa kuhusika katika ubadhilifu wa fedha za miradi mbalimbali wameshakabidhiwa kwa vyombo vya dola huku watumishi wengine wakiendelea kuchunguzwa.”Watumishi wote waliohusika na wizi huu watapata tabu sana”

No comments: