Advertisements

Friday, December 28, 2018

Waziri Mhagama aitaja Mikoa 11 vinara kwa Mabaraza ya Biashara

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akisisitiza jambo wakati alipokutana na wajumbe wa Baraza la Biashara Mkoa wa Kigoma, wakati alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa, kulia kwake ni Mkuu wa mkoa huo, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga, Katibu Tawala wa mkoa huo, Rashid Mchata na Mkuu wa Wilaya  ya Kigoma, Samson Anga.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akimsikiliza Katibu Tawala wa Mkoa Kigoma, Rashid Mchata, akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Baraza la Biashara la mkoa huo, wakati Waziri alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa,
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akimsikiliza Mratibu wa Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (LIC), Andrew Mhina akiwasilisha taarifa ya utekelezaji wa Mradi huo mkoani Kigoma, wakati Waziri alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiongea na Mjasiriamali aliyekuwa akihudumiwa  katika kituo cha Biashara (One Stop Business Center) wilayani Kigoma, wakati alipofika mkoani Kigoma kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Kazi, Ajira, Vijana na Watu Wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya Wajumbe wa Baraza la Biashara la Mkoa wa Kigoma, wakati Waziri alipofika mkoani humo kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Biashara la Taifa
Na. OWM, Kigoma.
Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Mhe. Jenista Mhagama (Mb), ameitaja mikoa 11 ambayo ilianzisha mabaraza ya Biashara na hadi sasa yako hai na kubainisha kuwa mikoa mingine ilitekeleza agizo la kuanzisha mabaraza hayo tu lakini utendaji wa Mabaraza hayo umekuwa siyo endelevu.
Waziri Mhagama ameitaja Mikoa hiyo 11 ambayo Mabaraza yake yako hai hadi sasa kuwa  ni Dodoma, Kigoma, Tanga, Geita, Morogoro, shinyanga, Dar es Salaam, Pwani, Iringa, Songwe na Mbeya. Aidha, Mhagama amebainisha kuwa Mikoa mingine ambayo mabaraza yake hayafanyi vikao inakiuka Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 unaosisitiza kuanzishwa kwa mabaraza hayo na utendaji wake kuwa endelevu.

Akiongea wakati wa kufuatilia utekelezaji wa shughuli za Baraza la Taifa la Biashara mkoani Kigoma, Waziri Mhagama alifafanua kuwa Dhumuni kuu la kuanzisha mabaraza ya biashara hususani katika ngazi ya wilaya na mikoa ni kuweka mfumo rasmi wa kuwakutanisha viongozi wakuu wa Serikali na Sekta Binafsi katika kila ngazi ya utawala, kujadiliana jinsi ya kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini kwa ajili ya kukuza sekta binafsi ambayo ndio muhimili muhimu wa kukuza  uchumi wa nchi.

“Hatuwezi kuwa tunamshuhudia Mhe. Rais wa awamu ya tano Dkt. John Pombe Magufuli anaitisha vikao vya Baraza la Taifa la Biashara  katika ngazi ya Taifa lakini katika ngazi ya mkoa na wilaya hamtekelezi maagizo hayo, lazima mabaraza yakutane ili kutatua kero za wafanyabiashara na wawekezaji katika ngazi ya mkoa na wilaya, lakini pia itasaidia kuibua fursa za uwekezaji na kuzinadi fursa hizo, na sisi tumeamua kukagua mkoa mmoja baada ya mwingine ili kupunguza kero za wafanya biashara na wawekezaji” Amesema Mhagama

Wakiongea kwa nyakati tofauti wakati Waziri Mhagama alipokutana na Wajumbe wa Baraza la Mkoa la Biashara, Mkuu wa mkoa wa Kigoma, Brigedia Jenerali Mstaafu, Emmanuel Maganga , Mkuu wa wilaya ya Kigoma, Samson Anga na Katibu Tawala wa Mkoa huo, Rashid Mchata, walieleza kuwa  kupitia Mradi wa Kuboresha Mazingira ya Biashara na Uwekezaji (LIC), wameweza kuimarisha mfumo wa majadiliano kati ya serikali na sekta binafsi  kupitia Mabaraza ya Biashara ya Mikoa na Wilaya.
Naye Mratibu wa Mradi huo, Andrew Mhina alibainisha kuwa Mradi huo unalenga kuhakikisha kuwa unaboresha mazingira ya Biashara na  uwekezaji nchini tayari kwa kushirikiana Baraza la Taifa la Biashara wameandaa mwongozo wa Majadiliano Kati ya Serikali na Sekta Binafsi ngazi ya Mkoa na Wilaya ili kuyajengea uwezo Mabaraza ya Mikoa yaweze kuwa endelevu na yenye ufanisi.

Baraza la Taifa la Biashara lilianzishwa kwa Waraka wa Rais Na. 1 wa mwaka 2001 na kuchapishwa kwenye Gazeti la Serikali Na. 39 la tarehe 28 Septemba 2001.  Baraza hilo  ni jukwaa la majadiliano kati ya Sekta ya Umma  na Sekta Binafsi, na lengo kuu la Baraza ni kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji kwa njia ya majadiliano kati ya sekta ya umma na sekta binafsi.Aidha Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Biashara ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

No comments: