Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa (wa kwanza kutoka kulia) akizungumza kuhusu masuala ya Watu wenye Ulemavu alipofanya ziara Wilaya ya Kongwa kukagua utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deogratius Ndejembi akitoa taarifa ya utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu kwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa.
Daktari wa Mazoezi ya Viungo kutoka Kituo cha Utengamao Mlali, Dkt. Nshashuku Joseph akimwelezea Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa aina ya mazoezi wanayoyatoa kwa Watoto wenye ulemavu wa viungo. (katikati) ni Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deogratius Ndejembi.
Baadhi ya wazazi wakimsikiliza Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia (Wenye Ulemavu) Mhe. Stella Ikupa (hayupo pichani) alipotembelea Kituo cha Utengamano kilichopo Mlali, Wilaya ya Kongwa.
NA; OWM (KVAU) - KONGWA
Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia masuala ya Watu wenye Ulemavu, Mhe. Stella Ikupa ameridhishwa na utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu katika Wilaya ya Kongwa.
Hayo ameyasema wakati wa ziara yake katika wilaya hiyo kuangalia hali ya utekelezaji wa masuala ya Watu wenye Ulemavu.
Akitoa pongezi hizo, Naibu Waziri, Ikupa alisema kuwa ushirikishwaji wa kundi hilo maalum ni jambo la msingi katika kuhakikisha haliachwi nyuma kwenye nyanja mbalimbali za maendeleo.
“Endeleeni kuwajali na kuweka mipango thabiti yenye kuhakikisha watu wenye ulemavu wanapata haki sawa kama wengine,” alisema Ikupa.
Pia, aliipongeza wilaya ya kongwa kwa kusaidia Watu wenye Ulemavu kuhudhuria maadhimisho mbalimbali ya Kitaifa yanayofanyika hapa nchini.
“Matukio hayo yamekuwa yakiwapa hamasa kubwa na kuona fursa ambazo zinaweza kuwasaidia kujikwamua kiuchumi,” alieleza Ikupa
Aidha, Mhe. Ikupa alitoa rai kwa Watu wenye Ulemavu kuwa wabunifu na kuweza kutambua fursa kutokana na mazingira waliyopo na kuzitumia kujiongezea kipato.
Hata hivyo, Naibu Waziri Ikupa alihimiza uboreshwaji wa miundombinu rafiki zitakazowesha kundi hilo, kuelimisha jamii juu ya haki za watu wenye ulemavu, uundwaji wa kamati za kuhudumia kundi hilo maalum na kuwapatia taarifa watu wenye ulemavu kuhusu fursa za mikopo zinazotolewa na halmashauri, ajira na upatikanaji wa dawa, mafuta ya wenye ualbino na vifaa saidizi.
Naye, Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, Mhe. Deogratius Ndejembi alimshukuru Mhe. Ikupa kwa kufanya ziara Wilayani humo, na kuahidi kuendelea kutoa huduma kwa kundi hilo maalum ikiwemo asilimia 2 ya mapato ya ndani ya halmashauri zinatengwa na kutoa mikopo kwa Vikundi vya Watu wenye Ulemavu, pia kuhakikisha kamati za Watu wenye Ulemavu zinaundwa katika kila Kijiji na kufanya kazi kulingana na miongozo.
Katika ziara hiyo Naibu Waziri, Ikupa alitembelea Kituo cha Utengamao kilichopo Mlali na Shule maalum Kongwa Kitengo cha Viziwi. Pia alitembelea Wilaya ya Mpwapwa, Shule ya msingi Chazungwa na Mpwapwa Sekondari ambazo zina wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
MWISHO
No comments:
Post a Comment