Advertisements

Wednesday, March 30, 2011

Urais watesa vijana wa CCM

  Sasa waanza vita vya kikanda
  Arusha wawalaani wa Pwani 
  Wamtoa mwenzao kafara
Chama cha Mapinduzi (CCM)

Tetesi na hisia za mbio za urais mwaka 2015 zinaelekea kuzidi kuugawa Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) na sasa matamko ya vikao tofauti vya mabaraza ya mikoa miwili yanashutumiana kwa madai ya kuhubiri siasa za kibaguzi kuhusu urais.
Baraza la UVCCM Mkoa wa Arusha limesema limesikitishwa sana na kauli zilizotolewa na baadhi ya vijana wa UVCCM Pwani wakianza kuhubiri siasa ya kibaguzi wa makabila kwa kutoa matamko kwamba Rais wa Tanzania katika Uchaguzi Mkuu wa 2015 asitoke Kanda ya Kaskazini.

Baraza linachukua fursa hii kuwaonya vijana wenzetu hao wanaopotoka na labda kama ambavyo wamekumbushwa juzi, tuwaambie tena kwamba Rais wa awamu ya kwanza Marehemu Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alitokea Mkoa wa Mara (Kanda ya Ziwa), Rais wa awamu ya pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi alitokea Zanzibar (Visiwani), Rais awamu ya tatu Mhe. Benjamin William Mkapa alitokea Mtwara (Kanda ya Kusini) na Rais wetu wa sasa Mhe. Jakaya Mrisho Kikwete anatokea mkoa wa Pwani (Kanda ya Pwani),” lilieleza tamko lililotolewa na Mweneykiti wa UVCCM Mkoa wa Arusha, James Ole Millya juzi usiku mjini Longido na kuongeza:
Sasa kama hawa vijana wenzetu wangetaka Watanzania wafanye uchaguzi kwa kuangalia maeneo ambayo viongozi hao wanatoka, basi tungetegemea waseme sasa kwamba 2015 ni zamu ya Rais kutokea Kanda ya  Kaskazinui au, Nyanda za Juu Kusini, na tunaamini kote huku kuna viongozi mahiri na makini wenye uwezo wa kuongoza nchi vizuri kabisa.
“ Lakini sisi kama vijana weledi wa CCM na tuliolelewa vizuri kwenye misingi thabiti ya nchi yetu ya umoja na amani, hatuamini hata siku moja kwenye kuchagua viongozi kwa kuangalia rangi, dini au kabila.”
Tamko hilo lilieleza kuwa  Hayati Mwalimu Nyerere alishaonya kwa ukali sana kuhusu ubaguzi wa aina yoyote. “Sisi tunaamini kila raia wa Tanzania kutokea upande wowote ule wa nchi anayo haki ya kikatiba ya kuwania nafasi ya urais na wananchi wa Tanzania watampima kwa rekodi yake ya uongozi na uwezo wake wa kutatua matatizo ya wananchi, hii ndiyo Tanzania tunayoifahamu sisi kama vijana wa Chama Cha Mapinduzi,” tamko hilo lilieleza.
Tamko hilo limefuatia tamko la UVCCM Mkoa wa Pwani lililotolewa na Mwenyekiti wake, Abdallah Ulega, likiwashutumu mawaziri wawili wastaafu, Frederick Sumaye na Edward Lowassa, kwamba wanatoa kauli za kukosoa chama na serikali nje ya vikao rasmi.
Ulega alisema wanasiasa hao wana malengo yao ya kisiasa ya mwaka 2015.
Ingawa tamko la UVCCM Arusha halikutaja majina ya wanasiasa wa Kanda ya kaskazini ambao walilengwa na tamko la vijana wa Mkoa Pwani, lakini Sumaye na Lowassa wote wanatoka Kanda ya Kaskazini katika mikoa ya Manyara na Arusha.
KADA AUNDIWA ZENGWE 
Katika hatua nyingine, Mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM Taifa, Mrisho Gambo, amevuliwa wadhifa wa ujumba wa Baraza Kuu la jumuiya hiyo Wilaya ya Arusha kwa tuhuma mbalimbali zikiwemo za kukihujumu CCM katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana.
Uamuzi huo ulifikiwa juzi katika kikao cha Baraza Kuu la UVCCM Mkoa wa Arusha ambacho pia kilipendekeza kwa vikao vya juu vya chama hicho kumvua nyadhifa nyingine alizonazo katika CCM.
Millya alisema kuwa kikao hicho kwa kauli moja kimefikia maamuzi hayo kutokana na kuridhishwa na ushahidi uliopo wa kimazingira na wa watu wanaozungumza juu ya hujuma hizo dhidi ya Gambo.
Dalili za kutimuliwa kwa Gambo zilianza kuonekana mapema kabla kikao hicho kuanza kutoka ma msimamo waliokuwa nao wapambe wa kundi linalodaiwa kutoafautiana kimsimamo na Gambo.
Gambo anadaiwa kueneza maneno ya kashfa dhidi ya aliyekuwa mgombea ubunge wa CCM katika Jimbo la Arusha Mjini, Dk. Batilda Buriani, ambaye aliangushwa na mbunge wa sasa kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Godbless Lema.
 Millya alisema ushahidi huo ni pamoja na kauli alizokuwa akizitoa Gambo kwa watu yakiwemo matusi ambayo alidai hawezi kuyatamka kuhusu sababu zilizomsababisha Gambo asimpigie kampeni Dk. Burian.
Millya alisisitiza kuwa kikao hicho kina uwezo wa kikatiba kumuondoa mjumbe huyo katika nafasi yake hiyo na kuongeza kuwa kwa nafasi zingine za juu alizonazo ikiwemo ya ujumbe wa Baraza la Taifa la UVCCM na kwamba wanaandaa barua ya mapendekezo kwa Kamati ya Utekelezaji ya Taifa.
Hatuna imani naye tena na kamwe hatuwezi kukubali kukaa na nyoka, tunaandaa barua kuwasilisha katika vikao vya ngazi ya juu,” alisema Millya.
Alisema kamwe UVCCM haiwezi kuendelea kuwalea vijana na wanachama wanaoonekana kuwa ndumilakuwili na ni vyema kuwatimua ili kama wanataka kuvisaidia vyama vya upinzani waende upinzani moja kwa moja badala ya kuwa vigeugeu.
Akizungumzi hatua hiyo kwa njia ya simu, Gambo aliendelea kuwa na msimamo wake kwamba kamwe hawezi kuwa mnafiki kwa kutaka kutetea baadhi wana-CCM aliodai kuwa wanakisababishia chama hicho kuchukiwa na wananchi kutokana na kukosa maadili.
Kama ilivyo kwa katiba ya chama chetu kwamba nitasema kweli daima fitina kwangu ni mwiko na kamwe sitaweza kuendelea kufikiria kwa kutumia tumbo badala ya kutumia kichwa,” alisema akisisitiza kauli aliyonukuliwa akiitoa katika kikao cha Baraza Kuu la UVCCM mjini Dodoma hivi karibuni wakati akiwasema baadhi ya vigogo waandamizi wa CCM wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Alisema kuwa suala hilo anatarajia kuliweka kwa kina hadharani kesho katika kikao na waandishi wa habari na kudokeza kuwa hatua iliyochukuliwa na kikao cha Longido ni shinikizo la kigogo mwenye nguvu kubwa ndani ya chama hicho mkoani Arusha. Hakutaja jina.
Alidai kuwa kupitia shinikizo hilo, wajumbe wanne wa kikao hicho (majina tunayo) walikutana katika Hoteli ya Mount Meru Jumapili iliyopita majira ya usiku na kuandaa tamko hilo ambalo linadaiwa lilivuja na kusambaa kabla hata ya kikao hakijaisha.
Gambo alisema anachofahamu vijana hao waliotoa maazimio hayo dhidi yake wanasumbuliwa na uchanga katika siasa unaosababishwa na kutofahamu kanuni na kueleza kuwa hali hiyo itawatoka pale watakapokua kisiasa.
Alidai kuwa siyo kweli kwamba kutimulikwa kwake kumetokana na kuhujumu chama hicho wakati wa uchaguzi, bali kunatokana na msimamo wake kuhusiana na mwenendo wa baadhi ya wanachama ndani ya chama hicho katika mkoa wa Arusha.
Katika kikao cha Baraza Kuu wa UVCCM Taifa inadaiwa kuwa Gambo alitoa maneno makali kuhusiana na baadhi ya vigogo wa chama hicho akitaka wafukuzwe kutokana kashfa ya Richmond na Dowans.
Akifunga kikao hicho, Millya alisema vijana wanapaswa kuwa wakweli wakati wote katika kuzungumzia masuala yanayohusu taifa pasipo kuvunja taratibu, sheria na kanuni za nchi wakati wa kutoa maoni yao.

SITTA BADO ATIKISA UVCCM TABORA

Katika hatua nyingine, UVCCM Mkoa wa Tabora wameshauriwa kuacha kulumbana, badala yake wakae chini kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa mgogoro unaowakabili kupitia vikao halali vya jumuiya yao.
 Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tabora jana, Mjumbe wa Mkutano Mkuu wa Mkoa wa Tabora, Alli Mwantende, alisema kuwa suluhisho la mgogoro wao wa kumvua ulezi wa UVCCM wa mkoa huo, Mbunge wa Urambo Mashariki, Samuel Sitta, utamalizwa kwa njia ya vikao.
 Alisema baada ya kutolewa kwa tangazo la kuvuliwa kwa  Sitta, lililotolewa na Mwenyekiti UVCCM Mkoa wa Tabora, Robert Kamoga, yamezuka malumbano makubwa.
 Alisema tayari vijana katika ngazi ya wilaya na mkoa wametoa matamko ya kuikana kauli hiyo ya mwenyekiti na kudai kuwa inakwenda kinyume cha kanuni za umoja huo na kwamba imelenga kumdhalilisha Sitta ambaye ni Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
 Alisema Sitta ni kiongozi mwandamizi na mwadilifu kwani ameweza kushika nyadhifa mbalimbali kama uspika, uwaziri na ubunge na kwamba akiwa kada wa CCM, amekuwa akitoa michango mbali mbali kwa umoja huo.
 Alisema kinachotakiwa sasa ni vijana kuitisha kikao cha Kamati ya Utekelezaji cha mkoa kisha Baraza Kuu la Mkoa huo ili kuwatambua viongozi walioleta chokochoko ndani ya umoja huo na kuchukua hatua ili kumaliza mtafaruku huo.
 Alisema njia pekee ya kumaliza mzozo huo ni kuitisha vikao hivyo vya kikatiba ambavyo vitakuwa na mamlaka ya kisheria ya kuweka mustakabali wa vijana katika mkoa huo.
CHANZO: NIPASHE

No comments: