Advertisements

Thursday, December 6, 2018

UPATIKANAJI WA NAKALA ZA HUKUMU NA NYARAKA NYINGINE ZA MAHAKAMA WABORESHWA ZAIDI

 Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga (katikati) akitia saini Mkataba wa utoaji huduma ya Posta mlangoni (The post at your door step), anayeshuhudia kulia ni Msajili Mkuu- Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati aliyeketi kushoto ni Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe, wanaoshuhudia (waliosimama) ni baadhi ya Viongozi/Maafisa kutoka Mahakama na Shirika la Posta.
Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe akitia saini Mkataba huo.
Makabidhiano ya Mikataba hiyo mara baada ya kuhitimisha zoezi la utiaji saini. Kulia ni Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Bw. Hussein Kattanga na kushoto ni Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe.
 Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati (kulia) akiongea jambo mara baada ya utiaji saini wa Mkataba huo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)

Na Mary Gwera, Mahakama ya Tanzania
Mahakama ya Tanzania iliingia mkataba na Shirika la Posta kuhakikisha kuwa huduma ya kusambaza nyaraka mbalimbali za Mahakama inatolewa kwa nchi nzima. Mkataba huu chini ya huduma mpya ya Posta mlangoni (The post at your door step) iliyoanzishwa na Shirika la Posta, umelipa jukumu la kukusanya na kusafirisha/kusambaza nakala za hukumu na nyaraka mbalimbali za Mahakama na kuzifikisha kwa wahusika kulingana na anuani zao na mahali walipo (Anuani za makazi).

Kwa kipindi kirefu kumekuwa na malalamiko miongoni mwa wananchi/wateja wa Mahakama juu ya usumbufu katika upatikanaji wa Nakala za hukumu na baadhi ya nyaraka za Mahakama, hali ambayo kwa namna moja au nyingine ilisababishwa kwa kutokuwa na taarifa sahihi za Mdaawa/Mteja na utaratibu stahiki wa ufikishaji wa nyaraka hizo. Mahakama ya Tanzania katika utekelezaji wake wa majukumu mbalimbali inawalenga wateja wake ili kuhakikisha haki inatolewa kwa wakati na kuimarisha imani ya Wadau kwa Mahakama. Utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na mambo mengine unajumuisha utoaji wa nyaraka mbalimbali kama nakala za hukumu, wito wa kuitwa Mahakamani (Sumons).

Aidha; nyaraka muhimu zinazosambazwa kupitia huduma ya Posta Mlangoni ni Nakala za Hukumu ‘Judgment’, ‘Summons’ wito wa Mahakama, Mwenendo wa shauri/mashauri ‘Proceedings’, Maamuzi ‘Rulings’,  Amri ‘Order’, Tuzo ‘Award’/ ‘Decree’. Akizungumza kabla ya utiani saini wa mkataba huo Aprili, 2018, Mtendaji Mkuu wa Mahakama, Bw. Hussein Kattanga alisema kuwa hatua hii ni mwendelezo wa maboresho mbalimbali yanayoendelea kufanyika ili kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

Aidha; katika utiaji saini wa Mkataba huo, Mtendaji Mkuu alilitaka Shirika hilo kutekeleza makubaliano hayo kwa ufanisi, ikiwa ni pamoja na kusambaza nakala za hukumu na nyaraka nyingine kwa wahusika na kwa wakati. “Sitarajii kuona wananchi wanapanga foleni Mahakamani kutafuta hukumu zao na nyaraka nyingine, nina imani kuwa Posta mtafanya kazi ya kukusanya na kusambaza nyaraka hizo kwa wananchi ipasavyo,” alisema Mtendaji Mkuu. Akizungumza wakati ya utiaji saini Mkataba huo, Posta Masta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Bw. Hassan Mwang’ombe alimuhakikishia Mtendaji Mkuu wa Mahakama kuwa watafanya kazi hiyo kwa ufanisi mkubwa.

“Kusainiwa kwa Mkataba huu kutawezesha pia kuongeza kasi ya usambazaji wa barua za kawaida za Mahakama kuwafikia walengwa mapema zaidi kwani zitachukuliwa Mahakamani na Maofisa wa Posta na kupelekwa moja kwa moja kwa mhusika/wahusika,” alisema Bw. Mwang’ombe. Vilevile Mkuu huyo wa Shirika la Posta, alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Maofisa wa Posta hususani kwa kuandika anwani za makazi pamoja na postikodi. Naye Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati alieleza kufurahishwa kwake na kuanza rasmi kwa huduma hiyo 
kwani itasaidia kufikia ndoto ya Mahakama ya muda mrefu ya kuwafikia wananchi kwa karibu zaidi.

“Naomba kusema kuwa, nimefurahishwa sana na hatua hii, kwani ni ndoto ya Mahakama ya muda mrefu, vilevile hatua hii itarahisisha utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Jaji Mkuu ya kutoa nakala za hukumu bure kwa kuwa zitawafikia wananchi popote watakapokuwa,” alisema Mhe. Revokati.
Aidha; Mhe. Revocati alifafanua zaidi kuwa lengo hasa la Mahakama kuingia katika huduma hii ya Posta Mlangoni ni kuondoa kero ya ugumu wa upatikanaji wa nakala za hukumu Mahakamani, kero ambayo wananchi walikuwa wanakutana nayo.

Mhe.Revokati aliongeza kuwa huduma hii itatolewa katika Mahakama nchi nzima, na huduma hii inahusisha kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu na Divisheni zake, Mahakama za Hakimu Mkazi/Mkoa, Mahakama za Wilaya ambapo Mahakama za Mwanzo huwasilisha nyaraka zake katika Mahakama za Wilaya na hatimaye nyaraka hizo kuchukuliwa na Maafisa Posta kwa ajili ya usambazaji kwa Wahusika.  Akiongea katika mahojiano maalum, juu ya tathmini ya utendaji kazi wa huduma hiyo, Mhe. Revocati alisema kuwa imesaidia kuboresha huduma kwa wateja kwa sababu ilikuwa ni kero kwa wateja.

“Kwa sasa huduma hii imesaidia kupunguza kero ya upatikanaji wa nyaraka za Mahakama kwa wateja, kwani huduma inamfikia akiwa nyumbani, hali ambayo pia inasaidia kuondoa mazingira ya viashiria vya rushwa,” alifafanua Msajili Mkuu. Vilevile huduma hii imesaidia kupunguza mzigo/ msongamano wa kazi katika Masjala za Mahakama, na kuwasaidia Wateja kufungua rufaa kwa wakati. Mhe. Msajili Mkuu alitoa wito kwa wananchi kutoa ushirikiano kwa Mahakama kwa kuacha anuani au taarifa sahihi ili waweze kupelekewa nyaraka zao kwa wakati.

Akizungumza kwa niaba ya Mtendaji wa Mahakama Kuu, naye Bw. Peter Mushi alisema kuwa tangu kuanza rasmi kwa huduma hiyo Julai, 2018 jumla ya nakala 5,942 za nyaraka mbalimbali za Mahakama tayari zimeshasambazwa kwa wateja kufikia Septemba 15, 2018. Katika mahojiano maalum na Kaimu Meneja Barua, Shirika la Posta Tanzania, Bw. Josephat Gabriel alisema kuwa huduma hiyo inaendelea vizuri na kuongeza kuwa kuendelea vyema na utoaji wa huduma hiyo ni dhahiri kwao ni mafanikio makubwa.

“Zoezi hili linaenda vizuri, na napenda kuishukuru na kuipongeza Mahakama ya Tanzania kwa kuliamini Shirika la Posta na kuona tunafaa kufanya kazi kwa pamoja na tunaahidi kufanya kazi kwa uwezo zaidi ili kuendeleza ushirikiano,” alisema Bw. Gabriel. Meneja huyo alisema kuwa kufuatia unyeti wa huduma ya Posta mlangoni kwa upande wa Mahakama, Shirika hilo limeteua watu maalum kila mkoa ambao kazi yao maalum ni kushughulikia huduma ya Posta Mlangoni Mahakamani.
Aidha; Bw. Gabriel aliwakumbusha Watumishi wa Mahakama kuchukua taarifa sahihi za mawasiliano ya Wateja wanaofika Mahakamani kwani inasaidia kuwafikia walengwa bila usumbufu wowote.


Bw. Gabriel aliongeza kuwa wamejipanga vyema katika utekelezaji wa kazi hiyo, ambapo alifafanua kuwa kabla ya kuwafikishia wateja barua na nyaraka mbalimbali zitokazo Mahakamani, nyaraka hizo husajiliwa/huingizwa kwenye mfumo wa kompyuta kwa ajili ya kumbukumbu na ufuatiliaji wa karibu zaidi. Mahakama ya Tanzania inaendelea na Utekelezaji wa Mpango Mkakati wake ambao umelenga katika kukidhi na kufikisha huduma za Mahakama kwa wananchi na vilevile kupandisha kiwango cha Wananchi kuridhika  na  huduma zitolewazo na Mahakama kwa kupungua  malalamiko mbalimbali yanayoelekezwa kwa Mhimili huu. Kufuatia hili, Mahakama imefanya na inaendelea kufanya maboresho mbalimbali ya huduma zake yote yakiwa na lengo la kuwafikia wananchi na Wadau wote wa Mahakama kwa ujumla.

No comments: