ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, January 27, 2019

Kiunzi Kazi Uimarishaji Ubora Huduma za Jamii Chazinduliwa

 Meneja wa Mradi wa Wauguzi kutoka shirika American International Healthy Alliance Eliarehema Ayo akitoa neno wakati wa uzinduzi wa Kiunzi kazi cha ubora wa huduma za Afya leo Jijini Dodoma.
 Baadhi ya wajumbe wakimsikiliza Mkurugenzi wa Uhukiki wa  Ubora Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mohamed Mohamed (hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa kiunzi kazi leo Jijini Dodoma.
 Mkurugenzi wa Uhukiki wa  Ubora Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mohamed Mohamed akizungumza na wajumbe (hawapo pichani)wakati wa uzinduzi wa kiunzi kazi cha ubora wa Huduma za Afya
 Mkurugenzi wa Uhukiki wa  Ubora Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mohamed Mohamed akionyesha kiunzi kazi  cha ubora wa huduma za afya  kilichozinduliwa leo , Jijini Dodoma.
Mkurugenzi wa Uhukiki wa  Ubora Huduma za Afya kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Mohamed Mohamed akizindua kiunzi kazi cha ubora wa huduma za afya  kilichozinduliwa leo  mbele ya wadau wa Afya, Jijini Dodoma.


Angela Msimbira&Majid Abdul Karim
Mkurugenzi  wa uhakiki wa ubora wa huduma za afya  kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia , Wazee na Watoto Dkt. Mohamed Mohamed amezindua kiunzi kazi uimarishaji ubora huduma za jamii katika mkutano uliofanyika kwenye ukumbi wa Dodoma Hotel Jijini Dodoma.
Akizindua kiunzi kazi hicho Dkt. Mohamed amesema kiunzikazi hicho itakua ni nyenzo muhimu katika kutoa huduma bora na za wakati kuanzia kwenye ngazi ya msingi.
“ kukamilika kwa Kiunzikazi  hiki kitasaidia kutoa muongozo wa huduma za afya katika ngazi ya jamii kwa kufuata miongozo na viwango vinavyotakiwa na hivyo kusaidia kuboresha Afya ya jamii yetu kwa ujumla” alisema Mohamed.
Ameongeza kuwa Kiunzi kazi hiki pia kitawasaidia watoa huduma ngazi ya jamii kutoa huduma bora ambazo  zinamlenga mwananchi moja kwa moja kabla hajafikia kwenye ngazi ya kituo cha Afya au Zahanati.
Aidha alisema “huduma hizi za afya ya msingi kwa kipindi kirefu  zimekuwa zikitolewa bila kufuata utaratibu na pia watoaji wa huduma hizo hawakuwa hawakuwa na misingi na kanuni zinazowaongoza wao katika kuihudumia jamii; Lakini kwa kuwa Serikali yetu ni makini iligundua pengo  lililokuwepo na kwa kushirikiana na wadau kwa pamoja tukaandaa Kiunzikazi cha Uimarisha Ubora huduma za Jamii katika jamii yetu.
“Wote tunafahamu kuwa magonjwa mengi yanaanzia ngazi ya jamii yaani kwenye mtaa au kwenye kijiji sasa kupitia mpango huu ambao utaongozwa na Kamati ya Afya ya Mtaa/Kijiji itasaidia kudhibiti magonjwa yanayoweza kutokea katika Jamii” alisema Mohamed. 
Dkt. Mohamed ametoa wito kwa wadau, wataalamu wa huduma za afya na jamii kwa ujumla kutoa ushirikiano katika kutekeleza majukumu yao kwa kutumia kiunzi kazi hicho ili kuleta matokeo chanya katika utoaji huduma bora za afya katika ngazi ya jamii.
Kwa upande wake Afisa Muuguzi Mkuu Lucy Robby Issarow amesema kuwa kiunzi hicho kinalenga kumpa mteja uhakika wa kupata huduma bora kabla ya kufikia kwenye ngazi ya vituo vya afya na hospitali za Wilaya. 
“Tumekuwa na kamati za Afya kwenye zahanati, vituo vya Afya na mpaka kwenye hospital kaini kamati hizo hazikuwahi kuwepo kwenye jamii sasa ndio tunataka ziundwe na zifanye kazi yake ipasavyo kwa kutumia kiunzi kazi kilichozinduliwa “ 
Katika uzinduzi huo Mratibu Uhakiki Ubora  Idara ya  Uhakiki Ubora Huduma za Afya Dkt.Talhiya Yahya  akiwasilisha mada ya namna kiunzi kazi kilivyoandaliwa alisema lengo la kuandaa mpango huo ni kuimarisha ubora wa huduma za Afya kwenye ngazi ya jamii na kuanisha mazingira wezeshi yatakayoiwezesha Kamati na kila mhusika aliyetajwa kufanya kazi kwa kuzingatia muongozo.
Kwa kuhitimisha Meneja wa Mradi wa Wauguzi kutoka Shirika la American International Health Alliance (AIHA) Eliaremisa Ayo ametaka yale yaliyoandikwa kwenye kiunzi kazi yakatekelezwe kwa ufanisi  na sio kuweka mpango huo kabatini kama nyaraka tu bila kuifanyika kazi . 

No comments: