Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

TP Mazembe kutua Dar keshokutwa

Wakati mabingwa mara mbili mfululizo wa Ligi ya Klabu Bingwa Afrika, timu ya TP Mazembe kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ikitarajiwa kutua nchini keshokutwa Ijumaa, kiingilio cha chini katika mechi yao ya marudiano dhidi ya Simba itakayochezwa Jumapili kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam kimetajwa kuwa ni Sh. 5,000.
Tiketi za kiingilio hicho zitatolewa kwa mashabiki watakaoketi kwenye viti vya rangi za kijani na bluu na mechi hiyo itachezwa kuanzia 9:30 alasiri.

Akizungumza jijini Dar es Salaam jana, Afisa Habari wa Simba, Clifford Ndimbo, alisema kuwa maandalizi ya mechi hiyo yanaendelea vizuri ambapo mechi ya Ligi Kuu ya Tanzania Bara waliyocheza jana dhidi ya Kagera Sugar waliichukulia pia kuwa ni sehemu ya maandalizi yao.
Ndimbo alisema kuwa hadi jana mchana, wapinzani wao hawakuwa wamewapa kwa maandishi taarifa za ujio wao na idadi ya wachezaji watakaokuja nao nchini.
"Ila kwa mujibu wa kanuni, tayari tumeshawaandalia Mazembe hoteli ya kufikia na sisi pia tuko katika hali nzuri na tunasubiri siku hiyo ya mechi ifike," alisema Ndimbo.
Aliongeza kuwa kiingilio cha juu katika mechi hiyo kitakuwa Sh. 40,000 kwa mashabiki watakaokaa kwenye viti vya VIP A, Sh. 20,000 kwa VIP B na Sh. 10,000 kwa watakaokata tiketi za eneo la VIP C.
Alisema vilevile kuwa tiketi za viti vya rangi ya machungwa zitauzwa kwa Sh. 8,000 na uuzwaji wa tiketi zote utaanza leo katika vituo mbalimbali jijini Dar es Salaam.
Aliongeza kuwa kurejea kwa kocha wao Mzambia Patrick Phiri, kumeimarisha ari katika kikosi chao ambapo wamejipanga kuhakikisha wanaweka rekodi kwa kulipiza kisasi cha kufungwa 3-1 katika mechi yao ya kwanza waliyocheza ugenini kwenye Uwanja wa Stade de la Kenya mjini Lubumbashi na kuwaondoa mabingwa hao watetezi.
Alisema kuwa waamuzi wa mechi hiyo ambao wanatoka Shelisheli, watawasili nchini kesho pamoja na kamisaa ambaye atatoka Kenya.
Daktari wa Simba, Cosmas Kapinga alisema kuwa wachezaji ambao hawatacheza Jumapili kutokana na majeraha ni Joseph Owino, Hillary Echessa na Uhuru Selemani.
Kapinga alisema kuwa hatma ya Amri Kiemba kuhusiana na mechi hiyo itajulikana Ijumaa baada ya kufanyiwa uchunguzi wa mwisho.
Ili Simba wasonge mbele na kuwaondoa Mazembe, watalazimika kushinda walau 2-0 dhidi ya wanafainali hao wa Kombe la Dunia la Klabu la FIFA.
CHANZO: NIPASHE

No comments: