Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Ndesamburo alalamika chopa kuzuiwa Kwenda kwa Babu

Mbunge wa Moshi Mjini, Philemon Ndesamburo (Chadema), ameiomba serikali kuangalia uwezekano wa kuondoa zuio la helkopta kuruka kwenda katika kijiji cha Samunge, Loliondo wilayani Ngorongoro nyumbani kwa Mchungaji Ambilikile Mwasapile, kupeleka wagonjwa kupata tiba.
Taarifa iliyotolewa na Ndesamburo na kusainiwa na Katibu wake, Basili Lema, hatua ya Mamlaka ya Anga kuweka zuio kwa ndege (helkopta) kuruka kwenda Samunge ni kuwaumiza wananchi kwani kwa sasa hali ya barabara si nzuri, hivyo usafiri ulio mzuri ni wa njia ya anga.

 “Usafiri wa barabara kuelekea kwa Babu Samunge, umekuwa mgumu sana kutokana na mvua zilizonyesha karibuni na pia msongamano mkubwa wa wagonjwa wanaokwenda kijijini humo kupata uponyaji, njia ya anga ndio ingekuwa rahisi na salama zaidi na kwamba zuio hilo limefanyika bila kuwahusisha wadau,” alisema.
 “Inafahamika kote ulimwenguni kuwa helkopta ni kifaa kinachotumika zaidi kwa shughuli za uokoaji. Kule Samunge hali ni mbaya watu
wanahitaji kuokolewa katika hatari, watu wanahitaji chakula cha haraka, kifaa muhimu cha kuwaokoa ni helkopta,” taarifa hiyo ilieleza.
Alisema wanatambua kuwa wapo watu waliozidiwa sana ambao wanahitaji kuchukuliwa haraka na kurejeshwa hospitali na njia pekee ya kuwasaidia ni ndege.
Kuna maiti ziko kule, maiti hizi zimekutwa na mauti baada ya kukosa huduma muda mrefu, sasa kwa mila na tamaduni zetu Afrika ni lazima tuwape heshima marehemu wetu, tunalazimika kuwahifadhi kwa heshima na hatimaye tuwasindikize katika safari yao ya mwisho katika mazishi,” ilieleza sehemu ya taarifa hiyo.
Alisema wakati serikali ikitoa tamko la kuzuia safari za barabarani na angani kwenda Samunge, kampuni ya Key’s Aviation ilikuwa ina order (maombi) nyingi za kuwapeleka wagonjwa ikiwa ni pamoja na kuomba kupeleka dawa kwa ajili ya kuhifadhi maiti ya mzazi wa mmoja wa watumishi wa serikali na kumchukua mgonjwa mmoja aliyezidiwa sana.
 MAGARI YASOGEA MTO WA MBU
Katika hatua nyingine,  magari yaliyokwama juzi katika eneo la Meserani, Monduli baada ya kuzuiwa na Jeshi la Polisi, jana yaliruhusiwa kusogea hadi Mto wa Mbu kwa ajili ya kupata huduma muhimu za kiafya, zilizoandaliwa na serikali kwa ajili ya  wagonjwa wanaozidiwa.
 Magari hayo yanayokadiriwa kufikia kuwa ni zaidi ya 85 yakiwa na watu zaidi ya 300, yalionekana yakiwa kwenye foleni katika kijiji cha Losirwa, ambako kuna geti kubwa la kuingilia kwa  Mchungaji Mwasapile.
Mkuu wa Wilaya ya Monduli, Jowika Kasunga, alisema eneo hilo ndipo serikali ilipoamua kuwa na kizuizi kikubwa na magari yote kutoka pande zote yatakuwa yanafikia hapo na kupata namba za kuingia kwa Mchungaji Mwasapile.
Alisema serikali imeamua kutenga eneo hilo kwa sababu ndipo eneo muhimu lenye huduma muhimu za binadamu na tayari imepeleka mahema makubwa ya kujenga vituo maalum vya kutolea matibabu kwa wagonjwa watakaozidiwa wakati wakisubiri foleni ya magari yao kuruhusiwa kwenda Samunge.
Hapa tutatoa magari kwa namba maalum na siyo bora kila gari kwenda bila mpango na imekuwa ngumu serikali kuwazuia wagonjwa hawa kwa sababu wanatoka mbali mtu anakuambia siwezi kurudi Mbeya bora nikae hapa nisubiri foleni hivyo tumeamua bora tusimamie zoezi hili la kutoka magari hapa,” alisema Kasunga.
Alisema njia za panya kwa sasa hawataweza kuzidhibiti, lakini wanaamini muda unavyokwenda na utaratibu wa kutoa namba kwa magari yanayokwenda kwa mchungaji ukiimarika, watakosa huduma kwa Babu na wataacha kuingilia njia hizo na kufuata utaratibu uliopangwa.
Mtendaji wa Kijiji cha Losirwa, Faraji Shabani, alisema kijiji kimewapokea watu hao tangu jana na wanamudu kuwapatia mahitaji muhimu.
Alisema kijiji kimewahamasisha wafanyabiashara kufanya biashara zao eneo hilo na tayari wameanza kujenga mabanda ili kutoa huduma za binadamu.
Mmoja wa wagonjwa, Claud Mashalla, mkazi wa Jiji la Mwanza, alisema amefurahishwa na uamuzi wa serikali kuwaruhusu kutoka Meserani na kusogea hadi Mto wa Mbu.
Hapa tuna imani kuwa tunafuata utaratibu, kwani tunaona magari mangapi yanatoka kwa Babu na mangapi yaruhusiwe kwenda na siyo pale Meserani tuliposimamishwa juzi na pia huduma za kiafya hazikuwepo. Hapa tunapata vyakula vya kutosha na sehemu ya kulala,” alisema Mashalla.
AFA AJALINI AKITOKA KWA BABU
Mtu mmoja amefariki dunia wakati gari alilokuwa anasafiria akitoka kupata kikombe kwa Babu kuacha njia na kupinduka ndani ya Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.
Kamanda wa Polisi mkoani Mara, Robert Boaz, alithibitisha kutokea ajali hiyo juzi saa 5:30 asubuhi katika eneo la kijiji cha Namibu kata ya Neruma wilayani Bunda wakati gari likitoka Loloindo kwa Babu.
Ndani ya gari hilo kulikuwa na watu zaidi ya 10 na liliacha njia na kupinduka, ambapo tisa walijeruhiwa na mmoja akapoteza maisha muda mfupi baada ya kufikishwa hospitalini.
Kaimu Mganga Mkuu wa Hospitali Teule ya Wilaya ya Bunda, Dk. Said Karamba, alimtaja marehemu kwa jina la Hamad Abdallah (32), mkazi wa jijini Mwanza.
MCHUNGAJI AMPIGIA DEBE BABU
Jijini Dar es Salaam, Mchungaji Alphonce Temba wa Kanisa la Huduma  ya Penuel Healing Ministry ya Kibangu, amewataka Watanzania wanaoenda Loliondo kunywa dawa ya Mwasapile kuzingatia masharti ili wapone.
Akizungumza na waandishi wa jana, Temba alisema dawa hiyo inaponyesha kwa imani hivyo inapasa watu wote wanaoenda kuinywa kuzingatia masharti ya Babu ili wapone.
Dawa hii inahusu imani zaidi hivyo nawataka watu wote ambao wanakunywa dawa hii bila kuzingatia masharti kamwe wasitegemee kupona,” alisema Temba.
Alifafanua kuwa wachungaji wengine wamekuwa wakipinga huduma hiyo ila lazima wakumbuke kuwa ni wagonjwa hao hao ambao wamesali kwenye makanisa yao kwa muda mrefu bila kupona ndio waliokwenda kwa Babu kunywa dawa na sasa ni wazima.
Imeandikwa na Salome Kitomari, Moshi, Cynthia Mwilolezi, Arusha, Rosemary Masanja, Dar na Ahmed Makongo, Bunda.
CHANZO: NIPASHE

No comments: