Advertisements

Friday, December 7, 2018

NEC YATANGAZA KUFANYIKA KWA UCHAGUZI MDOGO JIMBO LA TEMEKE NA KATA 46 ZA TANZANIA BARA.

Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (R), SemistoclesKaijage akitoa taarifa kwa umma kuhusu Uchaguzi Mdogo wa Ubunge jimbo la Temeke na Udiwani katika kata 46 za Tanzania Bara.

Tume ya Taifa ya Uchaguzi  (NEC) imetangaza kufanyika kwa uchaguzi mdogo katika Jimbo la Temeke, Mkoani Dar es Salaam na kwenye Kata 46 za Tanzania Bara.
Akitangaza kufanyika kwa uchaguzi huo Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji (Rufaa), Semistocles Kaijage amesema kuwa uchaguzi huo utafanyika Januari 19 mwaka 2019 na fomu za uteuzi wa wagombea zitatolewa kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 20 Desemba 2018.

"Uteuzi wa Wagombea utafanyika tarehe 20 Desemba, mwaka huu. Kampeni za Uchaguzi zitafanyika kati ya tarehe 21 Desemba, hadi tarehe 18 Januari, mwaka 2019 na siku ya uchaguzi itakuwa ni tarehe 19 Januari mwaka 2019,” amesema Jaji Kaijage.

Jaji Kaijage amebainisha kuwa Tume imetangaza uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge kwenye Jimbo la Temeke baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,  Mhe. Job Ndugai juu ya uwepo wa nafasi wazi ya Ubunge katika jimbo hilo.


Amesema kuwa Tume ilipokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambaye kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343, aliitarifu Tume uwepo wa nafasi wazi ya Mbunge wa Jimbo la Temeke katika Halmashauri ya Wilaya ya Temeke Mkoani Dar es Salaam kufuatia Kujiuzulu uanachama wa Chama Wananchi CUF kwa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo hilo Mhe. Maulid Said Abdllha Mtolea.

Kwa upande wa nafasi wazi za Udiwani Jaji Kaijage  amesema kuwa Tume ilipokea taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali ya Mtaa akiitaarifu  Tume juu ya uwepo wa nafasi wazi za Udiwani katika Kata 46.

“Tume imepokea Taarifa kutoka kwa Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaaa mbaye kwa kutumia mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 13(1) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura ya 292, aliitarifu Tume uwepo wa nafasi wazi za Madiwani katika Kata 46 za Tanzania Bara,” amesisitiza Jaji Kaijage.

Ametoa wito kwa vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia Sheria, Kanuni, Maadili ya Uchaguzi, Taratibu, Miongozo na maelekezo yote yatakayotolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi wakati wa kipindi cha Uchaguzi mdogo.

Jaji Kaijage amefafanua kuwa kuwa uchaguzi huo mdogo utafanyika ndani ya Halmashauri 28 zilizopo kwenye Mikoa 14 ya Tanzania Bara.

Halamashauri na Kata zitakazokuwa na Uchaguzi ni pamoja na Ngorongoro (Sale,Misigyo,Malambo, Orgosorok na Olorien/Magaiduru), Arusha(Kimnyak), Kilwa (Kiranje ranje, Kikole, Pande Mikoana), Liwale (Kata Kichonda na Mlembwe), Babati(Dareda na Magara, Kiteto(Makame), Simanjiro(Loiborsiret, Ruvu Remit, Naberera), Kwimba(Walla), Sengerema(Nyampulukano), Ulanga(Msogezi), Mvomero(Mtibwa, Tchenzema, Mangae), Kilosa(Magomeni), Temeke(Keko), Kinondoni(Magomeni).


Halmashauri nyingine ni pamoja na Kasulu (kata ya Kitanga), Kasulu Mji( Kata za Kigondo na Msambara), Buhigwe(Mnyegera), Bukoba(Buhendagabo, Nyakato, Kikomelo), Misenyi(Kanyigo), Ngara(Nyamiaga), Mbinga(Utiri), Songea(Mpitimbi), Mbozi(Ilolo, Hasanga, Ihanda), Tandahimba(Nahyanga, Namikupa), Dodoma(Dodoma Makulu), Serengeti(Geitasamo), Bariadi(Nkundwabiye) na Bariadi Mji(Nyangokolwa).

No comments: