
Mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana hotuba ya bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020 jana Jumanne Juni 18, 2019 katika mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka
Dodoma. Naibu Spika wa Bunge la Tanzania, Dk Tulia Ackson amesema wabunge wa upinzani ambao hawajaridhishwa na uamuzi wake kuhusu mbunge wa Kasulu Vijijini (CCM), Augustine Vuma aliyechana hotuba ya bajeti mbadala ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni mwaka 2019/2020, waandike barua kwa katibu wa Bunge kwa mujibu wa kanuni za chombo hicho cha kutunga sheria.
Dk Tulia ametoa kauli hiyo leo Jumatano Juni 19, 2019 bungeni jijini Dodoma wakati akijibu mwongozo wa kaimu mnadhimu wa kambi hiyo, Joseph Selasini aliyetaka Vuma kuomba radhi na kupelekwa katika kamati ya maadili ya Bunge.
Katika ufafanuzi wake, Dk Tulia amesema Vuma hawezi kupelekwa katika kamati hiyo kwa kuwa kipindi cha nyuma mbunge wa Bunda (Chadema), Ester Bulaya aliwahi kurusha vitabu bungeni na kuvichana lakini hakupelekwa katika kamati hiyo.
Jana jioni Jumanne Juni 18, 2019 wakati wa mjadala wa bajeti ya Serikali mwaka 2019/2020, Vuma alichana kitabu hicho na kusema kina maneno yasiyofaa na kinafaa kuchanwa na kisha kukichana.
Kitendo hicho kilisababisha zogo bungeni na mbunge wa Tunduma (Chadema), Frank Mwakajoka kutoa taarifa akitaka Vuma kuomba radhi, na Dk Tulia kumtaka mbunge huyo kufanya hivyo kwa kauli aliyoitoa wakati akichana kitabu husika, si kwa kitendo chake cha kukichana.
Uamuzi huo haukuwapendeza wabunge wa upinzani na kulalamikia jambo hilo kitendo kilichosababisha Dk Tulia kuwatoa nje ya ukumbi wa Bunge wabunge wa Chadema, Esther Matiko (Tarime Mjini), John Heche (Tarime Vijijini) na Dk Emmaculate Sware (Viti maalum).
No comments:
Post a Comment